Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Rwanda/DRC: Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa akaribisha makubaliano amani

**Watu Waliopoteza Makazi Wakimbia Kupitia Jiji la Goma kufuatia kusonga mbele kwa makundi ya waasi (Maktaba)
WFP
**Watu Waliopoteza Makazi Wakimbia Kupitia Jiji la Goma kufuatia kusonga mbele kwa makundi ya waasi (Maktaba)

Rwanda/DRC: Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa akaribisha makubaliano amani

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, jana Ijumaa Juni 27 amekaribisha kutiwa saini kwa makubalino ya amani kati ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Rwanda, yaliyoratibiwa na Marekani, akiyataja kuwa hatua muhimu katika kupunguza mvutano wa kikanda na kuelekea kwenye amani na utulivu wa kudumu.

Mkataba huo ulisainiwa Ijumaa mjini Washington, D.C., na unalenga kupunguza mvutano katika mashariki mwa DRC na ukanda mzima wa Maziwa Makuu. Guterres amesema kutiwa saini kwa mkataba huo ni hatua muhimu katika kufikia malengo ya muda mrefu ya amani na usalama kwa pande zote zinazohusika.
 

Mkataba wa mafanikio katikati ya mgogoro

 
Serikali ya DRC imekuwa ikishutumu Rwanda kwa kuunga mkono kundi la waasi la “M23” linalofanya harakati katika eneo la mashariki mwa nchi hiyo, likituhumiwa kwa ukatili dhidi ya raia na kusababisha maelfu ya watu kupoteza makazi. Rwanda imekanusha madai hayo. Kundi hilo limepata nguvu upya katika miaka ya hivi karibuni, na kuongeza mvutano kati ya nchi hizo mbili, hali iliyozua wasiwasi wa kimataifa.
 
Guterres ameisifu Marekani kwa uongozi wake katika kuratibu juhudi za upatanishi na pia akazitaja juhudi za Qatar, mpatanishi wa Muungano wa Afrika, na Rais wa Togo, Faure Gnassingbé, katika kusukuma mbele mchakato huo. Aidha, ametoa shukrani kwa mchango wa wawezeshaji watano wa pamoja walioteuliwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
 
Katibu Mkuu amezisihi pande zote kutekeleza kikamilifu mkataba huo na ahadi walizozitoa, hasa zile zilizoainishwa katika Azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa namba 2773, ikiwemo kutekeleza sitisho la mapigano na hatua zote walizokubaliana.
 
Azimio hilo linaagiza DRC na Rwanda kusitisha mapigano mara moja na linaunga mkono juhudi za kutatua mizozo yao kupitia mazungumzo ya kikanda na njia za kidiplomasia. Pia linairuhusu MONUSCO ambao ni Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini DRC  kusaidia utekelezaji wa mfumo wa usitishaji mapigano, kuwalinda raia, na kutoa msaada wa kiufundi na kimkakati kwa mchakato wa kisiasa, huku likisisitiza umuhimu wa kuheshimu sheria za kimataifa za kibinadamu, kulinda haki za binadamu, na kuzuia harakati za makundi yenye silaha kuvuka mipaka.
 

Juhudi za Kidiplomasia zavunja mkwamo

 
Mapema Ijumaa hiyo hiyo, Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu nchini DRC na Mkuu wa MONUSCO, Bi. Bintou Keita, alilihutubia Baraza la Usalama kuhusu hali ya hivi karibuni nchini humo. Alibainisha kuwa ingawa mvutano katika mashariki mwa DRC bado ni mkubwa, mchakato wa amani umefikia mafanikio muhim,  mawaziri wa mambo ya nje wa DRC na Rwanda walitia saini rasimu ya mkataba wa amani mjini Washington siku hiyo hiyo, hatua muhimu katika kusuluhisha mgogoro wa muda mrefu.
 
Bi. Keita aliisifu Marekani kwa jukumu lake muhimu katika kuwezesha makubaliano hayo na kutoa shukrani kwa Rais wa Angola, João Lourenço, na Rais wa Togo, Faure Gnassingbé, kwa juhudi zao za upatanishi. Alisisitiza umuhimu wa pande zote kuendeleza mshikamano wa kitaifa kupitia mazungumzo na kuunga mkono juhudi za maridhiano ya kitaifa zinazoongozwa na Rais wa DRC, Félix Tshisekedi, pamoja na viongozi wa dini na wanasiasa wa upinzani.