Katibu Mkuu wa UN azungumza na vyombo vya habari kuhusu Gaza
Katibu Mkuu wa UN azungumza na vyombo vya habari kuhusu Gaza
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres leo Juni 26 asubuhi ya saa za New York, Marekani ametoa wito wa dharura kwa kusitishwa kwa mapigano mara moja Gaza na kuchukuliwa kwa hatua za haraka kukabiliana na janga la kibinadamu linalozidi kuongezeka.
Akizungumza na waandishi wa habari katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani, kabla ya kuelekea Sevilla, Hispania kwa ajili ya Mkutano wa 4 wa Kimataifa kuhusu Ufadhili wa Maendeleo, ambao Umoja wa Mataifa unaandaa kwa ushirikiano na Serikali ya Hispania, Katibu MkuuGuterres amesisitiza kuwa ingawa dunia imeelekeza macho yake katika mgogoro kati ya Iran na Israel, mateso ya watu wa Palestina huko Gaza hayawezi kusahaulika.
"Makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Iran na Israel yanatoa matumaini. Na matumaini yanahitajika zaidi sasa kuliko wakati mwingine wowote," amesema. "Lakini hatuwezi kuruhusu mateso ya Wapalestina huko Gaza kusukumwa pembezoni."
Guterres amelaani mashambulizi ya Hamas ya tarehe 7 Oktoba na pia kulaani operesheni za kijeshi za Israel ambazo amesema zimesababisha “janga la kibinadamu la kutisha” ambalo amelitaja kuwa la kutisha zaidi katika historia ya mzozo huo wa muda mrefu. Amesema zaidi ya asilimia 80 ya watu wa Gaza wamepoteza makazi, wakilazimika kuishi katika eneo dogo lisilozidi moja ya tano ya ardhi ya ukanda huo sehemu ambayo bado inashambuliwa.
“Mabomu yanaanguka juu ya mahema, juu ya familia, juu ya wale wasio na pa kukimbilia,” amesema na kuongeza kamba, “watu wanauawa wakijaribu tu kutafuta chakula kwa ajili yao na familia zao.”
Amesisitiza kwamba kwa mujibu wa sheria ya kimataifa ya kibinadamu, Israel kama nguvu ya uvamizi, ina wajibu wa kuruhusu msaada wa kibinadamu kuingia. Hata hivyo, misaada inaendelea kuzuiwa. “Kwa zaidi ya miezi mitatu, vifaa vya kujenga makazi na mafuta kwa huduma muhimu vimezuiliwa. Madaktari wanalazimika kuamua nani apate dawa ya mwisho au kifaa cha kusaidia kupumua (ventilator) ya mwisho,” amesema. “Wasaidizi wa misaada nao wenyewe wanakumbwa na njaa. Hili haliwezi kuwa jambo la kawaida.”
Wiki hii, shehena ndogo ya dawa iliweza kuingia Gaza ikiwa ni misaada ya kwanza kutoka Umoja wa Mataifa kwa miezi kadhaa lakini Guterres ameonya kuwa hiyo haitoshi kabisa. “Tone la msaada linapaswa kuwa bahari,” amesisitiza.
Katibu Mkuu pia amepinga mipango mipya ya ugawaji wa misaada, akisema: “Hakuna sababu ya ‘kugundua upya gurudumu’ kwa mipango hatarishi. Tuna mpango madhubuti unaozingatia misingi ya kibinadamu… Uliwahi kufanya kazi wakati wa usitishaji wa mapigano uliopita. Lazima uruhusiwe kufanya kazi tena.”
Amewasilisha wito wa mambo matatu muhimu:
- Kusitishwa mara moja kwa mapigano Gaza,
- Kuachiliwa bila masharti kwa mateka wote,
- Upatikanaji kamili, salama na endelevu wa msaada wa kibinadamu kwa wote.
“Kwa wale walio madarakani, nasema: ruhusuni operesheni zetu kama sheria ya kimataifa ya kibinadamu inavyotaka. Kwa wale walio na ushawishi, nasema: tumieni ushawishi huo,” amehimiza. “Kwa Nchi Wanachama wote, nasema: timizeni ahadi yenu kwa Katiba ya Umoja wa Mataifa mliyorejelea jana kwa kumbukumbu ya miaka 80.”
Akihitimisha hotuba yake, Guterres amesisitiza kwamba suluhisho la kudumu ni la kisiasa. “Njia pekee ya kurejesha matumaini ni kwa kusonga mbele kuelekea suluhisho la mataifa mawili. Kidiplomasia na heshima ya utu kwa wote lazima vitawale.”