Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Elimu Jumuishi kupitia michezo: Watoto wenye ulemavu wa kuona wapate nafasi sawa

Mwanafunzi ambaye ana ulemavu wa kutoona vizuri anatumia kisoma maandishi ya nukta nundu.
© UNICEF/Hugh Rutherford
Mwanafunzi ambaye ana ulemavu wa kutoona vizuri anatumia kisoma maandishi ya nukta nundu.

Elimu Jumuishi kupitia michezo: Watoto wenye ulemavu wa kuona wapate nafasi sawa

Utamaduni na Elimu

Katika kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya viziwi wasioona, tunamulika hatua kubwa inayochukuliwa nchini Kenya katika kuhakikisha watoto wenye ulemavu wa kuona wanapata elimu bora na jumuishi. Mafunzo maalum yaliyofanyika jijini Nairobi yalileta pamoja wataalamu, walimu na mashirika ya maendeleo, kwa lengo la kuchochea elimu hiyo kwa njia ya michezo, kwa msaada wa Shirika la LEGO kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF Kenya

Peter Lothuron huyo, Mkuu wa Idara ya watu wenye ulemavu wasioona katika Taasisi ya Elimu Maalum ya Kenya (KISE), ameshiriki michezo ya kujifunza kwa vitendo pamoja na washiriki wa mkutano, wakitumia vifaa vya Nukta nundu au Braille na vinginevyo, anasisitiza kwamba michezo ni nyenzo muhimu ya mafunzo kwa watoto wote wawe na na ulemavu wa kuona au la.

Bwana Luthoron anasema “Iwe wewe ni mtu mzima au mtoto, michezo ni jambo la muhimu sana. Kwanza kabisa, inaburudisha. Na ndani ya hiyo michezo, pia unapata maarifa. Kwa hiyo, kuchanganya yote mawili ni uzoefu wa kipekee. Tusifanye mambo kuwa magumu. Tuwezeshe mafunzo haya yatiririke kwa njia ya asili kutoka kwa mwalimu hadi kwa mwanafunzi.”

Marrie Oddoux anasema kuwa Shirika lao la LEGO lilizindua vipande maalum vya michezo vinavyoitwa Braille Bricks  ambavyo vina maandishi ya nukta nundu kwa ajili ya watoto wasioona, lakini pia vinaweza kutumika na watoto wanaoona.  Kwa kutumia Braille Bricks, wana muundo wa kipekee unaofanya Nukta nundu au Braille kuwa ya jumuishi.  Kwa mujibu wa Marrie Oddoux, dhana ya ujumuishaji huo inaleta mabadiliko kwa kuwapa watoto wote nafasi sawa ya kushiriki kwa pamoja kupitia michezo… Natts Marrie Oddoux.

Margaret Nyayakio kutoka UNICEF Kenya anasisitiza kuwa teknolojia hizi mpya zinapanua ushiriki kwa watoto wenye mahitaji maalum, hasa walioko maeneo ya pembezoni kama Turkana. anasema,
“Huu ni mabadiliko makubwa katika suala la upatikanaji wa elimu jumuishi. Inafungua fursa zaidi kwa wanafunzi wenye uoni hafifu kujisikia ni sehemu ya darasa, hasa katika shule jumuishi. Inaleta nafasi ya kucheza kwa pamoja kati ya wanaoona na wasioona  na hatimaye itaathiri vyema matokeo yao ya kujifunza.”

Kwa wakufunzi kama Anab Abdi kutoka Garissa, dhamira yao ni kusambaza maarifa haya hadi mashinani ili walimu kote nchini waweze kuwafundisha watoto kwa njia jumuishi. Anasema,
“Kama mkufunzi wa wakufunzi, nitachukua maarifa niliyopata kutoka kwa mafunzo haya  hasa shughuli za ubongo ambazo zilikuwa za vitendo na kuyapeleka kwa walimu katika ngazi ya kaunti na kata ndogo.”