Je wafahamu kuhusu ulemavu wa uziwi na kutoona?

Je wafahamu kuhusu ulemavu wa uziwi na kutoona?
Leo ni siku ya kimataifa ya watu wenye ulemavu wa uziwi na kutoona, hali ya ulemavu wa pamoja wa kutoona na kutoweza kusikia au uziwi, kwa kiwango kikubwa kiasi kwamba hali hizi mbili haziwezi kufidia au kusaidiana.
Kwa sababu hiyo, ulemavu huo hutambuliwa kama ulemavu wa kipekee wenye changamoto, vikwazo na mahitaji maalum ya msaada na ujumuishaji, ambayo ni tofauti na yale yanayotolewa kwa watu ambao wana ulemavu wa kutoona pekee au viziwi pekee.
Changamoto zinazowakumba watu wenye ulemavu wa uziwi na kutoona
Umoja wa Mataifa kupitia wavuti mahsusi wa siku hii, unasema watu wenye ulemavu wa uziwi na kutoona hukumbwa na vikwazo kwa sababu hali yao haitambuliwi au haitolewi kipaumbele kama ulemavu wa kipekee.
Hali hii husababisha kutotambuliwa katika takwimu, sera na programu mbalimbali, jambo linalozuia upatikanaji wa huduma muhimu kwao.
Umuhimu wa wataalamu wa tafsiri na ukalimani
Watafsiri, wakalimani na waongozaji wa kitaalamu kwa watu wenye ulemavu wa uziwi na kutoona ni muhimu sana katika kuhakikisha upatikanaji wa taarifa, mawasiliano, huduma na haki za msingi.
Pia huwasaidia watu hao kuishi kwa kujitegemea na kushiriki kikamilifu katika jamii.
Kwa nini basi UN imechagua Juni 27 na si tarehe nyingine?
Tarehe 16 mwezi Juni mwaka 2025, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio namba A/79/L.92 la mwaka huu wa 2025, linalotangaza tarehe 27 Juni kila mwaka kuwa siku ya kimataifa ya watu wenye ulemavu wa Uziwi na Kutoona.
Tarehe hii Juni 27 ni kumbukizi ya kuzaliwa kwa mwandishi mashuhuri Hellen Keller mwaka 1880, ambaye ni miongoni mwa watu maarufu zaidi duniani wa jamii ya watu wenye ulemavu wa uziwi na kutoona.
Keller kabla ya kufariki dunia mwaka 1968, alitembelea makao makuu ya Umoja wa Mataifa mwaka 1949. Wakati wa ziara hiyo aliambatana na Msaidizi wake Molly Thompson ambaye alimsaidia kutafsiri mkutano ambao alihudhuria.
Azimio lenyewe A/79/L.92
Azimio hilo lililopitishwa bila kupigia kura liliwasilishwa na Antigua na Barbuda, Brazil, Cabo Verde, Croatia, Djibouti, Georgia, Jordan, Namibia, Qatar, Rwanda, na Tanzania.
Pamoja na mambo mengine azimio hilo lenye kurasa 2 na vipengele 6, linaeleza misingi ya kuwasilishwa kwake ni pamoja na kuzingatia kuwa watu wenye ulemavu wa uziwi na kutoona hukumbwa na vikwazo kutokana na hali hiyo kutotambuliwa na/au kutochukuliwa kama ulemavu wa kipekee.
Halikadhalika ukosefu wa huduma zao ili waweze kutangamana vema katika jamii na kwamba fimbo yenye rangi nyeupe na nyekundu ndio alama ya msingi inayotumiwa na watu wenye ulemavu wa uziwi na kutoona.
Hivyo azimio pamoja na mambo mengine linataka serikali kuzingatia kutambua ulemavu wa uziwi na kutoona kuwa ni ulemavu wa kipekee, na kwa mantiki hiyo sera na programu mahsusi ziandaliwe na zitambuliwe kwenye mifumo ya kisheria na kiutawala.