UN yaadhimisha miaka 80 ya Chata yake kwa wito mpya wa mshikamano duniani

UN yaadhimisha miaka 80 ya Chata yake kwa wito mpya wa mshikamano duniani
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limekutana leo mjini New York kuadhimisha miaka 80 tangu kutiwa saini kwa Mkataba wa Umoja wa Mataifa, huku viongozi wakitafakari umuhimu wa kudumu wa chombo hicho na haja ya kukifanyia mageuzi kwa dharura.
Katika hafla hiyo ya kumbukumbu ya miaka 80 tangu kutiwa saini kwa Mkataba wa Umoja wa Mataifa mwaka 1945, Katibu Mkuu António Guterres leo ametoa hotuba yenye msisitizo mkubwa, akiwahimiza viongozi wa dunia kujitolea upya kwa misingi ya sheria za kimataifa, amani, na haki.
Akihutubia Baraza Kuu la Umoja wa Umoja wa Mataifa, Guterres ameeleza kuwa Mkataba huo ni “tamko la matumaini na msingi wa ushirikiano wa kimataifa kwa ajili ya dunia bora. Kutoka kwenye majivu ya vita, dunia ilipanda mbegu ya matumaini,” amesema.
Ameongeza kuwa “Mkataba mmoja, maono ya aina moja, ahadi moja, kwamba amani inawezekana pale binadamu wanaposimama pamoja.” Alisisitiza kuwa Umoja wa Mataifa umekuwa jukwaa la kukutanisha mahasimu, kutoa sauti kwa wasiosikika, na kuwa injini ya maendeleo ya haki za binadamu na msaada wa kibinadamu.

Si menyu ya kuchagua vipengele
Guterres ametoa onyo kali dhidi ya tabia ya baadhi ya mataifa kuchagua vipengele vya chata wanavyovipenda na kupuuza vingine, akielezea hali hiyo kama “mashambulizi yasiyokuwa ya kawaida dhidi ya madhumuni na misingi ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa.”
Alitaja matumizi ya nguvu dhidi ya mataifa huru, ukiukwaji wa haki za binadamu, na matumizi ya chakula na maji kama silaha miongoni mwa mwenendo unaotia wasiwasi. “Mkataba wa Umoja wa Mataifa si wa hiari,” amesema akiongeza kuwa na “Si menyu ya kuchagua unachotaka. Ni msingi wa mahusiano ya kimataifa.”
Katibu Mkuu pia amezungumzia hali ya upinzani katika utawala wa kimataifa wa kisasa, mafanikio na kurudi nyuma kwa wakati mmoja. Ametoa mifano ya maendeleo ya demokrasia, misaada ya kibinadamu, na teknolojia, huku akikiri kuwepo kwa ongezeko la ukosefu wa usawa, mabadiliko ya tabianchi, na mizozo.
“Tumesherehekea mwisho wa vita huku tukishuhudia mwanzo wa vita vingine,” amesema.
Kwenda na dunia inayobadilika
Akimulika mbele, Guterres amesisitiza hitaji la mageuzi ndani ya Umoja wa Mataifa, akiwasihi wanachama waunge mkono “mkakati mpya mtambuka wa ushirikiano wa kimataifa unaoendana na karne ya 21”. Ametaja kupitishwa kwa Mkataba za Zama Zijazo mwaka 2024 kama hatua ya matumaini, lakini akasisitiza kuwa utekelezaji wa makubaliano hayo ni muhimu.
“Sasa zaidi ya wakati mwingine wowote, ni lazima tuheshimu na kujitolea tena kwa sheria za kimataifa kwa maneno na vitendo,” amesema. “Ili kuendana na dunia ya kidijitali na yenye nguvu nyingi za kiutawala.”
Ametoa wito wa ushirikishwaji mpana zaidi, hasa kwa vijana, jamii za kiraia, na sekta binafsi, ili kukabiliana na mishtuko ya kimataifa na kuendeleza malengo ya pamoja. “Lazima tufungue milango yetu zaidi,” amesema Guterres. “Na tujenge Umoja wa Mataifa ulioboreshwa, unaoakisi dunia tunayoishi leo.”
Kwa ajili ya sisi binadamu
Akihitimisha hotuba yake, Katibu Mkuu amerejea kwenye maono ya waanzilishi wa Umoja wa Mataifa. “Katika kumbukumbu hii, nawasihi wanachama wote waishi kwa mujibu wa dhamira na maandishi ya Chata,” amesema. “Kwa majukumu ambayo unatutaka tuyatimize. Na kwa ajili ya mustakabali unaotuita kuujenga. Kwa ajili ya amani. Kwa ajili ya haki. Kwa maendeleo. Kwa ajili ya sisi binadamu.”
Maadhimisho haya sio tu ya kutafakari miaka iliyopita, bali pia ni wito wa kuchukua hatua mpya, hasa wakati huu ambapo umuhimu na uimara wa ushirikiano wa kimataifa vinaendelea kupimwa.
Guterres amehitimisha kwa kusema “Kudumisha Chata ni jukumu lisiloisha na ni wajibu mtakatifu.”

Hiki ni kipindi cha machungu makubwa katia UN
Katika hotuba yake ya ufunguzi, Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Philémon Yang ameeleza hali ya sasa ya dunia kwa ukali, akisema, “tunaadhimisha siku hii katika kipindi cha maumivu makubwa katika maisha ya Umoja huu.”
Ametaja migogoro inayoendelea huko Gaza, Ukraine, na Sudan, akionya kwamba “vita na mapigano ya vurugu vinaonekana kuwa vya kawaida kuliko mazungumzo na diplomasia kwa ajili ya amani.”
Kwa kuzingatia hali ngumu ya ushirikiano wa kimataifa na misingi ya kimataifa kusambaratika, Rais huyo ametoa wito wa kuchukua hatua kwa ujasiri. “Baadhi ya mataifa muhimu yamechagua kutumia nguvu badala ya kuzingatia sheria za kimataifa na misingi ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa. Hali hiyo ni ya hatari sana,” amesema akiwahimiza wajumbe kupita tofauti za kisiasa, amewakumbusha maono ya kizazi kilichoasisi Umoja wa Mataifa akisema “Kwa pamoja waliweka msingi wa mpangilio mpya wa dunia unaopaswa kujengwa juu ya mazungumzo na ushirikiano.”
Lengo ni kuepusha vizazi vijavyo dhidi ya vita
Bwana Yang amekumbusha pia ahadi ya ujasiri ya Chata ya Umoja wa Mataifa kwamba ni “kuokoa vizazi vijavyo dhidi ya janga la vita.”
Akiendelea kwa lugha ya Kifaransa, Rais huyo amesisitiza haja ya mageuzi ili kuufanya Umoja wa Mataifa kuendana na hali halisi ya dunia ya leo, akitaja nyaraka muhimu kama Mkataba wa Zama Zijazo na mpango wa Katibu Mkuu wa UN80 Initiative kama njia za kuelekea mabadiliko.
“Uhalali wa Umoja wa Mataifa unategemea uwezo wake wa kuendana na wakati wetu,” amesema. Akihitimisha kwa wito wa dhati na kuhimiza mataifa yote “kufufua dhamira ya San Francisco na kuchagua mazungumzo badala ya migawanyiko, ushirikiano badala ya migogoro.”
Akirudia maneno ya mwanzo ya Mkataba huo, amewakumbusha wajumbe kwamba “Sisi, watu wa Umoja wa Mataifa, tukiwa na azma ya kuvilinda vizazi vijavyo dhidi ya janga la vita.”