Janga kubwa la kibinadamu linaendelea Gaza kufuatia ukosefu wa maji, njaa, na watu kutawanywa

Janga kubwa la kibinadamu linaendelea Gaza kufuatia ukosefu wa maji, njaa, na watu kutawanywa
Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Misaada ya Kibinadamu na Masuala ya Dharura OCHA leo imeripoti kuwa vituo vya maji safi vinavyotumika Gaza ni asilimia 40 tu, huku uhaba wa mafuta ukipelekea mifumo ya maji kukaribia kusambaratika kabisa.
Hadi katikati ya Juni, asilimia 93 ya kaya zilikuwa na uhaba wa maji, hali inayoongeza hatari ya kiu na magonjwa ya umma. Ofisi hiyo imesema familia nyingi Gaza zinakumbwa na njaa kubwa, wakijitahidi kuingia kwenye maeneo ya chakula huku vifo vikirekodiwa karibu kila siku.
Kaya nyingi zinaishi kwa mlo mmoja dhaifu wa lishe kwa siku, na watu wazima mara nyingi hukosa kula ili kuwalinda watoto, wazee, na wagonjwa.

Elimu imesimama na afya iko njiapanda
Wanafunzi zaidi ya 76,000 Gaza hawakuweza kuhudhuria mtihani wao wa kidato cha nne kwa miaka miwili ya masomo iliyopita, jambo linaloathiri mustakabali wa kizazi kizima limeonya Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF.
Matukio ya ukatili dhidi ya wanawake na wasichana yanaongezeka, wakiwa hatarini zaidi kutokana na unyanyasaji, ukatili na mikakati hatari ya kuishi katika hali hii ya maafa.
UNICEF imeripoti kuwa watoto 112 wanapatiwa matibabu ya utapiamlo mkali kila siku, na hali hii itazidi kuwa mbaya ikiwa haitatatuliwa haraka.
UNRWA yaonya kuhusu mipango ya kuifuta Palestina
Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la msaada kwa wakimbizi wa Kipalestina UNRWA Philippe Lazzarini amesema kuna mradi unaotekelezwa wa kuwagawa Wapalestina na ardhi yao, huku wakilazimishwa kuishi katika maeneo yanayofanana nageto au mitaa ya mabanda. Timu za UNRWA zinaendelea kutoa msaada licha ya mashambulizi na hali ngumu katika eneo hilo.
Mamlaka za Israel zimeongeza juhudi za kuwafurusha Wapalestina kutoka maeneo yao Ukingo wa Magharibi, ikiwemo Jerusalem Mashariki. Tarehe18 Juni, mabaraza ya mipango ya Israeli yalipiga marufuku vibali vyote vya ujenzi vya Wapalestina katika eneo la Masafer Yatta, likitumiwa kama eneo la mazoezi ya kijeshi.
Hali hii ni sehemu ya juhudi za kuanzisha makazi na kuchukua ardhi kinyume na sheria za kimataifa imesema UNRWA. Mashirika ya misaada ya kibinadamu yamehimiza jamii ya kimataifa kuchukua hatua za haraka kuzuia kuanguka kwa mifumo ya msaada Gaza na kuzuia kufukuzwa kwa watu katika Ukingo wa Magharibi.