Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UDADAVUZI: Mpango wa UN80 ni nini na kwa nini ni muhimu kwa dunia

Maafisa wa Umoja wa Mataifa wakiwa wameshikilia nakala za Katiba ya Umoja wa Mataifa kwenye makao makuu ya UN New York
UN Photo/Amanda Voisard
Maafisa wa Umoja wa Mataifa wakiwa wameshikilia nakala za Katiba ya Umoja wa Mataifa kwenye makao makuu ya UN New York

UDADAVUZI: Mpango wa UN80 ni nini na kwa nini ni muhimu kwa dunia

Masuala ya UM

Katika dunia inayokumbwa na migogoro inayoongezeka, tofauti zinazozidi kuongezeka, na kupungua kwa imani katika taasisi za kimataifa, Umoja wa Mataifa umezindua juhudi kabambe za kuimarisha namna unavyowahudumia watu kila mahali.

Mpango wa UN80, ambao ulizinduliwa mwezi Machi na Katibu Mkuu António Guterres, ni juhudi za mfumo mzima za kurahisisha uendeshaji, kuongeza ufanisi, na kuthibitisha tena umuhimu wa Umoja wa Mataifa katika dunia inayobadilika kwa kasi.

“Huu ni wakati mzuri wa kujitathimini na kuona endapo tunafaa kwa madhumuni yetu katika mazingira ambayo, tuseme ukweli, ni changamoto kwa mfumo wa kimataifa na kwa Umoja wa Mataifa,” amesema Guy Ryder, Naibu Katibu Mkuu wa Sera na mwenyekiti wa Kikosi Kazi cha UN80.

Ujulikanao kama Mpango wa UN80, mchakato huu unalenga sio tu kuboresha ufanisi, bali pia kusisitiza tena thamani ya mfumo wa kimataifa wa ushirikiano wakati ambapo imani imepungua na mahitaji ni makubwa.

Unalenga kuimarisha uwezo wa Umoja wa Mataifa kukabiliana na changamoto za sasa duniani kuanzia migogoro, ukimbizi na kutokuwepo kwa usawa hadi mabadiliko ya tabianchi na maendeleo ya haraka ya kiteknolojia huku pia ukikabiliana na shinikizo la nje kama vile kupunguzwa kwa bajeti na mgawanyiko wa kisiasa unaokua katika uwanja wa kimataifa.

“Tutatoka katika mchakato huu tukiwa na Umoja wa Mataifa ulio thabiti, unaofaa kwa matumizi, na tayari kwa changamoto za baadaye ambazo bila shaka zitakuja,” ameeleza Bw. Ryder.

Muonekano wa majengo ya Umoja wa Mataifa kutokea kisiwa cha Roosevelt New York
UN News/Anton Uspensky
Muonekano wa majengo ya Umoja wa Mataifa kutokea kisiwa cha Roosevelt New York

Nguzo tatu za mageuzi

Katika kiini cha UN80 kuna mikondo mitatu mikuu ya kazi:

  1. Kuimarisha ufanisi wa ndani
  2. Tathmini ya utekelezaji wa maagizo
  3. Mabadiliko ya kimfumo na mpangilio wa program

Mkondo wa kwanza unalenga kuboresha ufanisi na matokeo ya ndani, kupunguza urasimu, na kuboresha matumizi ya rasilimali kwa kuhamishia baadhi ya shughuli katika maeneo yenye gharama nafuu zaidi.

Bwana Ryder anabainisha kuwa taratibu za kiutawala zinazochukua muda na kurudiarudia zinashughulikiwa.
“Tunahitaji kuona ni nini tunaweza kufanya vizuri zaidi. Tunataka kuchunguza maeneo ambayo tunaweza kuboresha ufanisi na kuondoa taratibu zisizo za lazima za kiurasi,” ameeleza.

Mkondo wa pili ni tathmini ya utekelezaji wa maagizo, ambayo yanahusisha kuchambua karibu nyaraka 4,000 za maagizo zinazotoa mwongozo kwa kazi ya Sekretarieti ya Umoja wa Mataifa.

Maagizo haya hutolewa na nchi wanachama kupitia maazimio ya vyombo vya Umoja wa Mataifa kama Baraza Kuu au Baraza la Usalama.

Maagizo haya huongoza kazi za Umoja wa Mataifa kuanzia operesheni za kulinda amani na misaada ya kibinadamu hadi haki za binadamu na mazingira.

Kwa miongo mingi, takriban maagizo 40,000 yamekusanywa, mengine yakiwa yanarudiarudia au yamepitwa na wakati, ndiyo maana tathmini ni sehemu muhimu ya mpango wa UN80.
“Hebu tuyatazame,” amesema Bwana. Ryder. “Tuone kama kuna kurudiarudia, wapi tunaweza kutoa kipaumbele na wapi si lazima, na kutambua yaliyo ya ziada.”

Lakini kuchambua mlundikano huu wa maagizo si jambo jipya. “Tulijaribu kufanya hivi mwaka 2006. Haikufanikiwa sana,” amekumbusha Bwana Ryder.
Hata hivyo, safari hii kuna jambo moja jipya linalowezesha mchakato huu. “Sasa tunazo takwimu na uwezo wa uchambuzi. Tunatumia mbinu za akili mnemba kutoa taarifa bora zaidi na zilizopangwa vizuri kwa nchi wanachama hoja iliyo na nguvu zaidi ambayo inaweza kuendesha mchakato wenye mafanikio.”
Amesisitiza kuwa jukumu la kuamua ni maagizo yapi yabaki, yarekebishwe au yaondolewe liko mikononi mwa nchi wanachama.
“Maagizo haya ni ya nchi wanachama. Wao ndio waliyaanzisha, na ni wao pekee wanaoweza kuyatathmini. Sisi tunaweza kuangalia ushahidi, tukauwasilisha kwa nchi wanachama, lakini hatimaye wao ndiyo waamuzi wa maagizo – na kwa kiasi kikubwa, wa maamuzi yote yanayohusiana na UN80.”

Mkondo wa tatu unachunguza kama kuna haja ya mabadiliko ya kimfumo na upangaji upya wa programu katika mfumo mzima wa Umoja wa Mataifa. “Hatimaye, tunaweza kuhitaji kuangalia muundo wa mfumo wa Umoja wa Mataifa, ambao kwa sasa umejaa vipengele vingi na ni changamano,” amesema Bwana Ryder.

Mapendekezo pia yanatarajiwa kujitokeza kupitia tathmini ya utekelezaji wa maagizo.

Guy Ryder msaidizi wa Katibu Mkuu kwa ajili ya sera na mkuu wa mpango wa UN80
UN Photo/Manuel Elías
Guy Ryder msaidizi wa Katibu Mkuu kwa ajili ya sera na mkuu wa mpango wa UN80

Kikosi Kazi na mtazamo wa mfumo mzima

Ili kushughulikia mageuzi katika mfumo tata kama huu, Katibu Mkuu ameunda makundi saba ya mada chini ya Kikosi Kazi cha UN80, kila moja likiratibiwa na viongozi waandamizi wa Umoja wa Mataifa kutoka maeneo mbalimbali ya mfumo.

Makundi haya yanahusu amani na usalama, misaada ya kibinadamu, maendeleo Sekretarieti na mfumo wa Umoja wa Mataifa, haki za binadamu, mafunzo na utafiti, pamoja na mashirika maalum.

Ryder mwenyekiti wa Kikosi Kazi cha UN80 amesema “Ni muhimu kusema kwamba katika wakati ambapo mfumo uko chini ya shinikizo, mfumo unachukua hatua kama mfumoHii si kazi ya New York pekee, wala Sekretarieti pekee. Ni ya mfumo mzima.”

Kila kundi linatarajiwa kutoa mapendekezo ya kuboresha uratibu, kupunguza mgawanyiko, na kurekebisha majukumu pale inapohitajika.

Baadhi ya makundi tayari yamewasilisha mawazo ya awali. Seti pana ya mapendekezo inatarajiwa mwezi Julai.

Masuala ua ulinzi wa amani ni moja ya kiini cha mpango wa UN80
UNFICYP/Katarina Zahorska
Masuala ua ulinzi wa amani ni moja ya kiini cha mpango wa UN80

Mageuzi, siyo kupunguza wafanyakazi

Mjadala kuhusu mpango wa UN80 umejikita zaidi kwenye mapendekezo ya kupunguza bajeti na wafanyakazi, hali ambayo imeibua wasiwasi kuwa huu ni mpango wa kupunguza gharama pekee.

Hata hivyo, Bwana. Ryder anasisitiza kwamba mtazamo huo unakosa picha kamili.

“Ni kweli, tunakabiliwa na changamoto za kifedha. Hatuna haja ya kulifumbia macho hilo. Lakini huu si mpango wa kupunguza gharama au kupunguza ukubwa wa mfumo. Tunataka kuufanya Umoja wa Mataifa kuwa imara zaidi,” amesema.

Hata hivyo, shinikizo la kifedha katika mfumo mzima haliwezi kupuuzwa. Bajeti ya programu iliyorekebishwa kwa mwaka 2026, inayotarajiwa mwezi Septemba, inatarajiwa kujumuisha upunguzaji mkubwa wa ufadhili na nafasi za ajira kwa taasisi za Sekretarieti matokeo ya changamoto za mtiririko wa fedha kutokana na ucheleweshaji na ukamilishaji wa michango kutoka kwa nchi wanachama.

“Mpango wa UN80 unalenga kuboresha athari na ufanisi wa mfumo wa kimataifa wa ushirikiano na wa Umoja wa Mataifa,” Bwana Ryder anaeleza. “Sasa, hilo halimaanishi japokuwa tungetamani iwe tofauti kwamba hatupaswi kuangalia bajeti na rasilimali zetu katika sehemu mbalimbali za mfumo.”

“Taasis nyingi zimejikuta zikilazimika kufanya maamuzi magumu, na hilo linatokea kila siku. Hiyo ndiyo hali halisi tunayokabiliana nayo,” ameongeza.

Bw. Ryder anasisitiza kwamba uendelevu wa kifedha na utekelezaji wa majukumu ya Umoja wa Mataifa si mambo yanayopingana bali ni malengo yanayopaswa kutekelezwa kwa pamoja. “Lazima tulinganishe malengo haya mawili kujihakikishia uendelevu wa kifedha katika mazingira haya magumu, lakini pia kuzingatia daima athari tunayoleta katika kutekeleza wajibu wetu chini ya Katiba ya Umoja wa Mataifa,” amesema.

Watoto wa shule nchini Haiti wakipata  mlo kupitia programu ya mlo shuleni inayotolewa na shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula duniani, WFP nchini humo.
© WFP/Jonathan Dumont
Watoto wa shule nchini Haiti wakipata mlo kupitia programu ya mlo shuleni inayotolewa na shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula duniani, WFP nchini humo.

Kwa nini UN80 ni muhimu kwa watu wote duniani

UN80 si mageuzi ya kiutawala tu ni kuhusu watu. Ni kuhusu wale wanaotegemea msaada wa Umoja wa Mataifa wakati wa migogoro, majanga au changamoto za maendeleo.

“Iwapo Umoja wa Mataifa utaweza kujibadilisha, kujiboresha, wakati mwingine kupitia maamuzi magumu, maana yake ni kwamba msaada unaookoa maisha utafika kwa ufanisi zaidi kwa watu tunaowahudumia,” anasema Bwana. Ryder.

Umoja wa Mataifa unabaki kuwa jukwaa muhimu lisilo na mfano wake kwa ajili ya kuendeleza amani, maendeleo endelevu na haki za binadamu kwa wote.

“Huu ni Umoja wa Mataifa ukichukua kwa uzito wajibu wake kwa watu tunaowahudumia,” amesema Bw. Ryder.

Kwa sasa, Umoja wa Mataifa unawasaidia zaidi ya watu milioni 130 waliolazimika kuhama makazi yao, unatoa chakula kwa zaidi ya milioni 120, unasambaza chanjo kwa karibu nusu ya watoto duniani, na unaunga mkono shughuli za kulinda amani, haki za binadamu, uchaguzi, na hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi kote ulimwenguni. Kazi ya Umoja wa Mataifa ya maendeleo imechangia kujenga jamii zenye amani na uthabiti.

UNICEF inasaidia masuala ya chanjo katika kijiji cha Shan Myanmar
© UNICEF/UNI561135/Minzayar Oo.
UNICEF inasaidia masuala ya chanjo katika kijiji cha Shan Myanmar

Kinachofuata

Kikosi Kazi cha UN80 kitawasilisha mapendekezo yake kwa Katibu Mkuu, ambaye tayari ameainisha maeneo ya mwanzo yanayotarajiwa kuleta matokeo. Kikosi kazi kinachoshughulikia ufanisi ndani ya Sekretarieti ya Umoja wa Mataifa, kinachoongozwa na Naibu Katibu Mkuu Catherine Pollard, kinatarajiwa kuwasilisha mapendekezo ya awali mwishoni mwa Juni.

Ripoti kuhusu tathmini ya utekelezaji wa maagizo itawasilishwa mwishoni mwa Julai.

Kazi hii chini ya mikondo miwili ya awali ya UN80 itasaidia kutoa mwongozo kuhusu mabadiliko ya kimuundo na upangaji upya wa programu katika mfumo mzima wa Umoja wa Mataifa.

Mapendekezo ya mkondo wa tatu yatawasilishwa kwa nchi wanachama katika miezi ijayo na hata mwaka ujao.

Ingawa kazi bado iko katika hatua za mwanzo, Bwana Ryder anaamini kwamba Umoja wa Mataifa una zana sahihi pamoja na dira ya wazi ya matarajio na uharaka wa utekelezaji.

“Tunaendelea vizuri. Kuna kazi nyingi ya maandalizi zinazoendelea sasa,” amesema. “Kadri wiki zinavyosonga, suala hili litasogea zaidi kwenye uwanja wa nchi wanachama, na hapo ndipo tutaanza kuona matokeo.”

Hatimaye, nchi wanachama zitahitaji kuamua cha kufanya kuhusu matokeo hayo. “Itabidi waamue nini wanataka kufanya. Je, watapenda kuanzisha mchakato wa serikali na serikali? Katibu Mkuu tayari ametaja hilo kama uwezekano.”

Kufafanua mafanikio

Hivyo basi, mafanikio yanamaanisha nini?

“Ni mfumo wa Umoja wa Mataifa ambao unaweza kutoa huduma kwa ufanisi zaidi, kuimarisha na kuendeleza imani katika hatua za pamoja za kimataifa,” amesema Bwana Ryder.

“Mfumo ambao unaweza kuwathibitishia wananchi na watoa maamuzi wa kisiasa kuwa taasisi hii inastahili kuwekeza ndani yake. Kwamba hili linapaswa kuwa chaguo lako la kwanza unapokabiliana na changamoto za siku zijazo.”

Kwa mwenyekiti wa Kikosi Kazi cha UN80, mafanikio yanajikita kwenye uaminifu, uwezo, na imani ya umma na kuhakikisha kuwa Umoja wa Mataifa unabaki kuwa si tu muhimu, bali wa lazima.

“Sote tunapaswa kujali kuhusu hili,” anasema. “Ikiwa tunaamini kuwa mfumo wa kimataifa wa ushirikiano ni chombo bora tulicho nacho kwa ajili ya kukabiliana na changamoto za dunia, basi tunapaswa kuhakikisha tunakitengeneza upya, tunakiboresha, na kukifanya kifae kwa kazi yake kwa kiwango cha juu zaidi kinachowezekana.”