Afrika yasalia gizani licha ya mbinu rahisi zinazoweza kufikisha umeme majumbani - Ripoti
Afrika yasalia gizani licha ya mbinu rahisi zinazoweza kufikisha umeme majumbani - Ripoti
- Kila mwaka watu milioni 14 hujumuika na wengine wasio na umeme Afrika
- Teknolojia ya biogesi na sola bado hazipatiwi kipaumbele Afrika
- Nchi 18 kati ya 20 zenye upungufu mkubwa wa umeme zinapatikana eneo la Afrika kusini mwa Jangwa la Sahara.
- Ufadhili kwa Afrika bado ni kitendawili
Licha ya asilimia 92 ya wakazi wa dunia kufikiwa na huduma ya umeme, bado bara la Afrika linaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya watu wasio na huduma hiyo muhimu.
Taarifa hizo ni kwa mujibu wa ripoti mpya ya kimataifa kuhusu nishati iliyotolewa leo Marekani, Ufaransa, Uswisi na Falme za kiarabu, ambapo inaonesha hali ya kusikitisha kuhusu mustakabali wa nishati barani Afrika.
Bara la Afrika limeachwa nyuma zaidi katika upatikanaji wa umeme na nishati safi ya kupikia, imesema ripoti hiyo ikipatiwa jina; Ripoti ya Ufuatiliaji wa SDG 7: Tathmini ya Maendeleo ya Nishati 2025.
Kila mwaka watu milioni 14 hujumuika na wengine wasio na umeme Afrika
Wakati asilimia 92 ya watu duniani sasa wanapata huduma za msingi za umeme, ripoti inaonesha kuwa asilimia 85 ya wale ambao bado wako gizani wanatoka nchi za Afrika zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Cha kusikitisha zaidi ni kuwa idadi ya watu wasiopata nishati safi ya kupikia katika eneo hilo inaendelea kuongezeka—ikiongezeka kwa watu milioni 14 kila mwaka—na kuchangia kwenye jumla ya watu bilioni 2.1 wanaotegemea kuni na mkaa, ambazo ni nishati chafu na hatarishi.
Ugatuzi wa huduma za nishati: Fursa iliyopotezwa
Ripoti inasisitiza kuwa mifumo ya ugatuzi wa nishati jadidifu—kama vile mifumo ya sola isiyohitaji gridi na gridi za kati—ndiyo njia bora zaidi, kwa gharama nafuu, ya kuziba pengo la upatikanaji wa nishati katika maeneo ya vijijini na yaliyo hatarini.
Teknolojia hizi zinaweza kusambazwa kwa haraka na kuendana na mahitaji ya jamii zilizopo maeneo ya mbali ambako kupeleka gridi ya taifa si rahisi wala si endelevu kifedha.
Mbinu hiyo hiyo ya ugatuzi inapendekezwa pia kwa ajili ya kutatua changamoto za upatikanaji wa nishati safi ya kupikia. Teknolojia kama mitambo ya biogesi ya nyumbani na majiko ya umeme inayotumia gridi za kati, inaweza kupunguza kwa kiasi kikubwa athari za kiafya zinazotokana na uchafuzi wa hewa wa ndani ya nyumba—tatizo linalosababisha mamilioni ya vifo vya mapema kila mwaka, hasa kwa wanawake na watoto.
Hata hivyo, kasi ya kusambaza majawabu hayo bado ni ndogo mno, hasa barani Afrika, kutokana na vikwazo vya kifedha na miundombinu duni.
Hali katika nchi za Afrika zilizo kusini mwa Jangwa la Sahara
Licha ya ukuaji wa nishati jadidifu duniani, Afrika bado inasuasua. Mwaka 2023, kanda hii ilikuwa na wastani wa wati 40 za uwezo wa nishati jadidifu kwa kila mtu, ikilinganishwa na zaidi ya wati 1,100 katika nchi zilizoendelea. Tofauti hii ni kubwa hata kati ya nchi zinazoendelea—Afrika ikiwa na asilimia moja tu ya wastani wao.
Nchi 18 kati ya 20 zenye upungufu mkubwa wa upatikanaji wa umeme zinapatikana eneo la Afrika kusini mwa Jangwa la Sahara. Familia nne kati ya tano katika eneo hili bado zinategemea nishati hatarishi ya kupikia, hali inayochochea uharibifu wa mazingira na migogoro ya kiafya.
“Licha ya maendeleo katika baadhi ya maeneo ya dunia, upanuzi wa upatikanaji wa umeme na nishati safi ya kupikia unasonga polepole mno, hasa Afrika,” amesema Fatih Birol, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Kimataifa la Nishati (IEA). “Uwekezaji mkubwa unahitajika kwa haraka, ukiwemo msaada wa kupunguza gharama za mitaji kwa miradi.”
Pengo la ufadhili lazidi kuzuia maendeleo
Kiini cha tatizo hili ni ukosefu wa ufadhili wa kutosha na unaopatikana kwa gharama nafuu. Ingawa misaada ya kifedha ya kimataifa kwa nishati safi katika nchi zinazoendelea iliongezeka hadi dola bilioni 21.6 mwaka 2023, bado ni chini ya kiwango cha juu cha mwaka 2016 cha dola bilioni 28.4. Aidha, sehemu kubwa ya fedha hizi zimejikita kwenye nchi chache tu—ni nchi mbili pekee kutoka zile za Afrika zilizo kusini mwa Jangwa la Sahara zilizojumuishwa kati ya wapokeaji watano wa juu.
Mikopo ndiyo chanzo kikuu cha fedha hizo, ikiunda asilimia 83 ya msaada huo, wakati ruzuku—ambayo ni muhimu kwa maeneo yenye hatari kubwa na kipato cha chini—ilikuwa chini ya asilimia 10.
“Ingawa mikondo ya kifedha ya kimataifa inaongezeka, maendeleo bado hayajalingana kimataifa,” amesema Francesco La Camera, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Nishati Jadidifu (IRENA). “Afrika bado inakabiliwa na upungufu wa upatikanaji wa mitaji nafuu. Ili kufunga pengo hili, tunapaswa kuongeza fedha za masharti nafuu, ruzuku, na nyenzo za kupunguza hatari kwa muktadha wa ndani.”
Mapendekezo
Ripoti inatoa wito wa hatua za haraka na za pamoja kimataifa zenye kulenga hasa nchi za Afrika zilizo kusini mwa Jangwa la Sahara na maeneo mengine yaliyopuuzwa. Mapendekezo muhimu ni:
- Kufanya mageuzi ya mifumo ya fedha ya kimataifa na baina ya nchi ili kuongeza upatikanaji wa mitaji ya umma kwa gharama nafuu;
- Kuongeza fedha za masharti nafuu na ruzuku ili kupunguza hatari kwa wawekezaji na kusaidia miradi yenye matokeo makubwa;
- Kukuza majawabu ya ugatuzi wa nishati jadidifu, hasa katika maeneo ya vijijini na yaliyo mbali;
- Kusaidia upatikanaji wa nishati safi ya kupikia kwa kutumia teknolojia kama biogesi na majiko ya umeme;
- Kuboresha mipango ya kitaifa ya nishati na kanuni ili kuvutia uwekezaji wa sekta binafsi na kuwezesha utekelezaji wa miradi.
Hatua hizi zinalenga si tu kuongeza upatikanaji wa umeme, bali pia kushughulikia matatizo ya kiafya na kukuza maendeleo ya kiuchumi.
Mkutano wa Julai 16 2025 New York
Ripoti hii itawasilishwa kwa viongozi wa dunia kwenye Jukwaa la Kisiasa la Ngazi ya Juu kuhusu Maendeleo Endelevu litakalofanyika mjini New York tarehe 16 Julai.
Ujumbe ni wazi: Bila mabadiliko makubwa katika ufadhili na usambazaji wa nishati safi—hasa Afrika—dunia iko hatarini kuwaacha nyuma mamilioni.
Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani (WHO), amesisitiza dharura ya suala hili: “Tunahitaji kwa haraka kuchukua hatua na kuwekeza katika suluhisho za nishati safi ya kupikia ili kulinda afya ya watu na sayari—sasa na siku zijazo.”
Kuhusu ripoti hii
Ripoti ya Ufuatiliaji wa SDG 7: Tathmini ya Maendeleo ya Nishati 2025 ni chapisho la pamoja kati ya Shirika la Kimataifa la Nishati (IEA), Shirika la Kimataifa la Nishati Jadidifu (IRENA), Kitengo cha Takwimu cha Umoja wa Mataifa, Benki ya Dunia, na Shirika Umoja wa Mataifa la Afya Duniani (WHO).