Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

IOM yawezesha maendeleo yanayoongozwa na jamii nchini Somalia

Iftin na Aminaa wakiwa wamesimama mbele ya taa za barabarani zinazotumia nishati ya sola, ambazo sasa zinawezesha wasichana kutembea bila  hofu nyakati za usiku wakitoka masomoni.
© IOM/Spotlight Communications
Iftin na Aminaa wakiwa wamesimama mbele ya taa za barabarani zinazotumia nishati ya sola, ambazo sasa zinawezesha wasichana kutembea bila hofu nyakati za usiku wakitoka masomoni.

IOM yawezesha maendeleo yanayoongozwa na jamii nchini Somalia

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Jumuiya ya kimataifa ikijiandaa kukutana Hispania kujadili Ufadhili kwa Maendeleo duniani, tunakuletea simulizi ya ustahimilivu kutoka Somalia ambayo ni kumbusho tosha la manufaa ya mbinu bunifu za ufadhili. Katika Jimbo la Galmudug, katikati mwa Somalia, ndoto ya wasichana wawili, Iftin na Aminaa  ya kujiunga na Chuo Kikuu mjini Abudwaq ilikumbwa na changamoto nyingi.

Mathalani, umeme kukatika mara kwa mara na barabara ndefu na yenye giza kati ya chuo na mji, viliwafanya wao na wasichana wengine washindwe kuhudhuria masomo ya jioni. Lakini hawakukata tamaa.

Mfuko wa ushirikiano wa IOM (CFS)

Wakiwa na dhamira ya dhati kutafuta suluhisho, walikimbilia Mfuko wa Ushirikiano wa Ufadhili wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji (IOM) ambao hutoa ufadhili unaolingana na kiasi kilichochangishwa na jamii kwa miradi inayoongozwa na wananchi, kwa lengo la kuwawezesha watu wa Somalia kuongoza maendeleo yao wenyewe.

Kwa kushirikiana na wanafunzi wanawake wengine 19, Iftin na Aminaa waliwasilisha pendekezo rahisi lakini lenye matokeo makubwa, kuchangisha fedha kwa ajili ya taa za mtaa zitumiazo nishati ya jua, au sola na mfumo wa nishati ya jua kwa chuo.

Julai 2022, walikuwa wamekusanya dola 10,000. IOM ikalinganisha mchango huo na kuongeza dola 50,000 zaidi.

Paneli za sola ambazo zinapatia umeme wa  uhakika Chuo Kikuu cha Abuduwaq jimboni Galmudug nchini Somalia.
© IOM/Spotlight Communications
Paneli za sola ambazo zinapatia umeme wa uhakika Chuo Kikuu cha Abuduwaq jimboni Galmudug nchini Somalia.

Matokeo ya miradi ya CFS kote Somalia

Matokeo yake yalikuwa barabara iliyojaa mwanga na usalama kati ya mji wa Abudwaq na Chuo Kikuu, pamoja na mfumo wa nishati ya jua unaofanya kazi saa 24. Sasa chuo kinapata nishati safi muda wote, na haikuishia hapo.

Baadaye jamii iliamua kuunganisha kisima kilicho karibu na mfumo huo wa sola, na hivyo kutoa maji safi na bure kwa wakazi wote wa Abudwaq na jamii za wafugaji. Wafugaji huleta mifugo yao kunywa maji na kula majani karibu na kisima hicho.

Mohamed Mohamud Hussein, Afisa wa IOM anayehusika na mipango ya Jamii anasema, “Abudwaq haikuwa miongoni mwa maeneo tuliyopanga awali. Lakini tuliangalia pendekezo lao kwa sababu lilikuwa la kina, na lenye uwezo mkubwa wa kubadilisha jamii, likilingana na vipaumbele vya CFS kuhusu umiliki na uendelevu.”

Ujasiri wa Iftin na Aminaa uliwapa moyo jamii nyingine kote Somalia.

Historia ya CFS huko Somalia

CFS ilianzishwa kama mradi wa majaribio na IOM mwaka 2021 na imekuwa mojawapo ya nyenzo bunifu zaidi za ujenzi mpya nchini Somalia. Inawawezesha wananchi kuamua mustakabali wao.

Mwisho wa mwaka 2024, jumla ya miradi 42 ilikuwa imekamilika, ikiwafikia watu zaidi ya 580,000 katika wilaya 22 za Somalia ya kati. Miradi mingine 9 ilikuwa inaendelea.

Zaidi ya wanajamii 1,600, wakiwemo wanadiaspora, walichangia zaidi ya dola 500,000, huku IOM ikichangia dola milioni 2.3 zaidi.

Mifugo nayo inajipatia maji ya kunywa kutoka katika boza maji linalopatiwa nishati ya sola
© IOM/Abdirahman Deni
Mifugo nayo inajipatia maji ya kunywa kutoka katika boza maji linalopatiwa nishati ya sola

Umoja ni nguvu

Hata katika mazingira dhaifu, nguvu ya pamoja inaendelea kuleta mabadiliko. Katika Farjano, ujenzi wa makazi ya watu waliofurushwa katika Jimbo la Galmudug, ujenzi wa shule mpya ya msingi haukuishia tu kwenye madarasa, uliibua matumaini mapya.

Mara ya kwanza kabisa, watoto wangu wote waliweza kwenda shule bila gharama yoyote,” anasema Shamso, mama wa watoto watatu.

Huko Mataban, uwanja mpya wa michezo wa vijana ulileta mshikamano na utambulisho wa pamoja. “Uwanja huu umetufanya tuwe kitu kimoja kwa njia ambazo hatukuwahi kufikiria,” amesema Mustaf, mkazi wa Mataban. “Sio tu kwa michezo, ni mahali ambapo jamii yetu hujihisi kuwa kitu kimoja.”

Kutoka chini kwenda juu

Kwa kuitaka jamii ibaini mahitaji yake na kuchangia fedha za awali, mfumo wa CFS unatumia njia ya chini kwenda juu badala ya ile ya juu kwenda chini inayotumiwa mara nyingi. Mbinu hii huhakikisha kuwa miradi inaendeshwa na jamii yenyewe, na hivyo kuongeza nafasi ya mafanikio ya muda mrefu.

Somalia kama mfano wa mageuzi ya ufadhili wa maendeleo FFD4

Mkutano wa 4 wa Kimataifa wa Ufadhili kwa Maendeleo (FFD4), unaotarajiwa kuanza Sevilla, nchini Hispania tarehe 30 Juni 2025, unalenga kufanyia mageuzi mifumo ya ufadhili katika ngazi zote. Bila shaka, suluhisho za mashinani na juhudi zinazoongozwa na jamii, kama zile zilizoshuhudiwa Somalia, zitakuwa miongoni mwa mifano inayotazamwa kwa karibu.

Shule mpya ya msingi ilijengwa huko Farjano kutokana na mchango wa fedha wa jamii na IOM
© IOM/Abdirahman Deni
Shule mpya ya msingi ilijengwa huko Farjano kutokana na mchango wa fedha wa jamii na IOM