Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wanawake wa Somalia na usafirishaji baharini

Hafla ya mabaharia kwenye mjadala kuhusu wanawake katika sekta ya usafirishaji majini, uliofanyika kwenye mji mkuu Mogadishu, Somalia.
©UNTMIS
Hafla ya mabaharia kwenye mjadala kuhusu wanawake katika sekta ya usafirishaji majini, uliofanyika kwenye mji mkuu Mogadishu, Somalia.

Wanawake wa Somalia na usafirishaji baharini

Masuala ya UM

Nchini Somalia, suala la usawa wa kijinsia katika sekta ya baharini limepatiwa kipaumbele kwenye mjadala kuhusu wanawake katika tasnia hiyo, mjadala uliofanyika kwenye mji mkuu Mogadishu ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya kimataifa ya mabaharia inayoadhimishwa tarehe 25 mwezi Juni kila mwaka ikibeba maudhui Meli yangu isiyo na unyanyasaji. 

Fartun Abdukadir, Naibu Waziri wa bandari na usafiri wa baharini nchini Somalia akizungumza kwenye mjadala huo ulioleta pamoja wadau wa kitaifa na kimataifa wa sekta ya usafirishaji baharini kuhusu umuhimu wa kuondoa vizingiti kwa wanawake na kukuza usawa kijinsia katika sekta ya usafirishaji baharini anaelezea wanachofanya kukuza usawa wa kijinsia katika usafirishaji baharini.

“Somalia ina wanawake wanaofanya kazi bandarini, wanaofanya tafiti, kulinda mazingira, na kushughulika na sheria za usafirishaji baharini. Wizara imejizatiti kuondoa vikwazo vinavyowazuia wanawake kushiriki katika shughuli za usafirishaji baharini, na pia kupambana na ubaguzi.”

Kwa upande wake, Waziri wa uvuvi na uchumi wa bahari, Ahmed Hassan Aden, anasisitiza dhamira ya serikali katika kuwawezesha wanawake akisema, “Wanawake wameonekana kuwa uti wa mgongo wa maendeleo nchini Somalia. Tunajivunia kusema kuwa mwanamke wa Kisomali anaweza kupata maarifa, ujuzi, na fursa zote za kutimiza ndoto zake.”

Kwa upande wake Halima Abdi Mohamed, ambaye ni baharia akaelezea msingi wa yeye kujikita kwenye tasnia hiyo anasema “Nilihamasika kujiunga na sekta ya usafirishaji majini baada ya kuona manufaa mengi yanayowezekana kwa wanawake. Haikuepukika, nililazimika kujiunga.”

Nasrin Khan, Afisa kutoka Ujumbe wa Mpito wa Usaidizi nchini Somalia, UNTMIS akihutubia katika mjadala kuhusu wanawake katika sekta ya usafirishaji majini.
©UNTMIS

Nasrin Khan, Afisa kutoka Ujumbe wa Mpito wa Usaidizi nchini Somalia, UNTMIS akawa na ujumbe akisema kwa wanawake wote wasomali katika sekta ya bahari. Uongozi wenu, dira na ujasiri vinajenga mustakabal iwa Somalia na kuwa hamasa ya ukanda huu. Ninyi sio tu sehemu ya simulizi ya baharini, bali mnaongoza simulizi hiyo.