Wakimbizi milioni 2.5 watahitaji uhamisho mwaka 2026
Wakimbizi milioni 2.5 watahitaji uhamisho mwaka 2026
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR, linakadiria kuwa wakimbizi milioni 2.5 duniani kote watahitaji kuhamishiwa Kwenda katika nchi nyingine mwaka ujao, kwa mujibu wa ripoti ya Makadirio ya Mahitaji ya Uhamisho Duniani kwa Mwaka 2026 iliyotolewa leo asubuhi jijini Geneva, Uswisi.
Ingawa idadi hiyo bado ni kubwa, mahitaji ya kila mwaka ya uhamishaji yamepungua kwa mwaka ujao kutoka milioni 2.9 mwaka huu 2025 hata wakati idadi ya wakimbizi duniani inaendelea kuongezeka. Hali hii inatokana zaidi na mabadiliko nchini Syria, ambapo baadhi ya wakimbizi wameamua kurudi kwa hiari ili kuanza upya maisha yao.
Kwa mwaka 2026, makundi makubwa ya wakimbizi watakaohitaji uhamishaji ni kutoka Afghanistan (573,400), Syria (442,400), Sudan Kusini (258,200), Sudan (246,800), Rohingya (233,300) na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC (179,500).
Nchi zinazowahifadhi wakimbizi wengi wanaohitaji kuhamishwa ni Iran (348,900), Uturuki (258,000), Pakistan (215,000), Ethiopia (213,950) na Uganda (174,000).
Uhamishaji ni suluhisho halisi linalosaidia kuepuka safari hatarishi, linaonesha mshikamano wa kimataifa na linakuza ushirikiano kati ya nchi wahisani na nchi za wenyeji. Pia husaidia kupunguza mzigo kwa mifumo ya kitaifa ya huduma katika nchi zinazowahifadhi wakimbizi, hasa wale wanaohitaji msaada mkubwa wa kibinadamu.
Hata hivyo, kwa mwaka 2025, inatarajiwa kuwa nafasi za uhamishaji zitafikia kiwango cha chini zaidi katika kipindi cha miongo miwili chini hata ya viwango vilivyoonekana wakati wa janga la coronavirus">COVID-19, ambapo nchi nyingi zilisitisha programu zao.
Kupungua huku kwa nafasi za uhamishaji kunaweza kuhatarisha mafanikio yaliyopatikana kwa juhudi za pamoja katika miaka ya hivi karibuni, na kuwaweka wakimbizi kwenye hatari zaidi.
Wito
UNHCR inatoa wito kwa nchi zinazotoa nafasi za uhamishaji kudumisha na kuongeza programu zao, sambamba na kuweka mifumo inayoweza kukabiliana na mabadiliko na kuruhusu ugawaji wa nafasi kulingana na mahitaji ya dharura ya wakimbizi kwenye njia kuu za kimataifa.
Kwa mwaka 2026, jumuiya ya kimataifa imejiwekea lengo la kuhamisha wakimbizi 120,000. Historia ya karibuni inaonesha kuwa lengo hili linaweza kufikiwa. Ingawa nafasi kubwa za uhamishaji ni muhimu kufikia malengo hayo, hata nafasi ndogo zitaendelea kuwa na mchango mkubwa, hasa iwapo mchakato wa kuchambua na kupitisha kesi unaweza kufanyika kwa haraka na kwa njia ya mbali.
Kwa zaidi ya miaka 70, UNHCR imekuwa ikisimamia uhamishaji kama njia muhimu ya kuokoa maisha ya wakimbizi wanaokabiliwa na hatari kubwa kama vile kurejeshwa kwa nguvu, ukatili, dharura za kiafya na vitisho vingine vikubwa na itaendelea kufanya hivyo.
Mwaka jana, 2024, licha ya changamoto nyingi, zaidi ya wakimbizi 116,000 walipata fursa ya usalama na kuanza upya maisha yao kupitia uhamishaji ulioungwa mkono na UNHCR. Kila nafasi ni ya thamani kubwa kwa anayekimbia hatari, inasisitiza UNHCR.