Maafisa wa UN waonya kuhusu kuongezeka kwa janga la kibinadamu na ukandamizaji wanawake Afghanistan
Maafisa wa UN waonya kuhusu kuongezeka kwa janga la kibinadamu na ukandamizaji wanawake Afghanistan
Mwakilishi Maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Afghanistan, Roza Otunbayeva, ameliambia Baraza la Usalama kuwa Waafghanistani wanaamini kuwa nchi hiyo “itakuwa katika hali mbaya zaidi” bila msaada wa kimataifa. “Kwa kiwango cha chini kabisa, uwepo wa kimataifa unatoa kipengele cha ulinzi na kuzuia,” amesema Otunbayeva.
Akilihutubia Baraza la Usalama leo (23 Juni), Otunbayeva pia amesema kuwa utekelezaji wa jukumu la UNAMA ni changamoto na wakati mwingine hatari. Amesema, “Mwezi Mei huu, wafanyakazi wetu wa kike wa taifa kadhaa walipokea vitisho vya wazi vya kuuawa kutoka kwa watu wasiojulikana, vikihusiana na kazi yao na Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan, UNAMA pamoja na mashirika mengine ya Umoja wa Mataifa, mifuko na programu, jambo lililotulazimu kuchukua hatua za muda za kuwalinda. Tulipozungumza na mamlaka halisi baadaye, walikana kuhusika, lakini pia ilionekana wazi kuwa watu hao wenye silaha walikuwa wakifanya kazi kwa ushirikiano katika mji mkuu bila kuchukuliwa hatua yoyote. Hili ni pigo kubwa kwa madai ya mamlaka halisi kuwa wameimarisha usalama na kuhakikisha usalama na heshima ya wanawake wa Afghanistan.”
OCHA
Joyce Msuya, Naibu Katibu Mkuu wa Masuala ya Kibinadamu, amesema, “Mmoja kati ya kila Waafghanistani watano ana njaa. Watoto milioni 3.5 wanakabiliwa na utapiamlo mkali. Inakadiriwa kuwa watoto milioni 3.7 hawapo shuleni, wakiwemo wasichana milioni 2.2 wenye umri wa zaidi ya miaka 11 waliopigwa marufuku kupata elimu kutokana na vizuizi vya mamlaka halisi.”
Msuya ameongeza kuwa vifo vya kina mama wajawazito nchini Afghanistan bado ni vya kiwango cha kutisha. “Kiwango cha vifo vya akina mama ni zaidi ya mara 2.5 ya wastani wa dunia,” aliwaambia wajumbe wa Baraza.
Licha ya kuongezeka kwa mahitaji, ufadhili wa kibinadamu unaendelea kuwa mdogo. “Tuko katikati ya mwaka, lakini mpango wa misaada ya kibinadamu umefadhiliwa chini ya asilimia 21, ikiwa na pengo la dola bilioni 1.9 za Marekani,” Msuya ameonya. “Kutokana na upungufu wa fedha, tumelazimika kutoa kipaumbele kwa mahitaji muhimu zaidi ya watu milioni 12.5 katika maeneo yaliyoathiriwa vibaya zaidi, kutoka lengo la awali la watu milioni 16.8.”
Mkuu wa UN Women ambalo ni Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya wanawake, Sima Sami Bahous, amesisitiza athari mbaya za vizuizi dhidi ya wanawake wa Afghanistan. “Takwimu za karibuni kutoka kwa Kielelezo cha Jinsia cha Afghanistan cha UN Women, kilichozinduliwa wiki iliyopita, zinathibitisha hali mbaya: karibu asilimia 78 ya wanawake wa Afghanistan wenye umri wa miaka 18 hadi 29 hawafanyi kazi, hawasomi, wala hawajifunzi; jambo linalofanya Afghanistan kuwa moja ya nchi zenye pengo kubwa na linaloongezeka kwa kasi kati ya jinsia duniani,” amesema Bahous.
Ameongeza kuwa kuna ongezeko la kutengwa kiuchumi na ukatili wa kijinsia. “Wanaume wana uwezekano mkubwa mara tatu kuliko wanawake kumiliki akaunti ya benki au kutumia huduma za fedha kupitia simu. Kiwango cha ukatili wa wapenzi wa karibu kinaongezeka. Marufuku ya elimu pekee inakadiriwa kugharimu Afghanistan dola bilioni 1.5 kufikia mwaka 2030,” ameongeza.
Kwa niaba ya Ujumbe wa Afghanistan katika Umoja wa Mataifa, Kaimu Balozi Naseer Ahmad Faiq amelaani ukandamizaji unaoendelea nchini humo. “Karibu miaka minne tangu Taliban warejee madarakani chini ya utawala usio jumuishi, wa kimabavu na usio halali, watu wa Afghanistan, wakiwa katika hali ya kukata tamaa na kutojua hatma yao, wanaendelea kuvumilia mojawapo ya migogoro mikubwa zaidi ya haki za binadamu na kibinadamu duniani,” amesema Faiq.
“Ukosefu wa vita rasmi hautakiwi kuficha uzito wa mateso yanayoendelea nchini. Wananchi wanaishi chini ya ukandamizaji unaozidi kuongezeka, umaskini uliotapakaa na ubomoaji wa kimfumo wa haki, hasa kwa wanawake na wasichana,” ameongeza.
Faiq amekaribisha juhudi mpya za Umoja wa Mataifa katika kusaidia suluhisho la kisiasa, lakini ameeleza wasiwasi kuhusu pendekezo la hivi karibuni. “Tunakaribisha juhudi mpya chini ya Umoja wa Mataifa katika kuunga mkono njia jumuishi kulingana na mapendekezo ya Tathmini Huru iliyoidhinishwa na Baraza hili. Katika muktadha huu, tunalitambua wazo la rasimu ya njia ya ‘mosaic’. Hata hivyo, bado kuna wasiwasi mkubwa,” amesema.
“Rasimu ya njia ya ‘mosaic’, kama ilivyo sasa, haimilikiwi kwa dhati na Wafghanistani. Vikosi vya kidemokrasia vya Afghanistan, wanasiasa, asasi za kiraia, mashirika ya wanawake na wawakilishi wa vijana hawajashirikishwa kwa maana halisi katika uundaji wake,” Faiq ameliambia Baraza.