Ufuatiliaji Iran na uhamasishaji nishati ya nyuklia kwa amani - Wajibu wa IAEA wafafanuliwa

Ufuatiliaji Iran na uhamasishaji nishati ya nyuklia kwa amani - Wajibu wa IAEA wafafanuliwa
Siku chache kabla ya Israel kuzindua mashambulizi ya mabomu dhidi ya Iran, shirika la Umoja wa Mataifa linalosimamia nishati ya atomiki na hivyo linafuatilia shughuli za nyuklia za Iran (IAEA) lilitahadharisha kwamba Iran ilikuwa inakiuka ahadi zake za kutokueneza silaha za nyuklia.
Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA) lilianzishwa mwaka 1957, kufuatia hofu ya kimataifa baada ya matumizi ya kwanza ya silaha za nyuklia na wasiwasi juu ya kuenea kwa teknolojia ya nyuklia. IAEA ni taasisi inayojitegemea ndani ya mfumo wa Umoja wa Mataifa na hushughulika na masuala mbalimbali kama vile usalama wa chakula, udhibiti wa saratani, maendeleo endelevu, na matumizi mengine ya amani ya nishati ya nyuklia.
Majukumu yake mengine makuu, ingawa hayafahamiki sana kwa umma, ni utekelezaji wa mikataba ya “uangalizi wa nyuklia” (safeguards) na nchi mbalimbali. Mikataba hii ni ya hiari na inalenga kuzuia uenezaji wa silaha za nyuklia kwa kuthibitisha kwa njia huru kama nchi zinatekeleza ahadi zao za kutokueneza nyuklia. Kufikia mwaka 2024, takribani nchi 182 zina mikataba ya uangalizi na IAEA.

Katika hotuba yake ya tarehe 9 Juni kwa bodi ya shirika hilo, Mkurugenzi Mkuu wa IAEA Rafael Grossi alieleza matokeo yanayozua wasiwasi kuhusu utiifu wa Iran kwa makubaliano ya nyuklia ya kimataifa.
“Iran imeshindwa kujibu au kutoa majibu yenye uhalali wa kisayansi kwa maswali yetu,” Bwana Grossi aliieleza bodi yenye nchi wanachama 35. Aliongeza kuwa Iran imejaribu kusafisha maeneo ambayo sasa IAEA imebaini yalihusishwa na mpango wa nyuklia ulioelekezwa vizuri tangu mwanzoni mwa miaka ya 2000.
“Mradi Iran haijashirikiana ipasavyo katika kutatua masuala ya uangalizi yaliyosalia, IAEA haitaweza kuthibitisha kwa uhakika kuwa mpango wake wa nyuklia ni wa amani pekee,” alionya.
Bwana Grossi pia alieleza hofu kuhusu mkusanyiko wa zaidi ya kilo 400 za urani iliyoimarishwa kwa kiwango cha juu ambayo ni moja ya viambato muhimu katika utengenezaji wa bomu la nyuklia.

Wajibu Mkuu wa IAEA nchini Iran unagawanyika katika maeneo manne:
1. Ufuatiliaji
IAEA hutekeleza mikataba ya uangalizi chini ya Mkataba wa Kutokueneza Silaha za Nyuklia (NPT), mkataba wa kimataifa unaolenga kuzuia uenezaji wa silaha hizo. Ingawa mikataba mingi ni ya nchi zisizo na silaha za nyuklia, IAEA pia ina mikataba na India, Pakistan na Israel – mataifa ambayo si wanachama wa NPT.
Iran, kama mwanachama asiye na silaha za nyuklia, hairuhusiwi kumiliki silaha hizo na inapaswa kuruhusu IAEA kufanya ukaguzi wa mara kwa mara, hata kwa notisi fupi.
Maeneo yanayokaguliwa ni pamoja na vituo vya nyuklia kama Natanz, Fordow na Isfahan, kuhakikisha kuwa urani haitumiki kwa kutengeneza silaha.
Mnamo Juni 9, Bwana Grossi alisema chembe za urani zilizotengenezwa na binadamu zilipatikana katika maeneo mengine matatu yasiyojulikana: Varamin, Marivan na Turquzabad. Iran ilishindwa kutoa maelezo ya kisayansi kuhusu uwepo wa chembe hizo licha ya miaka ya mashauriano.
2. Ripoti
IAEA hutoa ripoti za mara kwa mara kwa bodi yake kuhusu shughuli za nyuklia za Iran kwa kutumia ukaguzi, vifaa vya kufuatilia, sampuli za mazingira, na picha za setilaiti. Kwa nchi zinazoangaliwa kwa karibu – kama Iran – ripoti hutolewa kila robo mwaka.
Ikiwa nchi haitekelezi masharti ya IAEA (kama kuzuia ukaguzi au kushindwa kueleza uwepo wa urani), shirika linaweza kuwasilisha suala hilo kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, linaloweza kuibua hatua za kidiplomasia au vikwazo.

3. Mazungumzo ya Kidiplomasia
IAEA hutetea suluhisho la kidiplomasia na umuhimu wa mazungumzo kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran. Bwana Grossi amekuwa akikutana moja kwa moja na viongozi wa Iran na wadau wa kimataifa ili kudumisha mawasiliano na uwazi.
Tarehe 13 Juni, alipohutubia Baraza la Usalama, alisema IAEA ilikuwa katika mawasiliano ya karibu na Mamlaka ya Kudhibiti Nyuklia ya Iran kutathmini hali ya vituo vilivyoathiriwa na kutathmini athari kwa usalama wa nyuklia.
4. Usalama na Ulinzi
Sehemu hii ni muhimu kwa dhamira ya IAEA ya kuzuia ajali za nyuklia, kuhakikisha matumizi ya amani ya nishati ya nyuklia, na kulinda watu na mazingira.
IAEA hushirikiana na Iran kuhakikisha vituo kama Natanz, Fordow na Esfahan vinaendeshwa kwa usalama kwa kupitia usanifu wa vituo, hatua za ulinzi dhidi ya mionzi, na mipango ya dharura.
Baada ya mashambulizi ya Israeli mnamo Juni 2025, IAEA ilithibitisha kuwa Natanz iliathiriwa lakini haikuripoti viwango vya juu vya mionzi. Hata hivyo, ilisisitiza kuwa shambulizi lolote la kijeshi kwenye kituo cha nyuklia ni ukiukwaji wa sheria za kimataifa na ni hatari kwa watu na mazingira.