Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sudan: Türk atahadharisha kuhusu kuongezeka kwa machafuko kwa kiwango cha janga

Wanawake na watoto waliokimbia makazi yao huko Tawila, Sudan, wakipika moto wazi.
© UNICEF/Mohammed Jamal Zaidi ya watu 700,000 wamekimbia makazi yao kutokana na ghasia huko Darfur, Sudan.

Sudan: Türk atahadharisha kuhusu kuongezeka kwa machafuko kwa kiwango cha janga

Wahamiaji na Wakimbizi

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Volker Türk, ameonya leo kuhusu athari mbaya zinazotokana na kuendelea na kuongezeka kwa mapigano katika maeneo ya Darfur Kaskazini na Kordofan nchini Sudan, ambako vimeripotiwa vifo vya raia, unyanyasaji wa kingono, utekaji nyara, na uporaji katika maeneo kadhaa.

“Mapigano ya hivi karibuni na hatari kubwa ya kuzidi kwa hali ya mgogoro huu ambao tayari ni wa kikatili na unaosababisha vifo vingi vinazua wasiwasi mkubwa kuhusu ulinzi wa raia, huku ukiukaji wa haki za binadamu ukiendelea kufanyika pasipo kuwajibika,” amesema Kamishna Mkuu akiwa Geneva, Uswisi.

Mnamo tarehe 15 Juni, baada ya kuzingirwa kwa mwaka mzima, Kikosi cha Rapid Support Forces (RSF) kilianzisha shambulio lingine dhidi ya mji wa El Fasher, kufuatia miezi ya kuhamasisha wapiganaji zaidi  ikiwa ni pamoja na kuandikisha watoto kote Darfur. Operesheni hiyo, yenye lengo la kuuteka mji huo kwa mashambulizi ya ardhini, inafanana na mashambulizi ya RSF kwenye kambi ya Zamzam ya wakimbizi wa ndani (IDPs) mwezi Aprili, ambayo ilisababisha vifo vya mamia ya raia, visa vya unyanyasaji wa kingono kwa kiwango kikubwa, na janga la kibinadamu.

Mwanamke aliyevaa kitambaa cha maua ya bluu kichwani akiwa amebeba rundo la vifaa vya misaada ya kibinadamu, ikiwa ni pamoja na chombo kikubwa cheupe cha povu na vitalu vya chakula, nchini Sudan.
© IOM Familia zilizofurushwa katika Bandari ya Sudan wapokea vifaa vya utunzaji wa nyumbani kutoka kwa IOM.

Katika jimbo la Kordofan Kusini, raia pia wamekwama katikati ya mapigano kati ya pande zinazowania udhibiti wa mji wa kimkakati wa Al Debibat. Wakati huohuo, katika jimbo la Kordofan Kaskazini, inaripotiwa kuwa RSF wameuzingira mji wa El Obeid, unaodhibitiwa na Jeshi la Sudan (SAF) na makundi washirika, na huenda wakaufanyia shambulio siku chache zijazo, kama ilivyotangazwa na kamanda wa RSF.

“Tunajua madhara ya kuongezeka kwa mapigano haya,” amesema Türk. “Kwa muda mrefu sasa, dunia imeshuhudia ukiukaji wa hali ya juu wa haki za binadamu unaoendelea Sudan na mateso makubwa kwa raia wake. Raia lazima walindwe kwa gharama yoyote ile. Ukiukaji na uhalifu lazima uchunguzwe kwa kina, na waliohusika wawajibishwe,” ameongeza.

Wito

“Ninazitaka pande zote kuhakikisha kuwa raia wanaweza kuondoka kwa usalama kutoka El Fasher, Al Debibat, na El Obeid, pamoja na maeneo mengine ambako wanaweza kuwa wamekwama kutokana na machafuko. Pande zote lazima ziepuke kushambulia maeneo ya raia, hatimaye waweke silaha chini na kusitisha mapigano,” amesema Türk.

“Naziomba nchi zote kutumia ushawishi wao kusukuma kwa ajili ya suluhisho la kisiasa la kudumu, na kuhakikisha kuwa pande zinazopigana zinaheshimu sheria ya kimataifa ya kibinadamu. Pia nazitaka nchi hizi kusukuma kusitishwa kwa mtiririko wa silaha kuingia nchini Sudan, na kuzuia biashara zinazochochea mgogoro huu.”