Mshikamano na wakimbizi uwe kwa vitendo na si maneno matupu: UN
Mshikamano na wakimbizi uwe kwa vitendo na si maneno matupu: UN
Leo ni Siku ya Wakimbizi Duniani, mwaka huu ikibeba maudhui “Mshinamano na wakimbizi” na Umoja wa Mataifa umetaka mshikamano huo kwa vitendo wakati idadi ya watu wanaolazimika kufungasha virago na kukimbia makayo yao ikifikia kiwango cha kihistoria.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres na Kamishna Mkuu wa wakimbizi na Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi duniani UNHCR Filippo Grandi wametoa wito wa dharura wa hatua thabiti na mshikamano wa kweli, wakionya kuwa dunia inashindwa kuwasaidia mamilioni ya watu waliokimbia vita, ukatili na mateso.
Kila hadithi ya mkimbizi ni ya masikitiko
“Kila mtu anabeba hadithi ya huzuni kubwa ya familia kung’olewa na maisha kutumbukia gizani,” amesema Katibu Mkuu Guterres katika ujumbe wake. “Wengi wanakumbana na milango iliyofungwa na mawimbi ya chuki dhidi ya wageni,” ameonya, akibainisha kuwa kuanzia Sudan hadi Ukraine, na kutoka Haiti hadi Myanmar, idadi ya watu waliolazimika kukimbia kwa ajili ya kunusuru uhai wao inaongezeka huku msaada wa kimataifa ukizidi kupungua.
Filippo Grandi: Wakimbizi wanawekewa dosari isivyo haki
Mkuu wa UNHCR Grandi ameangazia hali ya kutisha ya ufurushwaji wa watu duniani ambapo amesema zaidi ya watu milioni 122 wamelazimika kuhama makazi yao.
“Kushindwa kwa jamii ya kimataifa kumaliza migogoro kumeendelea kusababisha mateso yasiyoelezeka,” amesema akiwa Syria, ambako anakutana na familia zilizorejea nyumbani baada ya zaidi ya muongo mmoja wa ukimbizi.
“Hata hivyo, watu wasio na hatia wanaokimbia mashambulizi wanalaumiwa isivyo haki, hali inayowafanya washindwe kupata hifadhi salama na kujenga upya maisha yao.”
Mshikamano unapaswa kuwa kwa vitendo
Viongozi wote wawili wamesisitiza kuwa mshikamano wa kweli unahitaji hatua, si kauli za huruma pekee.
Guterres amehimiza nchi kulinda haki ya kuomba hifadhi, kuongeza misaada ya kibinadamu na ya maendeleo, na kuwekeza katika suluhu za muda mrefu kama elimu, kazi zenye staha na usawa wa haki.
“Kuwa mkimbizi si uamuzi wa mtu binafsi,” amesema. “Lakini jinsi tunavyokabiliana nao, ni uamuzi wetu. Basi tuchague mshikamano. Tuchague ujasiri. Tuchague utu.”
Kukatwa kwa misaada kunatiashia maisha
Grandi ameonya kuwa ukatwaji mkubwa wa misaada ya kibinadamu “ni kukata pumzi na kuweka maisha ya mamilioni ya watu hatarini”.
Ameendelea kusema kuwa “Ni muhimu sasa zaidi kuliko wakati mwingine wowote kuonesha mshikamano wa kweli kwa wakimbizi sio kwa maneno tu, bali kwa hatua za dharura.”
Amezipongeza nchi na jamii ambazo licha ya changamoto za kiuchumi, zinaendelea kufungua milango yao kwa wakimbizi kwa “vitendo vya huruma na utu usio na kifani.”
Dalili za matumaini Syria katikati ya magofu
Akiwa Syria, ambako watu milioni 2 tayari wamerudi makwao tangu kuanguka kwa utawala wa Assad mwezi Desemba 2024, Grandi ameeleza kuona matumaini ya kina.
“Furaha yao ya kurejea miongoni mwa nyuso walizozikosa kwa miaka mingi licha ya changamoto nyingi ni ushahidi wa shauku kubwa ya wakimbizi kurudi nyumbani,” amesema.
Ameongeza kuwa kurejea huko kumekuwa kukiwezekana tu kutokana na “mshikamano kutoka kwa majirani, jamii, na wahudumu wa kibinadamu.”
Wito: tugawane majukumu, turejeshe heshima
Umoja wa Mataifa umetoa wito kwa serikali, mashirika ya kifedha ya kimataifa, sekta binafsi, na watu binafsi kushiriki katika jukumu la kuwalinda wakimbizi. “Tukifanya hivyo,” Grandi alihitimisha, “naahidi kwamba wakimbizi wataonesha ujasiri wao, ari yao na ubunifu wao katika kujenga kesho iliyo bora na yenye matumaini kwa wote.”