Baada ya WFP kupunguza posho kwa wakimbizi Kakuma, mashirika ya kiraia yaonesha nuru

Baada ya WFP kupunguza posho kwa wakimbizi Kakuma, mashirika ya kiraia yaonesha nuru
Kuelekea siku ya wakimbizi duniani kesho Juni 20, tunamulika kambi ya Kakuma, kaunti ya Turkana huko Kaskazini-Magharibi mwa Kenya ambako wakimbizi kutoka mataifa mbali mbali wamesaka hifadhi wakikimbia ukosefu wa usalama kwenye nchi zao.
Miongoni mwa in Saras Katenda, mkimbizi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC ambaye alikuwa mwandishi wa habari jimboni Kivu Kusini, ila alilazimika kukimbia kwa sababu ya hali ya usalama.Walisafiri katika mazingira magumu kutokea Kivu Kusini hadi Uganda ndipo wakafanikiwa kuvuka mpaka na kuingia Kenya.
Kutoka mwandishi wa habari hadi kutunga shanga
Saras alipowasili Kalobeyei alipata usaidizi na kufadhiliwa na shirika la Inkomoko kuanza biashara ya kutunga shanga akishirikiana na wanawake wengine wakimbizi.
Baadhi wamejengewa nyumba za mawe ila wapo wanaojisitiri kwenye mahema maalum yaliyoimarishwa kwa mapaa ya mabati kuzuia upepo mkali.
Saras anaishi kwenye hema kwa hisani ya mashirika ya msaada ya Umoja wa Mataifa, mathalani lile la kuhudumia wakimbizi, UNHCR. Ana imani mambo yatabadilika akisema, “kwa sisi wa kijiji cha tatu bado hatujajengewa nyumba. Wale wa vijiji vya kwanza na pili wamejengewa nyumba za mawe. Wako vizuri. Kwa sisi bado lakini muhimu tuna amani maana kilichotutoa Kongo ni amani na hatujali. Siku watapata jinsi watatujengea tu.”

Matumaini ya kunufaika na siku ya wakimbizi
Saras anasema kwamba, “katika maadhimisho ya siku ya wakimbizi mwaka huu ana Imani mambo yatabadilika na,“Siku hii ni muhimu Kwani inatupatia nafasi kuonyesha tunavyofanya kambini. Kupitia Inkomoko kwa mfano inaweza kuwaunga mkono wanawake kuwawakilisha. Sisi kama wakimbizi tunaweza kupata fursa huko kuwashukuru UNHCR na serikali ya Kenya kwa kutupokea na kutulinda vizuri na Inkomoko kwa kuendelea kutushika mkono sisi kama wanawake.”
Bamba Chakula – Mradi wa WFP
Wanaopata hifadhi hapa walikuwa wakipokea fedha taslimu mkononi ila kwa sasa mfumo huo umesitishwa. Kwa sasa watapokea bidhaa za matumizi kwani hakuna fedha walizotengewa.Awali walipokea dola 17 kila mwezi kugharamia bidhaa ambazo hazipo kwenye mpango wa chakula cha msaada.
Bamba chakula ni mpango wa kupokea fedha kutoka WFP unaowawezesha wakimbizi kulipia bidhaa ambazo hawapokei kwenye mpango wa msaada.
Wafanyabiashara waliokopesha bidhaa sasa mashakani
Lakini tangu mpango wa Bamba Chakula usitishwe, mambo yamebadilika kwani sasa wakimbizi hawawezi kulipia bidhaa walizochukua kwa mkopo.
Claude Niyonzima, mfanyabiashara na mkimbizi anayetokea Burundi anasema, “walikuwa wanagawa fedha watu wananunua bidhaa. Wengine hii fedha haiwatoshi kwa hiyo wanakuja kukopa. Tunawapa bidhaa kwa mkopo. Sasa hivi fedha wamezikata mara moja, nasi fedha zetu zimepotea kwenye biashara. Wanakuja wanasema najua unanidai lakini sijui vile nitakulipa. Nabaki sina la kufanya. Hata nikienda kwake hana kitu cha kunipa. Tunasubiri tu labda mambo yakibadilika tutapata afueni.”
Inkomonko na mshikamano na wakimbizi Kakuma
Claude Niyonzima amefadhiliwa na shirika la kiraia la Inkomoko. Ili kuwashika mkono wakimbizi, mashirika ya kijamii yameingilia kati kuwapa mikopo ya kufadhili biashara. Samuel Mwangangi ni Meneja wa Uwekezaji katika shirika la Inkomoko katika kambi ya Kakuma na anasisitiza wakimbizi wanajitahidi.
Anasema “tulipoanza kuwafadhili wengi wao hawakuweza kupata mikopo kwasababu ya vigezo vilivyoko vya kukopesha fedha.Wakimbizi ni wafanyabiashara wavumilivu na wanajitahidi kulisogeza gurudumu la maisha katika mazingira magumu.Tungependa kuimarisha uhusiano wetu na wao ili waweze kuendelea kupata mikopo na kujisimamia.”
Posho ya WFP imepunguzwa kwa asilimia 30
Kila gunia lina nafaka kama mchele na aina ya choroko ambazo zinaweza kupatia familia mlo wa siku kadhaa.Kuanzia mwezi huu wa Juni, shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula duniani, WFP limepunguza hadi asilimia 30 kiwango cha posho inayopatia wakimbizi laki saba ishirini.
Hiki ni kiwango kidogo zaidi kuwahi kushuhudiwa nchini Kenya.Hivi karibuni, Marekani ilipunguza mabilioni ya dola ilizochangia kwenye mfuko wa misaada ya kibinadamu kote ulimwenguni.Kiwango hicho ni sawa na nusu ya mahitaji ya misaada ya kibinadamu na kiasi ya humusi moja ya bajeti ya Umoja wa Mataifa.
Vikapu na shanga za matumaini
Wanawake wanafuma vikapu kujipatia riziki, huku wanapokea mikopo kidogo kutoka Inkomoko inayoshirikiana na mashirika ya Umoja wa mataifa kwa njia moja au nyengine. Sara Ngonzimana anayetokea Burundi amekuwa Kalobeyei kwa miaka miwili. Anashusha pumzi kwa kiasi..kwavile,’’Tunatengeneza vikapu. Vikapu vinatusaidia kupata chakula cha watoto nyumbani. Wanaviuza, tunachukua pesa tunawanunulia watoto chakula nyumbani. “

Mkimbizi na ubunifu wa majiko banifu
Baadhi ya wakimbizi wamefanikiwa kutumia ujuzi wao kubadili maisha kambini. Miongoni mwao ni Vincent Obeli anatokea DRC ni muasisi wa kampuni ya Green Mind inayotengeza majiko banifu yanayotumia mkaa kidogo na kulinda mazingira.
Bwana Obeli anaamini kila mkimbizi ana mchango muhimu hasa pale msaada unapopungua kwani,“Wakati usaidizi unapungua , kwangu mimi ni wakati wa sisi kufikiria kufanya zaidi ya kile tulichokuwa tunapokea. Kama tunaweza kupata nafasi ya kufungua biashara , aliyekuwa amepungukiwa anaweza kupata usaidizi kwa kuajiriwa kambini. Kwangu sio nafasi ya kukata tamaa ila kufikiria zaidi ili kuepukana na changamoto anazopata.”