Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Umaskini: Bila maendeleo endelevu, hakuna amani: Guterres

Wasichana watatu wadogo wamesimama mbele ya hema la muda katika kambi ya wakimbizi nchini Yemen.
© UNFPA Yemen Watoto wanacheza kwenye kambi huko Yemen kwa watu waliofurushwa makwao na migogoro na mabadiliko ya tabianchi.

Umaskini: Bila maendeleo endelevu, hakuna amani: Guterres

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Umaskini, kutokuwepo kwa usawa, na ukosefu wa maendeleo vinachochea vita, amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres akionya kuwa endapo hali itaendelea kama ilivyo, ifikapo mwaka 2030, theluthi mbili ya watu maskini duniani watakuwa wakiishi katika nchi zilizo na migogoro au hali tete.

“Moto wa migogoro mara nyingi huendelezwa na umaskini wa muda mrefu na ongezeko la tofauti za kijamii,” amesema Guterres, mbele ya Baraza la Usalama leo Alhamisi, Juni 19.

Guterres ameshiriki katika mdahalo wa wazi kuhusu umaskini, ukosefu wa maendeleo, na migogoro, ambapo amesisitiza kuwa amani ya kudumu inahitaji maendeleo endelevu, na kuitaka jamii ya kimataifa kuongeza juhudi katika kupambana na ukosefu wa usawa na umaskini kwa ajili ya uthabiti wa kimataifa.

Migogoro huharibu maisha, huondoa mafanikio ya maendeleo, na kuwalazimisha mamilioni ya watu kuyakimbia makazi yao, na hivyo kuongeza umaskini na ukosefu wa haki.

Umaskini huzalisha kukata tamaa

“Umaskini huzalisha kukata tamaa; kukata tamaa kunachochea machafuko. Na machafuko huvunja mshikamano wa kijamii, huleta kutoaminiana, hofu na vurugu,” ameeleza Guterres.

Mambo haya huzidishwa na ukiukwaji wa haki za binadamu, uhalifu na rushwa vinavyoibuka katika mazingira ya machafuko na dharura, pamoja na majanga ya tabianchi yanayosababishwa na shughuli za kibinadamu, hali inayochangia kuenea kwa ugaidi, ameongeza.

Guterres amesisitiza kuwa kati ya nchi kumi zenye viwango vya chini zaidi vya maendeleo ya binadamu, tisa ziko kwenye migogoro jambo ambalo “si bahati mbaya,” alisema.

Kati ya watu milioni 700 wanaoishi katika umaskini uliokithiri, asilimia 40 wako katika maeneo yenye migogoro au hali tete. Aidha, watu zaidi ya milioni 120 duniani wamekimbia makazi yao ndani ya nchi zao.

Mama mmoja wa Sudan Kusini akiwapa watoto wake uji wa mtama katika kijiji cha vijijini.
FAO/Stefanie Glinski Nchini Sudan Kusini, mama akiwapa watoto wake uji wa mtama.

Kutoaminiana na mgawanyiko wa kisiasa wa kimataifa

Katibu Mkuu amekiri kuwa suluhisho linazidi kuwa gumu kutokana na mgawanyiko wa kisiasa duniani na hali ya kutoaminiana. “Uchumi wa dunia unapungua kasi, mvutano wa kibiashara unaongezeka, na misaada inapunguzwa, huku matumizi ya kijeshi yakipanda,” ameonya.

Ameeleza kuwa ikiwa hali ya sasa itaendelea, theluthi mbili ya watu maskini duniani watakuwa wakiishi katika nchi zenye migogoro ifikapo 2030. “Kadri nchi inavyozidi kuwa mbali na maendeleo jumuishi na endelevu, ndivyo inavyokaribia kwenye hali ya machafuko au migogoro.”

Hakuna kinga bora kuliko kuwekeza katika maendeleo

Katika muktadha huu, Guterres amesisitiza umuhimu wa kazi ya Umoja wa Mataifa inayojikita kwenye nguzo tatu: amani, maendeleo, na haki za binadamu.

“Tunaongozwa na kanuni rahisi: kuzuia ni tiba bora kwa hali ya machafuko na migogoro. Hakuna njia bora ya kuzuia migogoro kuliko kuwekeza katika maendeleo,” amesema.

Guterres ameeleza kuwa maendeleo ni ngome ya kwanza dhidi ya migogoro. Hata hivyo, amesikitika kuwa kasi ya kufikia maendeleo endelevu inazidi kupungua.

Miaka kumi tangu kupitishwa kwa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), theluthi mbili ya malengo hayo hayapo katika njia sahihi ya kutekelezwa, na nchi zinazoendelea zinahitaji zaidi ya dola trilioni 4 kila mwaka ili kuyafikia.

Injini ya maendeleo inakosa pumzi

“Nchi zinazoendelea zinateseka kwa ukosefu wa nafasi ya kifedha, madeni yasiyoweza kulipika, na ongezeko kubwa la bei. Injini ya maendeleo inakosa pumzi,” amesisitiza Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.

Kwa mantiki hiyo, ametaja Mkutano wa Ufadhili wa Maendeleo utakaofanyika tarehe 30 Juni kuwa ni “wakati muhimu wa kutengeneza na kuimarisha injini hii muhimu.”

Guterres ametoa wito kwa mataifa yanayokumbwa na matatizo ya kulipa madeni yao kupewa nafuu, na akatoa mwito wa kufanyika marekebisho ya mfumo wa kifedha wa kimataifa ili uakisi hali halisi na mahitaji ya dharura ya nchi zinazoendelea.

Amesisitiza pia umuhimu wa kuipa kipaumbele usalama wa chakula, elimu, afya, kazi yenye heshima, na ulinzi wa kijamii.

Pia amehimiza kuwekeza katika teknolojia rafiki kwa mazingira na uhimilivu wa mabadiliko ya tabianchi; ujenzi wa barabara, mifumo ya maji na chakula; kuhakikisha upatikanaji wa umeme na mtandao kwa wote; kuunda mifumo ya haki na utawala ya kuaminika; na kufungua fursa kwa ushiriki wa wanawake na vijana.

Mwanamke kutoka DRC amembeba mtoto mgongoni huku akimtazama mtoto mwingine.
UNDP/Almeras-Martino Hali ya maisha ya kaya huko Kivu Kaskazini katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ni duni, huku nyumba saba kati ya kumi zikiishi katika umaskini.

Amani hujengwa katika jamii

“Amani haijengwi katika kumbi za mihadhara”, amesisitiza Katibu Mkuu Guterres na kuongeza, “hujengwa mashuleni, katika kliniki, katika jamii. Amani hujengwa pale watu wanapokuwa na matumaini na fursa ya kushiriki katika kujenga maisha yao ya baadaye,” amesema.

“Kuwekeza katika maendeleo leo ni kuwekeza katika amani ya kesho. Tufufue tena ahadi yetu ya mshikamano na ushirikiano wa kimataifa,” amehitimisha Katibu Mkuu.