Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukanda wa Gaza: Wakati usambazaji wa mafuta unaisha, timu za misaada zinaonya juu ya hatari ya janga kubwa

Watoto katika kitongoji cha Shujaia cha Jiji la Gaza wamesimama karibu na pampu ya maji katika kambi ya muda.
© UNOCHA/Olga Cherevko Watoto wanakusanya maji kaskazini mwa Gaza

Ukanda wa Gaza: Wakati usambazaji wa mafuta unaisha, timu za misaada zinaonya juu ya hatari ya janga kubwa

Amani na Usalama

Baada ya zaidi ya siku 100 ya kuzuiliwa kabisa kwa mafuta kwa Gaza eneo la palestina linlaokaliwa kimabavu na Israeli, mashirika ya Umoja wa Mataifa ambayo bado yapo katika eneo hilo lililoharibiwa yamesema kwamba huduma muhimu zinaelekea kuzimwa "saa chache tu kutoka sasa”.

Akizungumza kutoka mji wa Gaza, kaskazini mwa eneo hilo, Olga Cherevko kutoka Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu na Misaada ya Dharura OCHA amesema kuwa pampu za maji zimeshakatika katika kituo kimoja cha watu waliofurushwa makwao ohapo jana Jumatano "kwa sababu hakuna mafuta."

"Tunakwama kweli ikiwa hali haitabadilika saa chache tu kutoka sasa tutashuhudia kuporomoka kwa huduma na kuzimwa kwa vituo vingine vingi kama mafuta hayataingia au hatutaweza kupata mafuta zaidi mara moja," amesema akizungumza na hababari za Umoja wa mataifa

Katika taarifa yake ya hivi karibuni kuhusu hali ya dharura, OCHA ilisema kuwa bila kuingia mara moja kwa mafuta au kufikia akiba zilizopo, asilimia 80 ya vituo vya huduma za dharura Gaza, muhimu kwa ajili ya uzazi na dharura za matibabu, vitazimwa.

Moshi mweusi unaongezeka juu ya mandhari ya mijini ya Jiji la Gaza, haswa kitongoji cha Shujaia, kufuatia milipuko.
© UNOCHA/Olga Cherevko Moshi unaotokana na milipuko unapanda kutoka kitongoji cha Shujaia cha Gaza City.

Wengi wameuawa wakitafuta misaada

Hali hii inakuja huku mamlaka za Gaza zikiripoti kuwa watu 15 waliuawa karibu na kituo cha ugawaji misaada katikati mwa ukanda leo Alhamisi.

Jumanne, video zisizothibitishwa zilizoenea kwenye mitandao ya kijamii zilionesha maiti zikiwa barabarani karibu na kituo cha misaada mjini Khan Younis kusini, zikiwa zimejeruhiwa baada ya milipuko wa risasi na makombora.

Kupata chakula ni changamoto kila siku kwa watu wa Gaza wanaoendelea kuwa katika hali ya kukata tamaa ambao "wana matumaini ya kupata chakula ili wasiangalie watoto wao wakifa na njaa mbele yao," Bi Cherevko amefafanua.

Ameongeza kuwa, "Nilizungumza na mwanamke mmoja siku chache zilizopita ambaye aliniambia alikwenda na rafiki yake ambaye alikuwa na ujauzito wa miezi tisa kwa matumaini ya kupata chakula. Hawakufanikiwa kwa sababu walikuwa na hofu kuingia maeneo ambapo kunaweza kuwa na matukio kama yale yaliyoripotiwa siku za hivi karibuni."

Harakati ya kutafuta makazi salama

Huko Gaza City, Bi. Cherevko wa OCHA amesema hali katika vituo vya hifadhi Gaza sasa ni mbaya kabisa na vimefurika na watu wanaendelea kuja kutoka kaskazini kila wakati. Wengine pia wanarejea kaskazini, labda ili kuwa karibu na maeneo ya kuingia kwa mabasi ya misaada.

Kiasi cha misaada kinachoingia Gaza leo ni kidogo sana na hakitoshi, kiasi kidogo kuliko mabasi 600 kwa siku yaliyoingia kabla ya vita kuanza Oktoba 2023. Katika taarifa yake ya hivi karibuni, OCHA iliripoti kuwa "nja na uwezekano mkubwa wa njaa vipo katika ukanda huo.

Akina mama 55,000 wenye ujauzito sasa wanakabiliwa na hatari ya kuharibika mimba, kukufa kwa watoto tumboni au kuzaliwa kwa watoto waliopungukiwa lishe kutokana na ukosefu wa chakula.

Chungu cheusi cha kupikia kimewekwa kwenye jiko la muda la chuma juu ya makaa ya moto katika kitongoji cha Shujaia cha Jiji la Gaza.
© UNOCHA/Olga Cherevko Wenyeji wa Gaza wanatatizika kupata chakula cha kutosha.

Ongezeko la njaa

"Kwa kiasi kidogo cha misaada kinachoingia, kila mtu anaendelea kukumbwa na njaa na watu wanahatarisha maisha yao kila mara ili kupata chakula," Bi. Cherevko anaendelea.

"Unakula au unakubali kufa kwa njaa."

Baada ya zaidi ya miezi 20 ya vita, vilivyozushwa na mashambulizi ya kigaidi yaliyoongozwa na Hamas nchini Israel, asilimia 82 ya eneo la Gaza ni eneo la kijeshi la Israel au limeathiriwa na amri za kuhama.

Miezi mitatu tangu mapigano yarejee tarehe 18 Machi, watu zaidi ya 680,000 wamehama mara mpya. "Kwa kuwa hakuna mahali salama pa kwenda, watu wengi wamekimbilia kila sehemu, ikijumuisha maeneo ya makazi yaliyojaa watu, makazi ya muda, majengo yaliyoharibika, barabara na maeneo wazi," imesema OCHA