Kudorora kwa usalama duniani kuchochea matumizi ya mihadarati na uhalifu: Ripoti ya UNODC 2025
Kudorora kwa usalama duniani kuchochea matumizi ya mihadarati na uhalifu: Ripoti ya UNODC 2025
Kutokuwepo kwa utulivu duniani kunachochea ongezeko kubwa la matumizi ya mihadarati au dawa za kulevya na kuimarika kwa makundi ya uhalifu wa kupangwa, limeonya Shirika la Umoja wa Mataifa la Kupambana na Dawa za Kulevya na Uhalifu UNODC kupitia Ripoti ya Dunia ya Dawa za Kulevya 2025 iliyozinduliwa leo mjini Vienna Austria.
Ripoti hiyo inaeleza hali ya wasiwasi kuhusu jinsi migogoro, misukosuko ya kiuchumi, na udhaifu wa utawala vinavyochangia mgogoro unaotishia afya, usalama na maendeleo duniani kote.
“Takwimu zinaonesha wazi, makundi ya usafirishaji haramu wa dawa za kulevya yanabadilika kwa kasi, yanatumia fursa za migogoro ya kimataifa na kuwalenga watu walio hatarini,” amesema Mkurugenzi Mtendaji wa UNODC, Ghada Waly.
Ameongeza kuwa “Tunahitaji hatua za pamoja kupitia kinga, haki, ushirikiano wa mipakani, na uwekezaji katika jamii ili kuvunja mitandao hii na kulinda jamii zetu.”
Watu milioni 316 walitumia dawa za kulevya 2023
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, watu milioni 316 walitumia dawa za kulevya mwaka 2023 sawa na asilimia 6 ya watu wote duniani wenye umri wa kati ya miaka 15 hadi 64 ikilinganishwa na asilimia 5.2 mwaka 2013.
Bangi imetajwa katika ripoti hiyo kuwa inaongoza kwa watumiaji milioni 244, ikifuatiwa na opioidi watu milioni 61, amfetamini watu milioni 30.7, cocaine watu milioni 25, na ecstasy watu milioni 21.
Ripoti inatahadharisha kuwa ongezeko la watu waliofurushwa makwao na hali ya sintofahamu kisiasa vinaweza kuendelea kuongeza idadi hii.
Biashara ya Cocaine inashamiri
Kwa mujibu wa ripoti moja ya mienendo ya kutia hofu ni ukuaji wa kasi wa biashara ya mihadarati aina ya cocaine, ambayo sasa ndiyo inakua kwa kasi zaidi duniani. Uzalishaji wacocaine uliongezeka kwa asilimia 34 mwaka 2023 na kufikia tani 3,708 ikiwa ni rekodi ya juu kabisa wakati mzigo uliokamatwa ulifikia tani 2,275 imesema ripoti hiyo.
Pia imeongeza kuwa wauzaji haramu wanaenea hadi masoko mapya barani Asia na Afrika, huku ushindani wenye ghasia ukienea barani Ulaya, hasa kutokana na vikundi vya uhalifu kutoka mataifa ya Balkani Magharibi.
Soko la dawa bandia linakua kwa kasi
Wakati huo huo, ripoti imeonya kuwa soko la dawa bandia hasa aina za amfetamini kama methamphetamine na Captagon linazidi kukua kutokana na gharama ndogo za uzalishaji na hatari ndogo ya kugundulika.
Licha ya machafuko ya kisiasa nchini Syria, captagon inaendelea kusambazwa kuelekea Rasi ya Arabia, huenda ikitokea kwenye maghala ya zamani au viwanda vipya vya siri imesema ripoti.
Imeongeza kuwa pia afyunyi bandia kama fentanyl pia zinaendelea kuwa tishio kubwa kwa afya ya umma na usalama.
Uchumi utokanao na dawa za kulevya ni mkubwa
Ripoti hiyo ya UNODC imebainisha kuwa Kiwango cha kiuchumi cha biashara ya dawa za kulevya ni kikubwa mno, kikizalisha mamia ya mabilioni ya dola kila mwaka. Imesema magenge ya dawa za kulevya yanatumia teknolojia katika uzalishaji, usafirishaji, na mawasiliano, hali inayowalazimu watekelezaji wa sheria kutumia zana za kisasa zaidi na ujasusi wa hali ya juu.
Ripoti inapendekeza kwamba kuchora ramani za mitandao ya kihalifu na kuwalenga wahusika wakuu kunaweza kuvuruga vibaya shughuli zao.
Athari za kiafya na kimazingira za mihadarati
Ripoti imesea zaidi ya usafirishaji haramu, athari za kiafya na kimazingira za matumizi ya dawa za kulevya ni kubwa sana.
Imeendela kusema kuwa Vifo karibu nusu milioni vinavyohusiana na dawa za kulevya na miaka milioni 28 ya maisha enye afya (DALYs) vilirekodiwa mwaka 2021. Hata hivyo, ni mtu 1 tu kati ya 12 wenye matatizo ya uraibu aliyepata matibabu mwaka 2023 imesema ripoti.
Ripoti pia inatoa tahadhari kuhusu uharibifu wa mazingira kutokana na kilimo cha mimea ya dawa za kulevya na taka za maabara, hasa barani Ulaya, ambako gharama za usafi zinaongezeka. Licha ya hayo, athari za mazingira bado hazijapewa uzito katika sera nyingi za sasa.