Mafanikio ya Mradi wa ACP MEAs 3 nchini Rwanda katika kuboresha kilimo endelevu na usimamizi wa viuatilifu
Mafanikio ya Mradi wa ACP MEAs 3 nchini Rwanda katika kuboresha kilimo endelevu na usimamizi wa viuatilifu
Shirika la Umoja wa Mataifa la chakula na kilimo FAO, kwa kushirikiana na Serikali ya Rwanda, linaendelea kujenga uwezo wa kitaifa katika kuhimiza matumizi ya mbinu rafiki kwa mazingira katika kilimo pamoja na usimamizi salama wa viuatilifu. Hili linafanyika kupitia utekelezaji wa awamu ya tatu ya mradi wa ACP MEAs 3 unaofadhiliwa na Muungano wa Ulaya EU. Mpango huu unalenga kuwawezesha wakulima wadogo kuhamia kwenye mifumo ya kilimo endelevu kimazingira na kuwajengea uwezo wa utekelezaji wa mikataba ya kimataifa ya mazingira.
Mpango huu unalenga kuwawezesha wakulima wadogo kuhamia kwenye mifumo ya kilimo endelevu kimazingira na kuwajengea uwezo wa utekelezaji wa mikataba ya kimataifa ya mazingira.
Video iliyoandaliwa na FAO inaanza kwa kuonesha mandhari ya kuvutia ya jiji moja nchini Rwanda, ikifuatwa na taswira ya mashamba ya kijijini. Kamera inasogea karibu, wakulima wakiwa shambani baadhi wakihudhuria mafunzo kuhusu mbinu bora za kilimo.
Kwa miaka mitatu iliyopita, wakulima wengi nchini Rwanda wamefaidika kupitia ushiriki wao katika mashamba darasa.
Kamari Jean Bosco, mmoja wa wanachama wa FFS anasema, "Nilianza kutumia mbinu bora za kilimo kama vile kuweka matandazo kwenye shamba la migomba, na nilipata mavuno mazuri. Pia nilifanya mbinu za kurutubisha udongo kwenye shamba la nyanya, na hili ongezeko la uzalishaji na kupungua kwa wadudu na magonjwa.”
Wakulima wengine kama Zainab Yukusenge wameona mafanikio makubwa. Kupitia elimu waliyoipata kupitia FAO, sasa wanaweza kutumia mbolea ya asili inayotokana na mifugo. Hili limewawezesha kuboresha rutuba ya udongo na kuongeza uzalishaji wa mazao.
Mradi wa ACP MEAs 3 pia una lengo mahususi la kuboresha usimamizi wa viuatilifu ili kupunguza athari zake kwa afya ya binadamu na mazingira. Ivy Saunyama, afisa wa kilimo wa FAO anasema, “Mradi huu umeisaidia Serikali ya Rwanda kufuata hatua tatu muhimu zilizokubalika kimataifa za kupunguza hatari za viuatilifu hatari. Hii ni pamoja na kutambua viuatilifu hatari sana, kufanya tathmini ya mahitaji na hatari zake, na kutambua njia mbadala kwa viuatilifu hivyo. Tunaendelea kushirikiana na serikali kuandaa mpango wa kupunguza matumizi ya viuatilifu hivyo kwa njia za kisheria na zisizo za kisheria.”
Naye Nyirabasirimu Anita, Mkulima na mwanachama wa FFS, anasema “Sababu kubwa ya kutotumia viuatilifu vya kemikali ni kwa sababu tuliona upotevu wa bayonuai. Udongo wetu ulianza kupoteza rutuba kutokana na matumizi ya viingilio vya kilimo vya kemikali. FAO walikuja kutufundisha jinsi ya kutengeneza viuatilifu vya asili, na sasa tunavitumia pamoja na mbolea asili mashambani mwetu. Tumeshuhudia kurudi kwa viumbe hai wa udongoni.”
Thomas Ameny, mtaalamu wa kimataifa wa FFS anatamatisha kwa kusema kuwa faida kubwa ya wakulima kufanya kazi kwa pamoja ni kwamba wanaposhirikiana, wanabadilishana maarifa na uzoefu, wanagundua suluhisho za kiasili kwa changamoto zao za ndani kama timu, kisha wanazitumia mashambani mwao kwa mafanikio makubwa.