Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tuepushe kauli za chuki kwenye ujumbe chanya - Guterres

Watoto wa shule ya Kihindi wakionyesha sanaa yao huko Bharat Mandapam, New Delhi, ili kutoa heshima kwa Mauaji ya Kimbari dhidi ya Watutsi ya mwaka 1994 nchini Rwanda.
© UN India/Blassy Boben Watoto wa shule kutoka India wakionesha sanaa yao huko Bharat Mandapam, New Delhi, kwa ajili ya kumbukumbu ya Mauaji ya Kimbari ya 1994 dhidi ya Watutsi nchini Rwanda, wakati zaidi ya watu milioni moja waliuawa kimfumo kufuatia miaka ya habari potofu na matamshi ya chuki yaliyosabaisha mivutano ya kikabila.

Tuepushe kauli za chuki kwenye ujumbe chanya - Guterres

Sheria na Kuzuia Uhalifu

Leo Juni 18 ni siku ya kimataifa ya kupambana na kauli za chuki ambapo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ametumia ujumbe wake kwa siku hii kutoa onyo kuhusu hatari zinazoongezeka za chuki mtandaoni, hasa zikichochewa na akili mnemba au (AI) na  na majukwaa ya kidijitali.

“Kauli za chuki ni sumu kali katika  jamii,” amesema Guterres na kuongeza kuwa “imetengeneza njia ya kuelekea katika ghasia na ukatili katika vipindi vya giza zaidi vya historia ya binadamu.”

Amesisitiza kuwa madhehebu madogo ya kidini pamoja na jamii za watu wa makabila madogo n mara nyingi ndio huathirika zaidi vibaya, wakikumbwa na ubaguzi, kutengwa, na madhara ya moja kwa moja.

Kaulimbiu ya mwaka huu inaangazia kasi na uwiano usio wa kawaida wa kuenea kwa kauli za chuki katika zama za kidijitali na ndipo Guterres anaelezea jinsi kanuni za upendeleo kwenye majukwaa ya mtandaoni yanavyozidi kutumika kusambaza maudhui hatarishi na kufungua njia mpya za udhalilishaji na unyanyasaji.

Mkataba wa Kimataifa wa Kidijitali

Ili kukabiliana na vitisho hivi vinavyozidi kuongezeka, Katibu Mkuu amesisitiza umuhimu wa Mkataba wa Kimataifa wa Kidijitali uliopitishwa mwaka 2024 wakati wa Mkutano wa Zama Zijazo.

Waandamanaji wanabeba mabango kwenye maandamano, na moja ya mabango hayo yanasema "HATRED IS VIRUS" kwa herufi za bluu na nyekundu.
© Unsplash/Jason Leung Watu wanashiriki katika maandamano ya kupinga ubaguzi wa rangi.

Mkataba huu unatoa wito wa ushirikiano wa kimataifa ulio imara kupambana na chuki mtandaoni, kwa msingi wa haki za binadamu na sheria za kimataifa.

“Tunahitaji ushirikiano katika kila ngazi,” amesema Guterres, akizihimiza serikali, asasi za kiraia, sekta binafsi, pamoja na viongozi wa kidini na kijamii kushirikiana.

“Lazima tupinge simulizi zenye sumu kwa ujumbe chanya, na kuwawezesha watu kutambua, kukataa, na kusimama dhidi ya hotuba za chuki.”

Harakati za UN kukabili kauli za chuki

Guterres pia amesisitiza jukumu la Mkakati na Mpango wa Umoja wa Mataifa wa Kupambana na Kauli za Chuki, kama muongozo katika juhudi hizi.

Ametaja pia Kanuni za Kimataifa za Uadilifu wa Habari alizozindua mwaka jana, kama nyenzo muhimu ya kukuza mazingira ya habari yenye kuaminika na ya kibinadamu zaidi.

Akiwaalika watu duniani kutumia teknolojia kwa manufaa, kiongozi huyo wa UN amehitimisha kwa kusema: “Tujitolee kutumia Akili Mnemba si kama chombo cha chuki, bali kama nguvu ya mema. Tushikamane katika kutafuta amani, heshima ya pamoja, na kuelewana kwa wote.”

Siku ya kimataifa ya kupinga kauli za chuki ilipitishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa tarehe 21 mwezi Julai mwaka 2021 na azimio namba A/RES/75/309.

Naye Nenna Ndukwe Kiongozi wa Umoja wa Mataifa wa Masuala ya Afya ya Akili na Ustawi Mahali pa Kazi akizungumzia mapambano dhidi ya kauli za hchuki mahali pa kazi amesema, "Athari za kisaikolojia zinaweza kuwa kubwa sana na kuathiri uwezo wa mtu kufanya kazi au kutekeleza majukumu yake ya kila siku. Hivyo basi, ni muhimu sana sisi sote kusimama kidete dhidi ya suala hili. Tunapaswa kutambua kuwa kila mmoja wetu ana jukumu na wajibu wa kuhakikisha mazingira salama ya kufanyia kazi, lakini pia mazingira salama ya nyumbani."

Nenna Ndukwe ameongeza kuwa kulifungia mdoto kuhusu suala hili hakutosaidia chochote akisema, "Hivyo basi, hakuna mmoja wetu anayepaswa kukaa kimya juu ya suala hili, bali tunapaswa kutambua kuwa kila mmoja ana jukumu. Ni wajibu wetu kuhakikisha kuwa matukio ya kauli za chuki yanapungua kadiri iwezekanavyo."