Shambulio la usiku wa jana ni la mauaji zaidi Kyiv nchini Ukraine katika kipindi cha mwaka mmoja: UN
Shambulio la usiku wa jana ni la mauaji zaidi Kyiv nchini Ukraine katika kipindi cha mwaka mmoja: UN
Mashambulizi ya ndege zisizo na rubani (drones) na makombora yaliyofanywa na jeshi la Urusi dhidi ya mji mkuu wa Ukraine, Kyiv, usiku wa kuamkia leo yameelezewa na Umoja wa Mataifa kama “mashambulio ya vifo zaidi kuwahi kutokea katika jiji hilo katika kipindi cha karibu mwaka mmoja.”
Kwa mujibu wa mamlaka za ndani ya Ukraine”Takriban raia 14 wameuawa na wengine 114 kujeruhiwa katika mashambulizi hayo yaliyofanyika usiku wa kuamkia Jumanne. Timu ya Ufuatiliaji wa Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa nchini Ukraine OHCHR, inaendelea kuthibitisha idadi ya wahanga na kiwango cha uharibifu”.
Danielle Bell, Mkuu wa Ujumbe wa wa haki za binadamu OHCHR nchini Ukraine amesema .“Katika mashambulizi ya usiku wa jana, mji wa Kyiv ndio ulioathirika zaidi.”
Ameongeza kuwa mashambulizi hayo yanadhihirisha “tishio kubwa linalosababishwa na mkakati wa kutumia makombora na idadi kubwa ya Ndege zisizo na rubani kwa wakati mmoja katika maeneo yenye watu wengi,” jambo linalosababisha vifo vya raia na mateso makubwa.
Mashambulizi yaliyoongezeka usiku
Mara ya mwisho Kyiv kushuhudia vifo vya kiwango kama hicho ilikuwa tarehe 8 Julai 2024, ambapo raia 32 waliuawa na 85 kujeruhiwa, katika shambulio lililoathiri pia Hospitali ya Watoto ya Okhmadyt.
Mbali na Kyiv, mashambulizi hayo yamesababisha kifo cha raia mmoja na majeruhi 19 katika miji ya Odessa, mkoa wa Chernihiv na maeneo ya mji mkuu mkubwa wa Kyiv, kutokana na matumizi ya silaha za masafa marefu.
Katika mashambulizi ya hivi karibuni, Jeshi la Urusi limeongeza mashambulizi ya usiku kwa kutumia drones na makombora, yakilenga miji kwa wingi. Usiku wa Jumatatu, mamlaka za Ukraine zimeripoti kuwa drones 440 na makombora 32 yalirushwa kuelekea Ukraine, ambapo Ndege zisizo na rubani 175 na makombora 14 yalielekezwa Kyiv pekee. Mashambulizi hayo yalilenga maeneo 30 katika wilaya saba za jiji hilo.
Takwimu zinazoongeza hofu
Kwa siku 17 za kwanza za mwezi Juni pekee, OHCHR imesema mamlaka zimeripoti kuwa Ndege zisizo na rubani 3,340 na makombora 135 yamerushwa Ukraine nzima ikiwa ni mara ya nne mwezi huu ambapo zaidi ya mizinga 400 imerushwa usiku mmoja.
Ukilinganisha na mwaka uliopita katika mwezi mzima wa Juni 2024, makombora 544 pekee ndiyo yalirushwa hivyo idadi imeongezeka sana zaidi ya mara tano.
Kabla ya shambulio la jana Jumatatu, timu za Umoja wa Mataifa tayari zilikuwa zimethibitisha kuwa raia 29 walikuwa wameuawa na 126 kujeruhiwa kutokana na makombora ya masafa marefu au vipande vya silaha vilivyoanguka wakati wa kuzuiwa.
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, mashambulizi ya ndege zisizo na rubani na makombora ya masafa marefu yamesababisha vifo vingi vya raia mwaka huu, huku ripoti ikionesha kuwa idadi ya vifo na majeruhi imeongezeka kwa asilimia 50 katika miezi mitano ya kwanza ya 2025 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka 2024.
Wakazi wa Ukraine wakimbilia mafichoni kila siku usiku
Mratibu wa Misaada ya Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa nchini Ukraine, Matthias Schmale, amelaani mashambulizi ya hivi karibuni ya Urusi kwa raia katika mji wa Kyiv, Odessa na miji mingine.
“Watu wa Ukraine hawapaswi kulazimika kukimbilia mafichoni kila usiku,” amesema, akikumbuka “usiku mwingine wa hofu ulioigubika jamii hiyo”.
Schmale amesisitiza kuwa “mashambulizi dhidi ya raia na miundombinu ya kiraia yanakatazwa na sheria ya kimataifa ya kibinadamu” na kuongeza kuwa:“Raia, wakiwemo watoto, hawapaswi kulengwa kamwe. Hatupaswi kuzoea vita.”
Misaada ya haraka yaendelea kutolewa
Mashirika ya ndani ya Ukraine, yakishirikiana na Umoja wa Mataifa na wadau wa kibinadamu, yanaendelea kutoa misaada ya haraka, ikiwa ni pamoja na huduma za matibabu ya dharura, vifaa vya hifadhi ya muda, na msaada wa kisaikolojia.
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa kipaumbele kingine ni msaada wa chakula, kilimo, na fedha taslimu.Katika mkoa wa Zaporizhzhia pekee, mashirika 145 ya misaada yamewafikia watu 285,000 tangu mwanzo wa mwaka, yakiwa yanalenga kusaidia mifumo ya usambazaji maji na usafishaji maji machafu,mikoa iliyoathirika tangu uharibifu wa bwawa la Kakhovka Juni 2023.