Mashariki mwa DRC, UNDP yaomba msaada kusaidia wakimbizi wa ndani kujikwamua
Mashariki mwa DRC, UNDP yaomba msaada kusaidia wakimbizi wa ndani kujikwamua
Huko jimboni Kivu Kaskazini, Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, juhudi za kidiplomasia zinaendelea kumaliza mapigano, huko nalo shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo, UNDP likitoa wito wa msaada kwa watu waliofurushwa makwao kutokana na mashambulizi ya waasi wa M23, msaada ambao utawasaidia kujenga upya maisha yao na njia zao za kujipatia riziki.
Ni Damien Mama Mwakilishi mkazi wa UNDP nchini DRC ambaye akiwa Sake, jimboni Kivu Kaskazini amezungumza kwa njia ya video na waandishi wa Habari wa Umoja wa mataifa walioko Geneva, nchini Uswisi, kuelezea hali halisi inayoendelea hivi sasa.
“Uchumi umeathirika vibaya. Benki zimefungwa, biashara zimeharibiwa, na zilizobaki zinafanya kazi kwa chini ya asilimia 30 ya uwezo wao, jambo ambalo ni pigo kubwa kwa maendeleo ya eneo hili. Kwa hiyo, kuhusu mpango wetu hapa Kivu Kaskazini, UNDP inakusudia katika kipindi cha miezi 5 ijayo kusaidia uundwaji wa ajira 1,000, pamoja na kurejesha miundombinu ya msingi ambayo itanufaisha takriban watu 15,000.”
Wakati huo huo, UNDP imejikita pia kusaidia wanawake na wasichana waliokumbwa na ukatili wa kijinsia, suala lililotajwa na shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto, UNICEF mwezi uliopita kuwa wakati wa kilele cha vita, mtoto mmoja alibakwa kila baada ya nusu saa.
Ili kutekeleza mpango huu, shirika hili la Umoja wa Mataifa linahitaji dola milioni 25.
“Mpango wetu umekadiriwa kugharimu dola milioni 25. Hadi sasa tumefanikiwa kupata dola milioni 14 kutoka Korea Kusini, Canada, Uingereza na Sweden. Wito wetu ni kwa nchi na wafadhili wengine kusaidia kutufadhili ili kufidia pengo lililobaki la dola milioni 11.”