Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkutano wa UN kuhusu bahari wafungwa Nice kwa ahadi lukuki

Muonekano wa chini ya maji wa kundi kubwa la samaki na mnandi kadhaa wanaoogelea juu ya mwamba wenye miamba.
© Taryn Schulz Ukiendeshwa na Ufaransa na Costa Rica, Mkutano wa UNOC3 Uliwaleta pamoja zaidi ya washiriki 15,000 Nice Ufaransa

Mkutano wa UN kuhusu bahari wafungwa Nice kwa ahadi lukuki

Tabianchi na mazingira

Meli zilizoko bandari ya Nice zimepiga miluzi ya ukungu siku ya Ijumaa, kama sauti ya kilele cha nadra cha mshikamano wa kimataifa wakati Mkutano wa Tatu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Bahari UNOC3 ulipofungwa rasmi. 

Dakika chache kabla, zaidi ya nchi 170 zilipitisha kwa kauli moja tamko la kisiasa linalotoa ahadi ya kuchukua hatua za haraka kulinda bahari.
 
“Tunafunga wiki hii ya kihistoria si kwa matumaini tu, bali kwa ahadi thabiti, mwelekeo ulio wazi, na msukumo usio na shaka,” amesema Li Junhua, Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayesimamia Masuala ya Kiuchumi na Kijamii na Katibu Mkuu wa mkutano huo.
Mkutano huo wa siku tano, ulioandaliwa kwa pamoja na serikali za Ufaransa na Costa Rica, uliwaleta pamoja washiriki 15,000 wakiwemo zaidi ya viongozi wakuu wa nchi na serikali 60 kwenye pwani ya Mediterania ya Ufaransa.
 
Ukiwa na zaidi ya matukio 450 ya kandoni na wageni karibu 100,000, mkutano huo, uliopewa jina la UNOC3, ulijenga juu ya kasi ya mikutano iliyotangulia wa New York (2017) na Lisbon (2022). Mkutano huo umefikia kilele kwa wito wa pamoja wa kupanua ulinzi wa bahari, kupunguza uchafuzi, kudhibiti maji ya kimataifa, na kufungua ufadhili kwa mataifa wa pwani na visiwa vilivyo hatarini.
Li Junhua, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia Masuala ya Uchumi na Jamii na Katibu Mkuu wa UNOC3, akizungumza katika mkutano wa mwisho na waandishi wa habari mjini Nice.
UN DESA Li Junhua Msaidizi wa Katibu MKuu wa Masuala ya Kiuchumi na Kijamii na Katibu Mkuu wa Mkutano wa UNOC3 akizungumza wakati wa kufungwa kwa mkutano

Ahadi za kijasiri

Matokeo ya mkutano, yanayojulikana kama Mpango wa Hatua wa Bahari wa Nice, ni mfumo wa sehemu mbili unaojumuisha tamko la kisiasa na zaidi ya ahadi 800 za hiari kutoka kwa serikali, wanasayansi, mashirika ya Umoja wa Mataifa, na jamii za kiraia tangu mkutano uliopita.
 
“Ahadi hizi zinahusisha kuhamasisha vijana, kukuza uelewa wa mifumo ya bahari ya kina, kujenga uwezo katika sayansi na uvumbuzi, na ahadi za kuridhia mikataba ya kimataifa,” amesema Bwana. Li.
Baadhi ya ahadi zilizotangazwa wiki hii zinaonesha ukubwa wa mgogoro wa bahari:
 
  • Tume ya Ulaya imetangaza uwekezaji wa euro bilioni 1 kusaidia uhifadhi wa bahari, sayansi, na uvuvi endelevu.
  • Polynesia ya Kifaransa imeahidi kuanzisha eneo kubwa zaidi la bahari linalolindwa duniani, likijumuisha ukanda wake mzima wa kiuchumi wa kipekee takriban kilomita za mraba milioni tano.
  • Ujerumani imezindua mpango wa euro milioni 100 wa kuondoa mabomu ya zamani kutoka Bahari ya Baltic na Bahari ya Kaskazini.
  • New Zealand imeahidi dola milioni 52 kuimarisha usimamizi wa bahari katika Pasifiki.
  • Hispania imetangaza maeneo mapya matano ya bahari yaliyohifadhiwa.
Ushirikiano wa nchi 37 unaoongozwa na Panama na Canada umezindua Muungano wa Azimio Kuu kwa Bahari Tulivu, kushughulikia uchafuzi wa kelele chini ya maji. Wakati huohuo, Indonesia na Benki ya Dunia wametambulisha ‘Bondi ya Matumbawe” kusaidia uhifadhi wa matumbawe.
 
“Wimbi la mabadiliko limeanza,” amesema Bw. Li. “Sasa ni jukumu letu sote kulisukuma mbele kwa ajili ya watu wetu, sayari yetu, na vizazi vijavyo.”
Washiriki katika Mkutano wa Bahari UN (UNOC3) wakifunga mkutano na waandishi wa habari huko Nice, Ufaransa.
UN DESA Olivier Poivre d’Arvor (kulia ) mjumbe wa Ufanransa kwenye mkutano wa UNOC3 akizungumza wakati wa kufunga mkutano

Jukwaa la kidiplomasia

Mkutano ulifunguliwa Jumatatu kwa onyo kali. “Hatuitendei bahari kama ilivyo urithi wa pamoja wa dunia,” alisema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres, akiwa pamoja na marais wa Ufaransa na Costa Rica, Emmanuel Macron na Rodrigo Chaves Robles, waliotoa wito wa kuimarisha ushirikiano wa kimataifa unaotegemea sayansi.
 
Ijumaa, mjumbe maalum wa Ufaransa kwenye mkutano huo, Olivier Poivre d’Arvor, amekumbusha hatari zilizoko: “Tulitaka huko Nice kubahatisha mabadiliko ya kweli. Nadhani tumesonga mbele, lakini hatuwezi kurudi nyuma tena.”
 
Mojawapo ya malengo makuu ya mkutano lilikuwa kuharakisha utekelezaji wa Mkataba wa Bahari ya Juu (BBNJ) uliopitishwa mwaka 2023, unaolenga kulinda uhai wa baharini katika maji ya kimataifa. Mataifa 60 yanahitajika kuridhia ili kuufanya uanze kutumika.
 
Wiki hii pekee, nchi 19 zimeridhia, na kufikia jumla ya 50 hadi Ijumaa. “Hii ni ushindi mkubwa,” amesema Bwana. Poivre d’Arvor. “Ni vigumu sana kufanya kazi kuhusu bahari kwa sasa wakati Marekani haijajihusisha kikamilifu.” Akimaanisha kutokuwepo kwa ujumbe wa ngazi ya juu kutoka Marekani, na pia agizo la rais wa zamani Donald Trump kuendeleza uchimbaji wa madini ya kina cha bahari. “Kilindi si cha kuuza,” amesema, akinukuu kauli ya awali ya Rais Macron.
 
Hata hivyo, Bwana. Poivre d’Arvor amesisitiza makubaliano makubwa yaliyofikiwa. “Huenda nchi moja imekosekana,” amesema. “Lakini asilimia 92 ya wamiliki wenza’walikuwepo Nice.”
 
Waziri wa Mambo ya Nje wa Costa Rica, Arnoldo André-Tinoco, amehimiza mataifa kuongeza kasi ya ufadhili kwa ulinzi wa bahari. “Kila ahadi lazima iwajibike,” amesema wakati wa kufunga mkutano.
Peter Thomson, Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu wa UN kuhusu Bahari, akizungumza na Habari za UN kwenye ukingo wa bahari katika Mkutano wa Bahari UN .
UN Video/Brianna Rowe Peter Thomson, mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu kuhusu masuala ya bahari akizungumza na UN News

Msukumo na mtihani

Kwa Peter Thomson, Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Bahari, Nice ilikuwa hatua ya mabadiliko. “Siyo tu kile kinachotokea katika mkutano, ni kile kinachofuata baada yake,” ameiambia UN News, akikumbuka nyakati za mwanzo za utetezi wa bahari wakati Malengo ya Maendeleo Endelevu ya SDG 14 yalipoanzishwa.
 
“Toka jangwa tulilokuwa 201 hadi tulipo sasa, ambapo unaona ushiriki wa ajabu.”
Mkutano wa Nne wa Bahari wa Umoja wa Mataifa unatarajiwa mwaka 2028, ukiandaliwa kwa pamoja na Chile na Korea Kusini. Bwana. Thomson ametabiri ongezeko la kasi kutoka sasa. Ameelezea matumaini kwamba makubaliano muhimu ya kimataifa kama mkataba wa BBNJ, Mkataba wa WTO kuhusu ruzuku za uvuvi, na mkataba wa kimataifa wa plastiki yatakuwa yameridhiwa na kutekelezwa kufikia wakati huo.
 
Mkutano huo pia utakuwa ukikabili ukomo wa SDG 14 unaotarajiwa 2030. “Tutafanya nini SDG 14 itakapotimia 2030?” amehoji. “Lazima tupanue malengo. Lazima tuwe na nguvu zaidi.” Amesisitiza kuwa ingawa lengo lilikuwa kulinda asilimia 10 ya bahari kufikia 2020 ambalo halikutimizwa lengo jipya ni asilimia 30 kufikia 2030.
 
Akiwa amevaa mkufu wa gamba uliotolewa na Visiwa vya Marshall, Mzaliwa wa Fiji ameyasifu mataifa ya visiwa vidogo kwa kuweka viwango vya juu vya ulinzi wa bahari. “Kama mataifa madogo yanaweza kuchukua hatua kubwa kama hizi, kwa nini mataifa makubwa yasiige mfano?”
Amewasifu pia wanasayansi 2,000 waliokutana kwa ajili ya Kongamano la Sayansi ya Bahari kabla ya mkutano. “Huu ni mfano bora wa kuendesha mambo,” amesema.
Wavuvi watatu huko Grenada wakiwa na boti zao majini.
PROCARIBE+ project Wavuvi wakiwa baharini Grenada

Ishara ya umoja

Licha ya hali ya sherehe, mvutano bado ulikuwepo. Mataifa ya Visiwa Vidogo yalitaka lugha kali zaidi kuhusu hasara na uharibifu madhara ya mabadiliko ya tabianchi yanayozidi uwezo wa kuhimili. “Huwezi kuwa na tamko la bahari bila SIDS,” ameonya mjumbe mmoja.
 
Wengine, akiwemo Rais Chaves wa Costa Rica, walitaka marufuku ya muda kuhusu uchimbaji wa madini ya kina cha bahari hadi sayansi ithibitishe hatari hatua ambayo haikuingizwa kwenye tamko la mwisho.
 
Hata hivyo, tamko la kisiasa lililopitishwa Nice, lenye kichwa Bahari yetu, mustakabali wetu: tumeungana kwa hatua ya haraka, linathibitisha tena lengo la kulinda asilimia 30 ya bahari na ardhi kufikia 2030, sambamba na kuunga mkono mikataba ya kimataifa kama Mkataba wa Kunming-Montreal wa Baiolojia, na malengo ya kimazingira ya Shirika la Umojoja wa Mataifa la masuala ya Bahari IMO.
 
“Mtihani wa kweli,” amesema Bwana. Li, “si kile tulichosema hapa Nice bali kile tutakachofanya baada ya hapa.”
 
Wakati jua lilipokuwa likitua nyuma ya Promenade des Anglais na kikao cha mwisho cha mkutano kikihitimishwa, bahari ya kale, muhimu, na katika hatari ilishuhudia kimya kimya ahadi dhaifu lakini za pamoja.