Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mashambulizi ya Israeli dhidi ya Iran, Katibu Mkuu wa UN alaani

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António  Guterres akizungumza na waandishi wa habari (Picha Maktaba)
UN Photo/Mark Garten
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akizungumza na waandishi wa habari (Picha Maktaba)

Mashambulizi ya Israeli dhidi ya Iran, Katibu Mkuu wa UN alaani

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, amelaani mashambulizi ya kijeshi yaliyofanywa na Israel dhidi ya vituo vya nyuklia vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, akionya juu ya hatari ya kuongezeka kwa mvutano katika eneo la Mashariki ya Kati.

Katika taarifa iliyotolewa na Naibu Msemaji wa Katibu Mkuu, Farhan Haq, usku wa kuamkia leo Ijumaa Juni 13 kwa saa za New York, Marekani, Katibu Mkuu ameeleza wasiwasi mkubwa kuhusu wakati uliotekelezwa mashambulizi hayo, hasa ikizingatiwa kuwa mazungumzo kati ya Iran na Marekani kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran yanaendelea.
 
“Katibu Mkuu analaani hatua yoyote ya kijeshi katika eneo la Mashariki ya Kati,” imesomeka taarifa hiyo. “Ana wasiwasi juu ya mashambulizi ya Israeli dhidi ya vituo vya nyuklia vya Iran wakati mazungumzo kati ya Iran na Marekani kuhusu hali ya mpango wa nyuklia wa Iran yakiendelea.”
 
Guterres amesisitiza umuhimu wa mataifa wanachama wa Umoja wa Mataifa kuheshimu Katiba ya Umoja wa Mataifa na sheria za kimataifa.
 
Akiwataka pande zote mbili kuwa na kiasi na kujizuia, Katibu Mkuu ameonya dhidi ya hatari ya mzozo mkubwa zaidi. “Ni lazima kuepuka kuingia kwenye mgogoro mkubwa zaidi  hali ambayo eneo hili haliwezi kuimudu,” taarifa hiyo imeongeza.
 
Taarifa hiyo inaakisi hofu inayoongezeka kimataifa kuhusu kuongezeka kwa uhasama na athari zake kwa usalama wa kikanda na wa kimataifa. Umoja wa Mataifa unaendelea kufuatilia kwa karibu hali hii na uko tayari kuunga mkono juhudi za kidiplomasia katika kutafuta suluhu ya amani.