Azimio lapitishwa Baraza Kuu kuhusu Gaza
Azimio lapitishwa Baraza Kuu kuhusu Gaza
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa leo Juni 12 limepitisha azimio linalotaka kusitishwa mara moja kwa mapigano huko Gaza eneo la Palestina linalokaliwa kimabavu na Israeli. Katika azimio hilo, nchi 149 zilipiga kura kuunga mkono, ilhali 12 zilipinga na nyingine 19 hazikupiga kura kabisa kwa azimio hilo linalotaka pia sitisho la mapigano liwe la kudumu na kusiweko na masharti yoyote.
Likipatiwa jina "Ulinzi wa raia na kuheshimu wajibu wa kisheria na kibinadamu," azimio linazitaka pande zote kuheshimu sheria za kimataifa, linatoa wito wa kuachiliwa kwa mateka, na linataka misaada ya kibinadamu ifikishwe Gaza bila kizuizi chochote.
Palestina yasema 'hali haramu' Gaza ikome
Kabla ya kupiga kura, Balozi Riyad Mansour, ambaye ni Mwakilishi wa Kudumu wa Palestina kwenye Umoja wa Mataifa, amesema “hali hii haramu, isiyo ya kimaadili haiwezi kuendelea. Lazima ikome, na ikome mara moja.”
Ameongeza kuwa “tunawashukuru wote waliopo mstari wa mbele kukomesha janga hili la kutisha, serikali na watu kutoka kila pembe ya dunia wanaosimama kwa ajili ya ubinadamu na kwa ajili ya kutetea taifa zima la Palestina.”
Israeli yalalama kutokuweko kwa sharti kuhusu mateka
Mwakilishi wa Kudumu wa Israeli kwenye Umoja wa Mataifa, Balozi Danny Danon naye alizungumza kabla ya kura akisema, “ni lazima tukubali kwamba kwa kushindwa kuweka sharti la kuachiliwa kwa mateka kama sehemu ya makubaliano ya kusitisha mapigano, mmepeleka ujumbe kwa kila kundi la kigaidi kuwa utekaji nyara wa raia ni njia inayofanya kazi. Hii si diplomasia. Huu ni usaliti.”
Urusi yasema la msingi ni kusitisha mauaji Gaza
Balozi Vasily Nebenzya ambaye ni Mwakilishi wa Kudumu wa Urusi kwenye Umoja wa Mataifa, amesema “leo, jumuiya ya kimataifa ina fursa nyingine ya kutuma ujumbe sahihi kwa pande zinazohusika na mzozo,. Lengo lake ni la kibinadamu tu, na linaangazia jambo la muhimu zaidi, kusitisha mauaji ya binadamu huko Gaza.”
Marekani yageukia wanachama wasiolaani Hamas
Marekani ambayo ni moja ya nchi 12 zilizopinga azimio hilo, ililikosoa kwa madai ya kushidwa kulaani moja kwa moja wanamgambo wa kipalestina wa Hamas.
Kaimu Mwakilishi wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Dorothy Shea amesema, “msaada wa upofu kwa Hamas kutoka kwa wanachama wa chombo hiki unadhoofisha juhudi za kweli za kidiplomasia za kuwaachilia mateka. Hatuungi mkono hatua zisizo na usawa zinazoshindwa kulaani Hamas.”
Kwa nini ni mkutano wa 10 wa dharura wa UNGA?
Huu ni mkutano wa 10 wa dharura unafanywa na Baraza Kuu kujadili ukaliaji wa Israeli huko Palestina kinyume cha sheria. Mkutano wa kwanza uliitishwa mwaka mwaka 1997 na aliyekuwa Rais wa Baraza Kuu la UN wakati huo Razali Ismaili wa Malaysia.
Mikutano ya dharura huitishwa pindi Baraza la Usalama linaposhindwa kupitisha uamuzi wa suala husika katika vikao mbali mbali.
Mkutano huu wa 10 ulianza Oktoba 26 mwaka 2023 baada ya Hamas kushambulia Israeli na Israeli kujibu mashambulizi na vita vinaendelea hadi leo. Vikao vya mkutano huo wa 10 vinaendelea ikiwemo kilichofanyika leo.