Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vitisho vya ‘kulogwa’ havikumzuia Milika kuepusha watoto na utumikishwaji

Milika Yohana, Mchechemuzi wa Haki za Watoto nchini Tanzania.
UN News
Milika Yohana, Mchechemuzi wa Haki za Watoto nchini Tanzania.

Vitisho vya ‘kulogwa’ havikumzuia Milika kuepusha watoto na utumikishwaji

Sheria na Kuzuia Uhalifu

Mkoani Mwanza, Kaskazini-magharibi mwa Tanzania, mtetezi wa haki za watoto Milika Thomas hukumbwa na vitisho ikiwemo hata ‘kulogwa’ kutokana na azma yake ya kuhakikisha hakuna mtoto anatumikishwa badala ya kwenda shuleni.

Milika anasema msingi wa yeye kubeba ‘bango’ la kuepusha watoto na suluba za maisha badala ya kusoma ni baada ya kuona wazazi kutokana na hali duni ya maisha, kuacha watoto wao waende ziwani kusaka vitoweo vya kulisha familia badala ya kubeba kalamu na madaftari na kujiendeleza kimasomo.

Akizungumza na Evarist Mapesa wa Redio Washirika SAUT FM nchini Tanzania, Milika anasema “nilikuwa nikiona watoto hawasomi wanaenda ziwani, iliniumiza sana. Niligundua baada ya kutembelea zile familia nikaona mama asubuhi anaenda kwenye pombe, vile vile baba anatelekeza familia. Niliona watoto wakienda shule yaani ndio taifa la kesho.

Mwanaidi* si jina lake halisi ni mzazi wa mtoto ‘Julius’* ambaye amekuwa anakwenda ziwani kusaka kitoweo kwa ajili ya familia.

Janeth Ringo, Afisa Miradi, Idara ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto kutoka shirika la Amani Girls. (Programme Officer - Amani Girls Organisation).
UN News
Janeth Ringo, Afisa Miradi, Idara ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto kutoka shirika la Amani Girls. (Programme Officer - Amani Girls Organisation).

“Kwa kweli mtoto wangu alikuwa haendi shule kwa sababu maisha yangu ya duniani yalikuwa magumu sana. Nguo za shule hamna kula kwenyewe kwa shida. Yaani kama vile namtegemea tu Mungu. Unapata msaada wa mahindi au kilo moja ya unga,” anasema Mwanaidi.

Juhudi za Milika zimezaa matunda kwani baada ya kupata mafunzo kutoka shirika lisilo la kiserikali la Angel girls lililoko mjini Mwanza, sasa amefanikiwa kuokoa watoto 25 waliokuwa wakifanyishwa kazi za uvuvi na kilimo.

Mtoto wa Mwanaidi ni Julius na anasema mwenye umri wa miaka saba hakuwahi kabisa kupelekwa shuleni, badala yake alikuwa akielekea ziwani kufanya kazi za uvuvi ili kupata chochote kitakachosaidia kuendesha maisha ya familia yao.

“Mama alikuwa hana hela, lakini sasa amepata fecha na amenunua vifaa vya shule na kunipeleka. Sasa hivi nimeanza kusoma mwaka huu. Ndoto yangu ni kuwa askari,” amesema Julius.

Tazama video nzima hapa