Migogoro, ufurushwaji na magonjwa vyachochea uhaba wa chakula Sudan Kusini
Migogoro, ufurushwaji na magonjwa vyachochea uhaba wa chakula Sudan Kusini
Kaunti mbili katika jimbo la Upper Nile, Sudan Kusini, ziko katika hatari kubwa ya njaa kali katika miezi ijayo kutokana na mzozo unaoongezeka. Migogoro, mashambulizi ya anga, na uharibifu wa makazi yamesababisha watu kuhama kwa wingi na kuathiri vibaya maisha ya wakazi wa maeneo haya. Hali hii pia imesababisha kuzuiliwa kwa usambazaji wa misaada ya kibinadamu, na hivyo kuongeza mateso ya watu walioko hatarini. Imesema taarifa iliyotolewa leo na mashirika ya Umoja wa Mataifa lile la Chakula na Kilimo (FAO), la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) na la Kuhudumia Watoto (UNICEF).
Kaunti mbili katika jimbo la Upper Nile, Sudan Kusini, ziko katika hatari kubwa ya njaa kali katika miezi ijayo kutokana na mzozo unaoongezeka. Migogoro, mashambulizi ya anga, na uharibifu wa makazi yamesababisha watu kuhama kwa wingi na kuathiri vibaya maisha ya wakazi wa maeneo haya. Hali hii pia imesababisha kuzuiliwa kwa usambazaji wa misaada ya kibinadamu, na hivyo kuongeza mateso ya watu walioko hatarini. Imesema taarifa iliyotolewa leo na mashirika ya Umoja wa Mataifa lile la Chakula na Kilimo (FAO), la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) na la Kuhudumia Watoto (UNICEF).
Hali ya uhakika wa chakula (IPC)
Ripoti mpya kutoka Mfumo wa Uainishaji wa Viwango vya Uhakika wa Chakula IPC) inaonesha hali mbaya zaidi ya uhakika chakula katika maeneo ya Sudan Kusini yaliyoathiriwa na mapigano. Katika jimbo la Upper Nile, watu katika kaunti 11 kati ya 13 wanakabiliwa na njaa katika viwango vya dharura, huku kaunti za Nasir na Ulang zikihesabiwa kuwa katika hatari ya njaa kali kabisa (IPC Awamu ya 5). Idadi ya watu wanaokabiliwa na njaa kali imeongezeka mara tatu ikifikia 32,000.
Sehemu zingine za Sudan Kusini ambazo hazijagubikwa na mzozo zimeonesha kuboreka kwa hali ya uhakika wa chakula.Hali imeshuka kutoka dharura, IPC Awamu ya 4 hadi IPC Awamu ya 3, kutokana na mazao mazuri na misaada ya kibinadamu. Hii ni ushahidi wa wazi kwamba amani na utulivu vinaweza kuleta mabadiliko chanya katika uhakika wa chakula.
Hata hivyo, watu milioni 7.7 (asilimia 57 ya idadi ya watu) bado wanakabiliwa na uhaba mkali wa chakula (IPC Awamu ya 3+), na kumekuwa na matukio ya njaa kali (IPC Awamu ya 5) katika maeneo fulani ya Sudan Kusini katika miaka ya karibuni, ambapo mzozo ni sababu kuu. Mara ya mwisho njaa ilipotangazwa rasmi Sudan Kusini ilikuwa mwaka 2017.
Meshack Malo, Mwakilishi wa FAO nchini Sudan Kusini amesema, “Sudan Kusini haiwezi kuruhusu mzozo kuendelea kwa wakati huu. Hii itaangamiza jamii zilizo hatarini kwa njaa kali, kwa sababu wakulima watazuiwa kufanya kazi mashambani. Mabadiliko kutoka IPC Awamu ya 4 hadi Awamu ya 3 katika kaunti kumi ni ushahidi wazi wa faida za amani.”
Changamoto za ufikiaji wa misaada na athari za mzozo
Ufikiaji wa misaada ya kibinadamu bado ni changamoto kubwa katika maeneo ya mzozo, ikiwemo Upper Nile. Hali hii inawaacha watu bila msaada muhimu wakati wa msimu mgumu. Takriban asilimia 66 ya watu wa jimbo hili wanakabiliwa na njaa katika viwango vya mgogoro, dharura au njaa kali sana. Mashirika ya misaada yanaonya kuwa mzozo unaendelea kuathiri vibaya maisha ya watu, kuharibu makazi, na kuongeza bei za chakula sokoni.
Mary-Ellen McGroarty, Mkurugenzi wa WFP nchini Sudan Kusini amesema, “mara nyingine tena, tunaona athari mbaya za mzozo kwa usalama wa chakula nchini Sudan Kusini. Mzozo hauharibui tu makazi na maisha ya watu, bali pia huvunja jamii, hukata njia za masoko, na kupelekea bei ya vyakula kupanda kwa kasi. Amani ya muda mrefu ni muhimu, lakini sasa hivi, ni muhimu timu zetu ziweze kufikia na kusambaza chakula salama kwa familia zilizokumbwa na mzozo huko Upper Nile, kuwasaidia kutoka kwenye hatari ya njaa.”
Ukosefu wa lishe na mlipuko wa kipindupindu
Pia, kuna ongezeko kubwa la ukosefu wa lishe miongoni mwa watoto na wajawazito, huku mlipuko wa kipindupindu ukizidi kuongezeka katika kaunti za Upper Nile na Unity. Idadi ya watoto walio hatarini kukumbwa na ukosefu wa lishe imeongezeka kutoka milioni 2.1 hadi milioni 2.3 mwaka huu. Changamoto za upatikanaji wa huduma za afya na lishe, pamoja na mlipuko wa magonjwa, zinaongeza hatari kwa maisha ya watoto wachanga.
Noala Skinner, mwakilishi wa UNICEF nchini Sudan Kusini. “makadirio haya mapya yanaongeza watoto 200,000 katika hatari ya ukosefu wa lishe . Changamoto za kufikia baadhi ya maeneo yaliyoathirika zaidi, pamoja na kufungwa kwa vituo vya afya na lishe, inapunguza uwezekano wa kuwahudumia na kuwasaidia mapema. Zaidi ya hayo, mlipuko wa kipindupindu umeongeza shida iliyokuwepo, na kuweka maisha ya watoto katika hatari kubwa ya kuishi. Sasa zaidi kuliko wakati wowote, tunahitaji kuendelea na kuongeza huduma za kuzuia ukosefu wa lishe.”
Wito wa haraka wa amani na misaada ya kibinadamu
Mashirika ya Umoja wa Mataifa na wahudumu wa misaada ya kibinadamu wanasisitiza kuwa Sudan Kusini haipaswi kurudi kwenye mzozo. Amri ya amani ni muhimu ili kulinda maisha ya watu na kuzuia janga la njaa. Kwa sasa, ufikiaji wa misaada unapaswa kuboreshwa haraka ili kuokoa maisha ya familia zilizoko hatarini katika kaunti za Upper Nile.