UNHCR yaonya: ufurushwaji wa watu waongezeka wakati ukata wa ufadhili ukishika kasi
UNHCR yaonya: ufurushwaji wa watu waongezeka wakati ukata wa ufadhili ukishika kasi
Watu waliolazimika kukimbia makazi yao kutokana na vita, ukatili na mateso duniani kote imefikia kiwango cha juu kisichovumilika, hasa wakati huu ambapo ufadhili wa misaada ya kibinadamu unapungua kwa kasi.
Kwa mujibu wa Ripoti ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia wakimbizi UNHCR iliyotolewa leo kuhusu mwelekeo wa Ulimwengu, kufikia mwisho wa Aprili mwaka huu, kulikuwa na watu milioni 122.1 waliolazimika kuhama kwa nguvu, ikilinganishwa na watu milioni 120 mwaka uliopita katika kipindi kama hicho.
Hali nchini Syria
Tipoti hiyo imesema watu milioni 13.5 walilazimika kuhama makazi yao kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria vilivyodumu kwa zaidi ya miaka 13, na kuifanya Syria kuwa na mgogoro mkubwa zaidi wa wakimbizi duniani kwa kipindi kirefu. Hali hii imebadilika.
Mwezi Desemba mwaka jana, kupinduliwa kwa utawala wa Assad na vikosi vya upinzani kulizusha matumaini kuwa wengi wa Wasyria wangeweza kurejea nyumbani hivi karibuni.
Kufikia Mei, wakimbizi 500,000 na watu furushwa makwao 1.2 milioni walikuwa tayari wamerudi kwenye maeneo yao ya asili.
Lakini hiyo si sababu pekee ya Syria kupoteza nafasi ya kuwa mgogoro mkubwa zaidi wa wakimbizi duniani.
Sudan yavunja rekodi ya wakimbizi wa ndani
Vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyoanza Sudan zaidi ya miaka miwili iliyopita vimesababisha watu milioni 14.3 kuhama makazi yao tangu Aprili 2022, wakiwemo milioni 11.6 waliokoseshwa makazi ndani ya nchi yao sawa na theluthi moja ya jumla ya idadi ya watu wa Sudan.
Kwa mujibu wa ripoti hii imekuwa rekodi ya juu zaidi kuwahi kutokea ya ufurishwaji wa ndani wa watu.
Ripoti hiyo mpya ya UNHCR imeonesha ukubwa wa tatizo hili, ikielezea hali ya ufurushwaji wa watu kuwa “isiyovumilika,” lakini pia ikabainisha “miale ya matumaini” licha ya athari za haraka za kupunguzwa kwa misaada kutoka kwa wafadhili kote duniani mwaka huu.
“Tunaishi katika wakati wa misukosuko mikubwa katika uhusiano wa kimataifa, huku vita vya kisasa vikisababisha mazingira ya hatari yaliyojaa mateso makali ya kibinadamu,” amesema Kamishna Mkuu wa Wakimbizi, Filippo Grandi.
Kusaka mahali pa amani
Kufikia mwisho wa mwaka 2024, ripoti imesema watu milioni 123.2 duniani walikuwa wamelazimika kuhama makazi yao idadi ya juu zaidi katika muongo mmoja kwa kiasi kikubwa kutokana na migogoro ya muda mrefu Sudan, Myanmar na Ukraine.
Watu milioni 73.5 walifurushwa ndani ya nchi zao, huku wakimbizi milioni 42.7 waliokimbilia mataifa ya nje wakipokelewa na nchi zenye kipato cha chini na cha kati kwa asilimia 73, na asilimia 67 kati yao wakihifadhiwa na nchi jirani.
Sadeqa na mwanawe ni wakimbizi waliokumbwa na ufurushwaji mara kadhaa. Walikimbia Myanmar baada ya mume wa Sadeqa kuuawa mwaka 2024. Walipokuwa Bangladesh waliishi katika kambi ya wakimbizi Waislamu wa Rohingya, lakini msongamano mkubwa uliwalazimu kutoroka tena kwa mashua.
Alipanda mashua hiyo bila kujua inaelekea wapi. Hatimaye waliokolewa baada ya wiki kadhaa baharini, na sasa anaishi na mwanawe nchini Indonesia.
“Tunatafuta mahali tunapoweza kuishi kwa amani,” amesema Sadeqa.
Kuna hadithi nyingi kama ya kwake. Hata hivyo, Bwana. Grandi amesema ripoti inaonyesha “miale ya matumaini.”
Mwaka huu, wakimbizi 188,800 walihamishiwa kwenye makazi ya kudumu katika nchi zinazowapokea ikiwa ni idadi kubwa zaidi katika kipindi cha miaka 40.
Aidha, watu milioni 9.8 walirejea nyumbani mwaka 2024, wakiwemo wakimbizi milioni 1.6 na waliofurushwa kwenye makazi makazi yao milioni 8.2, wengi wao kutoka Afghanistan na Syria.
Suluhu za kudumu
Ingawa watu milioni 8.2 waliorejea makwao ni idadi ya pili kwa ukubwa kuwahi kurekodiwa kwa mwaka mmoja, ripoti imeonesha changamoto zinazowakabili waliorejea.
Kwa mfano, ripoti imesema wakimbizi wengi kutoka Afghanistan na Haiti waliorejea mwaka uliopita walifukuzwa kutoka nchi walizokuwa wamekimbilia.
Ripoti imehimiza kwamba kurejea kwa wakimbizi lazima kuwe kwa hiari na heshima na usalama wa wanaorejea lazima vihifadhiwe wanaporejea kwenye maeneo yao.
Hili linahitaji juhudi za muda mrefu za kujenga amani na maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi.
“Utafutaji wa amani lazima uwe kiini cha juhudi zote za kupata suluhu za kudumu kwa wakimbizi na wale wote waliolazimika kukimbia makazi yao,” amesema Grandi.
Kupunguzwa kwa misaada ya fedha kunatishia usalama
Kwa mujibu wa ripoti katika kipindi cha muongo mmoja uliopita, idadi ya watu waliolazimika kuhama makazi yao duniani imeongezeka mara mbili, lakini kiwango cha fedha kwa ajili ya UNHCR hakijaongezeka kwa kiwango sawa.
Ripoti imeeleza kuwa ukosefu wa ongezeko la fedha unahatarisha jamii zilizokwisha kuwa katika hali ngumu, na kuleta hatari zaidi kwa amani ya kikanda.
“Hali ni mbaya na isiyovumilika, na kuwaacha wakimbizi na wengine wanaokimbia hatari katika mazingira magumu zaidi,” limesema shirika la UNHCR.