Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uongo kuhusu uzazi: Mambo Matano usiyoyajua kuhusu viwango vya uzazi duniani

Mchoro wa rangi ya maji wa mwanamke mjamzito na mwanamume aliyevaa umbo la sare.
© UNFPA/Stina Persson Katika ripoti kuu ya mwaka huu ya Hali ya Idadi ya Watu Duniani, UNFPA ilichunguza baadhi ya watu 14,000 katika nchi 14, na ikagundua kuwa karibu mmoja kati ya watano alisema hawataweza kupata idadi ya watoto ambao wangependa.

Uongo kuhusu uzazi: Mambo Matano usiyoyajua kuhusu viwango vya uzazi duniani

Afya

“Ungependa kupata watoto?” Kila siku, watu kote duniani hujiuliza au kuwauliza wengine swali hili. Lakini pia linaibua swali jingine: “Je, unahisi kuwa na uwezo wa kupata watoto?”

Kwa idadi ya watu inayozidi bilioni 8 duniani, hili limekuwa swali lenye uzito zaidi. Kwa baadhi ya watu, idadi hii ni kubwa kupita kiasi, imegawanywa kwa njia isiyo sawa, na itasababisha uharibifu. Wengine wanahofia kupungua kwa idadi ya watu duniani na kwamba jamii haziwezi kuhimili uzee unaoongezeka huku viwango vya uzazi vikishuka.

Hata hivyo, kati ya hofu hizi zote, ni wachache wanaouliza watu kile wanachokitaka kwa kweli. Ripoti ya mwaka huu ya Hali ya Idadi ya Watu Duniani, Janga Halisi wa Uzazi: Harakati ya Uhuru wa Kuamua Uzazi Katika Dunia Inayobadilika, iliuliza maswali haya na mengine, na kufichua mambo 5 kuhusu uzazi.

1. Mtu 1 kati ya 5 hapati idadi ya watoto anayopenda kuwa nao

Wakati watunga sera na wachambuzi wanapotaharisha kuhusu viwango vya uzazi, mara nyingi huhisi kuwa watu wanapata watoto kwa sababu wanaweza na wanataka, na kama hawawapati basi ni kwa sababu hawawezi au hawataki.

Lakini ripoti hii kuu ya UNFPA mwaka huu, iliyowahoji watu wapatao 14,000 katika nchi 14, iligundua kuwa karibu mtu 1 kati ya 5 alisema hatoweza kupata idadi ya watoto anayowatamani. Wengi wanatarajia kupata wachache au kutopata kabisa, ilhali baadhi walisema huenda wakapata zaidi ya wanavyopenda.

Mwanamke na watoto watatu wadogo wameketi mezani, wakifanya shughuli ya kujifunza wakiwa na karatasi na vifaa vya kuandikia.
© UNFPA/Artur Lupu Katika Jamhuri ya Moldova, baadhi ya programu zinasaidia familia kusawazisha huduma ya watoto na kazi.

2. Watu wengi wanataka watoto – lakini wengi wamezuiwa kuwa wazazi

Mara nyingi wanawake na vijana ndiyo wanaolaumiwa kwa ongezeko la idadi ya uzee na kushuka kwa viwango vya uzazi na idadi ya watu kwa jumla. Vichwa vya habari huwalaumu kwa “kukwepa ndoa” au kusema vijana “wameshindwa kuanza maisha.” Lakini utafiti unaonesha kuwa watu wengi wanataka watoto wawili au zaidi, lakini wana hofu kwamba hawawezi kutimiza hilo.

Zaidi ya nusu ya waliojibu walisema sababu kuu za kupata watoto wachache ni hofu za kifedha gharama za nyumba, malezi ya watoto na ukosefu wa usalama wa ajira.

Kuajiri wanawake wengi zaidi katika nguvu kazi ni mojawapo ya njia bora zaidi za kukabiliana na uhaba wa wafanyakazi. Hali hii inaonesha kuwa kushuka kwa uzazi na kudorora kwa uchumi vinachangiwa na jambo moja kuu, ukosefu wa usawa wa kijinsia.

Pale ambapo wanawake hawalazimiki kuchagua kati ya kazi na kuwa mama, wanaweza kupata familia wanayoitamani. Anastasia Aslan kutoka Moldova anasema, “tulipokuwa tukipanga kupata mtoto mwingine, tuliangalia kama tungeweza kujitegemea na kujikimu kifedha wakati wa likizo yangu ya uzazi na jinsi ya kugawana kazi za nyumbani na kazi ya kawaida .” Kwa upande wake, mazingira na masharti nafuu ya kazi yalirahisisha uamuzi. “Natumai kampuni zaidi zitahamasisha sera kama hizo, ili kuwaunga mkono akina mama kupanga maisha yao ya baadaye na familia zao kwa kujiamini.”

3. Watu wengi wanalazimishwa kupata watoto wasiotaka au kabla hawajajiandaa

Tatizo si tu kwamba watu wanapata watoto wachache kuliko wanavyotaka. Wengi pia hawana uwezo wa kuzuia ujauzito wasiotaka au kabla hawajajiandaa.

Takwimu za UNFPA zinaonesha kuwa 1 kati ya 3 amesema yeye au mwenza wake walipata ujauzito bila kupanga. 1 kati ya 5 amesema alilazimishwa kupata mtoto. Asilimia 25 ya wanaume na theluthi ya wanawake wanasema walishindwa kusema “hapana” kwa tendo la ndoa.

Mchoro wa rangi ya maji na mchanganyiko wa vyombo vya habari wa umbo la kike dhidi ya mandharinyuma nyekundu na njano dhahania.
© UNFPA/Marianna Gefen Suala sio tu watu kuwa na watoto wachache kuliko wanavyotaka. Watu wengi sana hawawezi kuzuia mimba wasiyoitaka au ambao hawako tayari.

Huko Nigeria, ambapo wanawake hupata wastani wa watoto 5, zaidi ya 1 kati ya 10 waliripoti matarajio ya kupata watoto zaidi ya wanavyotaka. Hili linachangiwa jamii na ukosefu wa huduma za afya ya uzazi.

Talatu Yakubu, mtoa huduma wa afya katika Hospitali ya Kuje, Abuja, amesema: “Kuna dhana potofu. Wanawake wengine huamini sindano ya uzazi ya miezi 3 husababisha utasa. Wengine hufikiri hawapaswi kuanza kutumia njia za kupanga uzazi hadi wawe na watoto 3 au 4.”

Anasisitiza kuwa wanaume wanapaswa kushiriki kikamilifu. “Waje na wake zao kupata ushauri. Taarifa ni nguvu, na unachojua kinaweza kufanyiwa kazi haraka."

4. Sera nyingi za uzazi hazifanyi kazi, nyingine huwa na athari kinyume

Hata katika nchi zenye idadi tosha au ongezeko la watu, watunga sera wanahofia idadi ya watu inayoshuka. Wengine wamejaribu kutoa motisha kama “bonasi za mtoto” au kusaidia gharama za kulea mtoto. Lakini juhudi hizi mara nyingi hazina matokeo ya muda mrefu.

Kundi la watu wazima na watoto linatembea kwenye njia ya changarawe katika eneo la vijijini lenye jengo la manjano na miti nyuma yake.
© UNFPA/Óscar González Katika Jamhuri ya Dominika, programu kama vile Casa Clave na Unidad de Atención Primaria zinasaidia vijana kuepuka mimba.

Katika hali mbaya zaidi, baadhi ya sera zimeanza kurudisha nyuma mafanikio ya haki za afya ya uzazi mfano kupiga marufuku elimu ya uzazi mashuleni, kupunguza upatikanaji wa uzazi wa mpango, na kufanya utoaji mimba kuwa kosa la jinai.

Haya yanaweza kuwa na athari mbaya zaidi kama vile kuongezeka kwa utoaji mimba usio salama, unaochangia vifo vya kina mama na utasa wa baadaye.

Kwa ujumla, juhudi za kulazimisha watu kupata watoto zaidi hushindwa. Kwa hiyo, nini hufanya kazi?

5. Watu wanahitaji usalama, usawa na matumaini

Ukweli mmoja umebainika wazi kuwa watu wachache sana wana mamlaka kamili ya kuamua kuhusu uzazi wao.

Karibu robo ya waliohojiwa wamesema walikuwa na hamu ya kupata watoto lakini wanahisi hawawezi kutokana na sababu za kifedha, kiafya, au ukosefu wa huduma. Zaidi ya asilimia 20 wamesema hali ya dunia kama vita, milipuko ya magonjwa, siasa na mabadiliko ya tabianchi huwafanya wasitake kupata watoto wengi.

Mchoro wa kisanii wa rangi ya maji unaoonyesha nyuso mbili katika wasifu zinazokaribia kubusu, zikiwa zimepangwa dhidi ya mandhari ya bluu iliyokolea.
© UNFPA/Graham Dean Watu wanahitaji tumaini la maisha yao ya baadaye, na ya baadaye ya watoto wanaotaka kuwa nao.

Badala ya kueneza hofu nchi zinapaswa kuongeza chaguzi na fursa za uzazi.

Hii ni pamoja na:

  • Kuboresha upatikanaji wa huduma za afya ya uzazi kwa wote, hasa makundi yaliyopuuzwa – watu wenye ulemavu, makabila madogo, wahamiaji na wengine wengi
  • Kusaidia wanawake kuingia na kubaki kazini bila kujinyima nafasi ya kuwa mama.
  • Kuondoa unyanyapaa kwa wanaume wanaojihusisha na malezi.
  • Kupanua msaada wa kifamilia, kama huduma za uzazi na uasili kwa watu wa jamii ya LGBTQIA+, watu wasio na wenza, na wanawake waliokuwa wakichukuliwa kuwa “wamezeeka”

Pia inamaanisha kuheshimu watu wasiotaka watoto kabisa, chaguo halali linalostahili kulindwa dhidi ya unyanyapaa na shinikizo.

Na mwisho, watu wanahitaji matumaini kwa maisha yao, na kwa maisha ya watoto wanaotamani kuwapata. Watunga sera lazima wasikilize kile ambacho watu wanasema wanahitaji.

Dkt. Natalia Kanem, Mkurugenzi Mtendaji wa UNFPA amesema “Idadi kubwa ya watu hawawezi kuunda familia wanazotamani. Tatizo si hamu ya kupata watoto, bali ukosefu wa chaguo na hili lina athari kubwa kwa watu binafsi na jamii. Huo ndio janga halisi wa uzazi.”  Anasema kuwa suluhisho liko katika kujibu mahitaji haya ya watu:

·        Likizo ya uzazi inayolipwa

·        Huduma nafuu za uzazi

·        Wenza wanaosaidia.