Haiti yashuhudia kiwango cha juu cha wakimbizi wa ndani
Haiti yashuhudia kiwango cha juu cha wakimbizi wa ndani
Takribani watu milioni 1.3 sasa wamekimbia makazi yao ndani ya Haiti, ikiwa ni ongezeko la asilimia 24 tangu Desemba 2024, kulingana na ripoti mpya iliyotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji (IOM). Mlipuko huu unaashiria idadi kubwa zaidi ya watu waliokimbia makazi yao kutokana na ghasia kuwahi kurekodiwa nchini humo.
Taarifa iliyosambazwa na IOM leo Juni 11 mjini Geneva, Uswisi na Port-au-Prince – Haiti inamnukuu Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, Amy Pope akisema, “nyuma ya takwimu hizi kuna maisha ya watu binafsi wenye mateso yasiyoelezeka, watoto, akina mama, wazee, wengi wao wamelazimika kukimbia makazi yao mara kadhaa, mara nyingi bila chochote, na sasa wanaishi katika mazingira yasiyo salama wala endelevu. Tunapaswa kuchukua hatua haraka. Uvumilivu wa watu wa Haiti ni wa kusisimua, lakini si suluhisho la pekee. janga hili halipaswi kuwa hali ya kawaida.”
Wakati jiji la Port-au-Prince likibakia kuwa kitovu cha mgogoro huu, ghasia za magenge sasa zimeenea nje ya mji mkuu. Mashambulizi ya hivi karibuni katika mikoa ya Centre na Artibonite yamelazimisha makumi ya maelfu ya watu zaidi kukimbia, wengi wao sasa wakiishi katika mazingira magumu na makazi ya muda. Ingawa karibu robo ya wakimbizi wote wa ndani bado wako mji mkuu, idadi inayoongezeka ya watu wanakimbilia maeneo mengine ya nchi wakitafuta usalama. Kaskazini, idadi ya watu waliolazimika kuacha makazi yao imeongezeka kwa karibu asilimia 80, inaeleza IOM.
Katika mkoa wa Artibonite, ghasia katika eneo la Petite Rivière peke yake zimesababisha maelfu zaidi kukimbia, na hivyo kufanya jumla ya wakimbizi katika eneo hilo kufikia zaidi ya 92,000. Hali ni ya kutisha zaidi katika mkoa wa Centre, ambapo mapigano katika miji kama Mirebalais na Saut-d’Eau yameongeza zaidi ya mara mbili idadi ya watu waliokimbia katika kipindi cha miezi michache, kutoka takriban 68,000 hadi zaidi ya 147,000. Wengi sasa wanakabiliwa na maisha bila huduma za afya, shule, au maji safi, jambo linalozidi kuwaumiza familia ambazo tayari ni dhaifu.
Kadri watu zaidi wanavyolazimika kukimbia, idadi ya maeneo ya makazi ya muda pia inazidi kuongezeka. Tangu Desemba, maeneo haya yameongezeka kutoka 142 hadi 246. Ongezeko kubwa zaidi limeonekana katika maeneo ambayo hapo awali hayakuwa na kambi yoyote, kama vile mkoa wa Centre, ambao sasa una maeneo 85. Hata hivyo, karibu asilimia 83 ya wakimbizi hawa wanahifadhiwa na familia wenyeji, hali inayoongeza mzigo mkubwa kwa kaya ambazo tayari zinapambana, hasa katika maeneo ya vijijini.
IOM inasaidia
IOM inaendelea kuchukua jukumu kubwa katika kusaidia misaada ya kibinadamu. Katika mwezi uliopita, shirika hilo liliwasaidia zaidi ya watu 20,000 kwa kuwapatia vifaa muhimu vya nyumbani kama ndoo na vifaa vya kupikia, likasambaza zaidi ya lita milioni 3 za maji safi, na kutoa huduma za afya za msingi kwa watu 6,000. Zaidi ya hayo, IOM imedumisha msaada wa afya ya akili kwa kuwafikia watu zaidi ya 8,500 waliokimbia makazi yao. Timu za IOM kwa sasa zipo mkoani Centre kufanya tathmini ya mahitaji ya sekta mbalimbali na kujiandaa na mwitikio wa haraka.
Kadri mahitaji yanavyozidi kuongezeka, IOM inasisitiza wito wake kwa jamii ya kimataifa kuongeza msaada wake. Bila ufadhili na upatikanaji wa haraka, mamilioni ya watu wako hatarini. Misaada ya kibinadamu ni ya lazima, lakini haitoshi peke yake. Suluhisho endelevu linapaswa kushughulikia mizizi ya tatizo la uhamishaji, kuboresha upatikanaji wa huduma muhimu, na kuunda mbadala halisi kwa vijana dhidi ya kujiunga na magenge ya ghasia. Hatua hizi ni muhimu katika kuvunja mzunguko wa ghasia na kurejesha utulivu.