Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kucheza kuna nafasi kubwa katika makuzi ya mtoto

Tarehe 5 Aprili 2025, watoto wakicheza katika eneo rafiki kwa watoto (CFS) linaloungwa mkono na UNICEF katika mtaa wa Alhatana, Omdurman, Jimbo la Khartoum, Sudan
© UNICEF/Ahmed Mohamd
Tarehe 5 Aprili 2025, watoto wakicheza katika eneo rafiki kwa watoto (CFS) linaloungwa mkono na UNICEF katika mtaa wa Alhatana, Omdurman, Jimbo la Khartoum, Sudan

Kucheza kuna nafasi kubwa katika makuzi ya mtoto

Utamaduni na Elimu
  • Je umemwekea mwanao fursa ya kucheza?
  • Kucheza hujenga stadi na udadisi
  • Baadhi ya watoto hunyimwa kucheza

Leo ni siku ya kimataifa ya kucheza, maudhui yakiwa Chagua Kucheza – Cheza Kila siku, lengo ikiwa ni kukumbusha serikali, sekta ya biashara, shule na familia kuchukua maamuzi yanayopatia kipaumbele michezo kwa watoto.

Katika wavuti mahsusi wa siku hii, inaelezwa kuwa kutafanyika tukio la ngazi ya juu likileta pamoja wawakilishi wa serikali na nchi wanachama kuchagiza umuhimu wa kucheza, tukio linaloandaliwa kwa pamoja na mashirika ya Umoja wa Mataifa, lile la Kuhudumia Watoto, UNICEF na la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO.

Kucheza hujenga stadi na udadisi

Azimio la kupitisha siku hii lilipitishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwezi Aprili mwaka jana wa 2024 na ambalo pamoja na mambo mengine limetambua nafasi ya michezo katika kujenga stadi muhimu za maisha zinazoweza kuhamishika za kimwili, kijamii, kiakili, mawasiliano na kihisia katika hatua zote za maisha.

Halikadhalika athari chanya za mchezo katika kuendeleza uvumilivu na ustahimilivu, na kuwezesha ujumuishaji wa kijamii, kuzuia migogoro na kujenga amani.

Mkurugenzi Mkuu wa UNICEF Catherine Russell anasema kuwa, “mchezo ni ishara kwamba watoto wanajisikia salama, wanatunzwa na wanapendwa. Wanahisi kwa kiasi fulani kwamba wanaweza kuwa watoto hata katikati ya magumu makubwa.”

Watoto wakimbizi kutoka Sudan Kusini wakicheza kuruka kamba katika makazi ya wakimbizi ya Palabek Ogili nchini Uganda
© UNICEF/Jimmy Adriko
Watoto wakimbizi kutoka Sudan Kusini wakicheza kuruka kamba katika makazi ya wakimbizi ya Palabek Ogili nchini Uganda

Je wajua?

  • Asilimia 71 ya watoto wanasema kwamba michezo ni muhimu kwa sababu huwafanya wawe na furaha, na asilimia 58 wanasema kwamba huwasaidia kupata marafiki na kufurahia muda pamoja na wengine.
  • Inakadiriwa kuwa watoto milioni 160 kote duniani wanafanya kazi badala ya kucheza au kujifunza.
  • Ni mtoto 1 kati ya 4 tu anayechukua muda wa kucheza nje mitaani mara kwa mara, ikilinganishwa na kizazi cha mababu na mabibi zao ambapo karibu robo tatu walisema walikuwa wakicheza nje mara kadhaa kwa wiki.
  • Asilimia 41 ya watoto wameambiwa waache kucheza nje na wazazi wao au watu wazima wengine kama majirani.

Faida za kucheza: Kujifunza, uhusiano

Umoja wa Mataifa unasema kuwa watoto hujifunza vyema zaidi kupitia michezo. Michezo huleta fursa madhubuti za kujifunza katika nyanja zote za ukuaji – kiakili, kijamii, kihisia na kimwili.

Halikadhalika, kupitia michezo, watoto hujifunza kuunda mahusiano na wengine, kujenga aina mbalimbali za uongozi, kukuza ustahimilivu, kuhimili changamoto za kijamii na mahusiano pamoja na kushinda hofu zao.

Zaidi ya yote, watoto hucheza ili kuelewa dunia inayowazunguka. “Kwa ujumla, michezo huwapa watoto jukwaa la kujieleza na kukuza fikra za ubunifu na ubunifu wenyewe, ambavyo ni stadi muhimu katika dunia ya kiteknolojia na ubunifu tunayoiishi leo,” umesema Umoja wa Mataifa.

Hata hivyo Umoja Mataifa unataka wadau kuweka mazingira rafiki ili watoto kokote pale waliko waweze kucheza bila madhara yoyote.