Vizingiti vya kijamii na kiuchumi, ndio chanzo cha janga la uzazi duniani na si uchaguzi: UNFPA
Vizingiti vya kijamii na kiuchumi, ndio chanzo cha janga la uzazi duniani na si uchaguzi: UNFPA
Changamoto ya uzazi duniani si kuhusu watu kukataa kuwa wazazi ni kuhusu kunyimwa fursa ya kuchagua kuwa mzazi imesema ripoti mpya ya shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu na afya ya uzazi UNFPA iliyotolewa leo na kuonesha kuwa kuwa matatizo ya kiuchumi, ukosefu wa usawa wa kijinsia, na hofu kuhusu mustakbali vinawazuia mamilioni ya watu kupata familia wanazotamani.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo Karibu asilimia 40 ya watu wanasema changamoto ya kifedha ndio kikwazo kikuu.
Mmoja kati ya watu wanne alihisi kuwa hakuwa na uwezo wa kupata mtoto wakati alipotaka.
“Huu siyo mgogoro wa viwango vya uzazi ni mgogoro wa uhuru,” amesema Mkurugenzi Mtendaji wa UNFPA Natali Kanem na kuongeza kuwa “Uchaguzi wa kweli wa uzazi unamaanisha kuondoa vikwazo, si kulazimisha maamuzi.”
Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA) limezindua ripoti yake kuu ya hali ya idadi ya watu duniani siku ya Jumanne,
Ikiwa na kichwa cha habari “Janga halisi la uzazi: Harakati za kuwa na uwezo wa kuamua uzazi katika dunia inayobadilika”,ripoti hiyo inasema kuwa kinachotishiwa kwa kweli ni uwezo wa watu kuchagua kwa uhuru lini na iwapo wapate watoto.
Changamoto za kifedha
Ripoti hii inatokana na utafiti wa UNFPA/YouGov uliofanywa karibuni katika nchi 14 zinazowakilisha kwa pamoja asilimia 37 ya watu wote duniani.
Ripoti inasema vizingiti vya kiuchumi vilitajwa kuwa sababu kuu, ambapo asilimia 39 ya washiriki walieleza kuwa ugumu wa kifedha ndio sababu kuu ya kupata watoto wachache kuliko walivyopenda.
Hofu ya mustakabali kuanzia mabadiliko ya tabianchi hadi vita pamoja na ukosefu wa ajira, zilitajwa na asilimia 19 na 21 ya washiriki.
Asilimia 13 ya wanawake na asilimia 8 ya wanaume walieleza kuwa mgawanyo usio sawa wa majukumu ya nyumbani ni sababu ya kutopata watoto kwa kiwango walichotamani.
Utafiti huo pia umebainisha kuwa mtu 1 kati ya 3 watu wazima amewahi kupata ujauzito usiopangwa, 1 kati ya 4 walihisi kushindwa kupata mtoto kwa wakati waliotaka, na 1 kati ya 5 waliripoti kushinikizwa kupata watoto wasiowataka.
Ripoti imeonya kuwa kuna idadi inayoongezeka ya watu ambao hawana uhuru wa kuanzisha familia kwa sababu ya gharama kubwa za maisha, ukosefu wa usawa wa kijinsia, na hali ya sintofahamu kuhusu mustakabali.
Suluhisho kwa janga la uzazi
Ripoti hiyo inaonya dhidi ya hatua rahisi na za kulazimisha kukabiliana na viwango vya chini vya uzazi kama vile kutoa bonasi kwa wanaopata watoto au kuweka malengo ya uzazi ambayo mara nyingi huwa siyo ya mafanikio na huweza kuvunja haki za binadamu.
Badala yake, UNFPA inazihimiza serikali kuongeza chaguo kwa kuondoa vikwazo vya uzazi vilivyotajwa na raia wao.
Hatua zinazopendekezwa ni pamoja na kufanya uzazi uwe wa gharama nafuu zaidi kupitia uwekezaji katika makazi, kazi zenye staha, likizo ya uzazi inayolipwa, na huduma kamili za afya ya uzazi.
Uhamiaji kama suluhisho
Shirika hilo pia linahimiza serikali kuangalia uhamiaji kama mkakati muhimu wa kushughulikia uhaba wa wafanyakazi na kudumisha tija ya kiuchumi katika enzi ya kushuka kwa viwango vya uzazi.
Kuhusu usawa wa kijinsia, ripoti inatoa wito wa kushughulikia unyanyapaa dhidi ya baba wanaojihusisha na malezi, mazingira ya kazi yanayowatenga kina mama, vizuizi vya haki za uzazi, na tofauti zinazozidi kuongezeka za mitazamo kati ya vizazi vichanga zinazochangia kuongezeka kwa watu wasioo au kuolewa.