Sudan yakabiliwa na janga la njaa WFP yatoa wito wa hatua za haraka za kimataifa
Sudan yakabiliwa na janga la njaa WFP yatoa wito wa hatua za haraka za kimataifa
Tishio la baa la njaa linaendelea kuiandama Sudan iliyoharibiwa vibaya na vita, limeonya leo Shirika laUmoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani WFP, likitoa wito wa dharura kwa jamii ya kimataifa kusaidia kukidhi mahitaji yanayoongezeka na kuzuia maafa zaidi ya kibinadamu.
Mkurugenzi wa WFP nchini Sudan, Laurent Bukera, akizungumza kutoka Port Sudan, amesema kuwa licha ya shirika hilo kupanua msaada wake na kufikia karibu watu milioni moja mjini Khartoum kwa msaada wa chakula na lishe, hali bado ni ya kutisha. “Tunahitaji kuendeleza kasi hii,” amesisitiza. “Maeneo kadhaa kusini mwa nchi yako hatarini kukumbwa na baa la njaa.”
Khartoum yafanana na mji wa mizimu
Katika taarifa ya hivi karibuni kutoka kwa ujumbe wa tathmini mjini Khartoum, Bukera amesema kuwa vitongoji vingi vimeharibiwa na kutelekezwa. “Ni kama mji wa mizimu,” amesema, akiongeza kuwa rasilimali zilizopo zinazidiwa uwezo huku jamii nyingi zikihifadhi wakimbizi wa ndani wakiwa katika hali ya kukata tamaa.
Mapigano kati ya Jeshi la Sudan na Kikosi chaMsaada wa Haraka RSF, yalianza kufuatia kuvunjika kwa mpango wa mpito kuelekea utawala wa kiraia mwaka 2023.
Zaidi ya miaka miwili ya mzozo imeharibu miundombinu na huduma muhimu kama maji safi, hali ambayo imechangia mlipuko wa kipindupindu na taarifa za miili kuoza katika Mto Nile karibu na Omdurman.
Dola milioni 500 zahitajika kuzuia janga kubwa zaidi la kibinadamu
Licha ya michango “ya ukarimu kutoka kwa wahisani, WFP inakabiliwa na upungufu wa ufadhili wa dola milioni 500 ili kuendeleza msaada wa dharura wa chakula na fedha taslimu kwa miezi sita ijayo.”
Tayari shirika hilo limelazimika kupunguza baadhi ya bidhaa muhimu kama mafuta na kunde kutoka kwenye vikapu vya msaada katika majimbo ya Khartoum, Blue Nile, Al Jazeera na Sennar.
Vyakula vya lishe kwa watoto wadogo na akinamama wajawazito au wanaonyonyesha pia havipatikani tena kutokana na ukosefu wa fedha.
“Jumuiya ya kimataifa lazima ichukue hatua sasa,” amesema Bukera. “Tuzuie njaa katika maeneo yaliyoathirika zaidi na kuwekeza katika kuijenga upya Sudan. Wakati huo huo, tunapaswa kudai ulinzi kwa raia wa Sudan na wafanyakazi wa misaada ya kibinadamu.”
WFP yaongeza msaada licha ya changamoto
Licha ya changamoto nyingi za usalama na miundombinu, WFP sasa inawafikia watu milioni nne kila mwezi kote Sudan idadi ambayo ni karibu mara nne zaidi ya ilivyokuwa mwanzoni mwa 2024.
Ufikiaji wa maeneo mapya, ikiwemo Khartoum, umewezesha upanuzi huu.
Misaada hiyo pia inajumuisha fedha taslimu ili kuchangamsha masoko ya ndani, pamoja na msaada kwa biashara ndogondogo na maduka ya kuoka mikate yanayojaribu kuanzishwa tenakwa akili ya juhudi za kuimarisha uthabiti wa jamii kwa muda mrefu.
“Tumeongeza haraka operesheni zetu kukidhi mahitaji yanayoendelea kuongezeka,” alisema Bukera.
“Tunatarajia kuwafikia watu milioni saba kila mwezi, tukiwapa kipaumbele wale walio hatarini zaidi kwa njaa katika maeneo kama Darfur, Kordofan na Al Jazeera.”
WFP imesisitiza kuwa bila msaada wa haraka wa kimataifa, juhudi za kuzuia njaa, kurejesha huduma muhimu, na kuimarisha jamii huenda zikakwama jambo ambalo litakuwa na athari mbaya kwa mamilioni ya Wasudan walioko kwenye ukingo wa janga.