Afrika iko mstari wa mbele katika kulinda bahari: UNOC3
Afrika iko mstari wa mbele katika kulinda bahari: UNOC3
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ametoa wito mzito wa kuchukua hatua katika mkutano wa kilele wa “Afrika kwa Ajili ya Bahari”, kandoni mwa mkutano wa tatu wa Umoja wa Mataifa wa Bahari UNOC3 mjini Nice Ufaransa akisisitiza kuwa hatim ya Afrika haiwezi kutenganishwa na afya ya bahari zinazolizunguka bara hilo.
Akihutubia viongozi na wageni mashuhuri wakiwemo Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa na Mkurugenzi wa Taasisi ya Mohammed VI, Binti Mfalme Lalla Hasnaa wa Morocco miongoni mwa wengine , Guterres ameitaja Afrika kuwa “nguvu ya baharini yenye zaidi ya kilomita 30,000 za pwani na nchi 38 za pwani. Hatima yake pia inaandikwa katika maji yake,” alisema.
Utajiri wa Uchumi wa bluu uko hatarini
Licha ya rasilimali zake kubwa, Katibu Mkuu ameonya kuwa utajiri wa bahari wa Afrika uko katika hatari kubwa kutokana na uchafuzi wa mazingira, uvuvi haramu, na athari mbaya za mabadiliko ya tabianchi. Ameongeza kuwa usalama wa baharini unazidi kutishiwa na uharamia, usafirishaji haramu wa silaha na watu, pamoja na uhalifu wa kimataifa.
Guterres ameelezea mafanikio yaliyopatikana kupitia Mpango wa Yaoundé uliosaidia kupunguza visa vya uharamia katika Ghuba ya Guinea kama mfano wa hatua zinazowezekana kuigwa sehemu nyingine duniani.
Suluhu za Kiafrika zinazoongoza dunia
Guterres amesifu hatua za Afrika katika kuendeleza suluhu endelevu za bahari. Kuanzia ushirikiano wa kikanda hadi Mkakati wa Muungano wa Afrika wa Bahari wa Mwaka 2050, ameeleza kuwa Afrika imekuwa mstari wa mbele katika mazungumzo ya kimataifa.
Amesisitiza mchango mkubwa wa Kundi la Afrika katika mazungumzo ya Mkataba wa BBNJ kuhusu utofauti wa viumbe wa baharini nje ya maeneo ya kitaifa, ambao umepatikana kwa masharti ya usawa, uhamisho wa teknolojia na ujenzi wa uwezo.
“Afrika inasikika kwa sauti kubwa na wazi,” amesema Katibu Mkuu katika taarifa yake.
Uwekezaji ni muhimu ili kuufungua uwezo
Ili kutimiza uwezo wake wa baharini, Afrika inahitaji kile alichokiita Guterres “msukumo wa kisiasa na kifedha.” Ametoa wito wa uwekezaji katika miundombinu yenye mnepo dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, kama vile bandari za kisasa zitakazosaidia kuunganisha nchi za pwani na zile zisizo na pwani kwa minajili ya ukuaji wa pamoja.
“Hakuna nchi inayopaswa kuachwa nyuma,” amesema, akisisitiza umuhimu wa uchumi wa bahari unaojumuisha nishati mbadala, ufugaji wa samaki na utalii wa mazingira unaozalisha ajira hasa kwa vijana na wanawake.
Haki na mageuzi kwa mustakabali endelevu
Katibu Mkuu pia amegusia dhuluma za kihistoria ambazo zimeziacha nchi za Afrika nyuma katika uwekezaji wa bahari na uwakilishi wa kifedha duniani. “Dhuluma hizi pia zinaonekana baharini,” amesema, akihimiza mageuzi ya taasisi za fedha za kimataifa ili kuhakikisha usawa na haki kwa nchi zinazoendelea. Amerejelea wito wa “Mkataba wa Zama Zijazo” uliopitishwa Septemba 2024, unaotaka mfumo wa kifedha wa dunia uwe wa haki na unaoendana na hali halisi za sasa.
Afrika imechukua usukani
Akihitimisha hotuba yake, Guterres ametoa taswira ya Afrika yenye mafanikio na inayolinda mazingira: “Kutoka Dakar hadi Djibouti, kutoka Cape Town hadi Casablanca, Afrika inaonesha kuwa ustawi na utunzaji wa mazingira vinaweza kwenda sambamba.”
Amehimiza washirika wa kimataifa kuitambua Afrika si kama mnufaika tu, bali kama kiongozi wa kweli katika hatua za kulinda bahari. “Dunia inahitaji Afrika kukabiliana na changamoto za bahari. Na bahari inahitaji Afrika ichukue usukani,” amesema.