Bendera ya UN yapandishwa Nice kuelekea kuanza UNOC3 Jumatatu hii
Promenade des anglais, Nice, Ufaransa
Bendera ya UN yapandishwa Nice kuelekea kuanza UNOC3 Jumatatu hii
Tabianchi na mazingira
Li Junhua, Mkuu wa Idara ya Masuala ya Uchumi na Kijamii ya Umoja wa Mataifa ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Mkutano wa Tatu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Bahari, (UNOC3) amesema, “kesho mkutano unaanza, na umuhimu wake haujawahi kuwa mkubwa kuliko wakati huu.”
Wakati wa hafla ya kupandisha bendera leo (8 Juni) huko Nice, Ufaransa ambako bendera ya Umoja wa Mataifa imepandishwa sambamba na bendera ya mwenyeji Ufaransa, Bwana Junhua amesema, “bahari zetu ziko hatarini, na tupo katika kipindi nyeti kwa ushirikiano wa kimataifa. Mkutano huu ni fursa muhimu sana ya kukabiliana moja kwa moja na changamoto hizi, na kujitolea kwa uwekezaji na hatua za mabadiliko zinazohitajika kwa ajili ya afya ya bahari yetu.”
Kwa upande wa Katibu Mkuu wa UNOC3 upande wa Ufaransa, Anne de Blic, amesema, “Leo, bendera ya Umoja wa Mataifa inapoinuliwa juu ya Bandari ya Lympia katika siku hii ya Kimataifa ya Bahari, kwa ishara tunaingia katika Eneo la Bluu, eneo rasmi la Mkutano wa Tatu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Bahari. Hafla hii inaashiria siyo tu kukabidhiwa rasmi kwa bandari hii ya kihistoria kwa Umoja wa Mataifa, bali pia mwanzo wa wiki ya kujitolea kwa pamoja, uwajibikaji, na matumaini.”
Kuhusu mkutano
Mkutano wa ngazi ya juu wa mwaka 2025 wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Kusaidia Utekelezaji wa Lengo la Maendeleo Endelevu la 14: Kuhifadhi na kutumia bahari kwa njia endelevu, bahari kuu, na rasilimali za baharini kwa maendeleo endelevu (Mkutano wa Bahari wa 2025 wa Umoja wa Mataifa) utafanyika Nice, Ufaransa kuanzia Jumatatu hii tarehe 9 hadi 13 Juni 2025, ukiandaliwa kwa pamoja na Ufaransa na Costa Rica.
Mkutano huu utajenga juu ya Mikutano ya awali ya Bahari ya Umoja wa Mataifa, iliyofanyika mwaka 2017 huko New York na kuandaliwa na Sweden na Fiji, na mwaka 2022 huko Lisbon, Ureno, kwa ushirikiano wa Ureno na Kenya.
Mpango wa Hatua za Bahari wa Nice, utakaoundwa na tamko la kisiasa na orodha ya ahadi za hiari kutoka kwa wadau mbalimbali, utapitishwa kufuatia majadiliano ya kimataifa wakati wa Mkutano huo.