Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkutano kuhusu bahari kuanza Jumatatu Juni 9 mjini Nice, Ufaransa

Zaidi ya 50% ya viumbe vya baharini vinakabiliwa na tishio la kutoweka kufikia 2100.
© Daniel Sly
Zaidi ya 50% ya viumbe vya baharini vinakabiliwa na tishio la kutoweka kufikia 2100.

Mkutano kuhusu bahari kuanza Jumatatu Juni 9 mjini Nice, Ufaransa

Tabianchi na mazingira

Tarehe 9 Juni, wajumbe kutoka kote duniani watakutana katika Mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu Bahari (UNOC3), mjini Nice, Ufaransa, ili kuharakisha hatua na kuhamasisha wadau wote kulinda na kutumia bahari kwa njia endelevu.

Katika mahojiano kabla ya Mkutano huo, Li Junhua, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na Masuala ya Kiuchumi na Kijamii na Katibu Mkuu wa Mkutano huo wa UNOC3, alisema kuwa bahari inakabiliwa na janga lisilo la kawaida kutokana na mabadiliko ya tabianchi, uchafuzi unaotokana na plastiki, upotevu wa mifumo ikolojia, na matumizi kupita kiasi ya rasilimali za baharini.

Kaulimbiu kuu ya Mkutano huo ni: “Kuharakisha hatua na kuhamasisha wadau wote kulinda na kutumia bahari kwa njia endelevu.”

Mkutano huu, ambao utajumuisha kikao cha ufunguzi, mikutano kumi ya jumla, Majukwaa kumi ya Hatua za Bahari, na kikao cha kufunga, unalenga kuunga mkono hatua za dharura zaidi za kulinda na kutumia bahari, bahari kuu, na rasilimali za baharini kwa maendeleo endelevu, pamoja na kubaini njia zaidi za kusaidia utekelezaji wa SDG 14.

Takriban 60% ya mifumo ikolojia ya baharini duniani imeharibiwa au inatumika isivyostahili.
© Patrick Webster
Takriban 60% ya mifumo ikolojia ya baharini duniani imeharibiwa au inatumika isivyostahili.

Junhua anasisitiza kuwa, “Kufanikisha SDG14 kufikia mwaka 2030 kunahitaji takriban dola za Kimarekani bilioni 175 kila mwaka, lakini kwa bahati mbaya, chini ya dola bilioni 10 zilitengwa kati ya mwaka 2015 hadi 2019, jambo linalofanya SDG14 kuwa Lengo la Maendeleo Endelevu lililo na ufadhili mdogo zaidi.”

Aliongeza kuwa, “Mkutano wenyewe utapitisha tamko fupi, zenye lengo la kuchukua hatua, na pia utakusanya ahadi za hiari kutoka sekta zote, ambazo zitakuwa sehemu ya kile kitakachoitwa Mpango wa Hatua za Bahari wa Nice.”

Aidha, alibainisha kuwa “tamko la Kisiasa bado liko katika mchakato wa majadiliano unaoongozwa na Australia na Cape Verde. Rasimu hiyo inajikita zaidi katika utunzaji wa bahari na uchumi endelevu unaotegemea bahari, na inajumuisha hatua halisi za kuharakisha utekelezaji.”

Mkutano huu utajikita katika kutumia vyombo vilivyopo kuunda ushirikiano wenye mafanikio kuelekea kukamilisha na kutekeleza kwa ufanisi mchakato unaoendelea wa kuhifadhi na kutumia bahari kwa njia endelevu.

Junhua anasema: “Mkataba wa Paris wa mwaka 2015 uliweka malengo makubwa ya kupunguza ongezeko la joto duniani, na sasa, miaka kumi baadaye, tuna UNOC3 kushughulikia janga linaloikumba bahari yetu. Changamoto kama uchafuzi wa plastiki, uvuvi kupita kiasi, kupotea kwa bayonuai, uongezaji aside baharini, na joto la bahari vimeunganishwa sana, na pia vinaongeza kasi ya mabadiliko ya tabianchi. Hivyo basi, yote yanahitaji hatua za mabadiliko, tukizingatia pia upande wa binadamu.”

Li Junhua, Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Masuala ya Uchumi na Kijamii.
UN News/Heyi ZOU
Li Junhua, Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Masuala ya Uchumi na Kijamii.

Mkutano huu utahusisha wadau wote muhimu, ukiwaleta pamoja Serikali, mfumo wa Umoja wa Mataifa, mashirika ya kimataifa ya serikali, taasisi za kifedha za kimataifa, miili mingine ya kimataifa yenye nia, mashirika yasiyo ya kiserikali, mashirika ya kiraia, taasisi za kitaaluma, jamii ya wanasayansi, sekta binafsi, mashirika ya kifilantropia, Watu wa Asili na jamii za wenyeji, pamoja na wadau wengine kutathmini changamoto na fursa zinazohusiana na utekelezaji wa Lengo la 14.

Junhua anahitimisha kwa kusema, “ahadi za hiari ndani ya Mpango wa Hatua za Bahari wa Nice zitadhihirisha maono na dhamira ya serikali, wafanyabiashara, na jamii ya kiraia. Tunatumai Mkutano huu utachochea azma ya kipekee, ushirikiano wa kibunifu, na labda ushindani wa afya.”

Mkutano wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa wa mwaka 2025 wa kusaidia utekelezaji wa Lengo la Maendeleo Endelevu la 14: Kuhifadhi na kutumia kwa njia endelevu bahari, bahari kuu na rasilimali za baharini kwa maendeleo endelevu (Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Bahari 2025) utafanyika Nice, Ufaransa, kuanzia tarehe 9 – 13 Juni 2025, na utaandaliwa kwa pamoja na Ufaransa na Costa Rica.