Kuelekea Mkutano wa Bahari UNOC3, UNEP yatoa wito wa hatua madhubuti kukabili taka za plastiki
Kuelekea Mkutano wa Bahari UNOC3, UNEP yatoa wito wa hatua madhubuti kukabili taka za plastiki
Katika kuelekea Mkutano wa Tatu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Bahari UNOC3, utakaofanyika mjini Nice, Ufaransa kuanzia tarehe 9 hadi 13 Juni 2025, Ofisi ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira UNEP nchini Tanzania imetoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua za haraka na madhubuti kukabiliana na changamoto ya uchafuzi wa bahari, hasa wa taka za plastiki.
Akizungumza na Kituo cha Habari cha Umoja wa Mataifa nchini humo UNIC jijini Dar es Salaam, Clara Makenya, Mkuu wa Ofisi ya UNEP nchini Tanzania na Afisa Mawasiliano wa shirika hilo kwa Namibia, alisisitiza umuhimu wa kushughulikia kwa haraka tatizo la taka za plastiki ambazo nyingi hutokea nchi kavu na kuishia baharini.
“Kiwango kikubwa cha taka zinazoharibu bayoanuai ya bahari ni plastiki, na zinatoka nchi kavu. Viumbe wa baharini wanakufa, na takwimu zinaonyesha kuwa kufikia mwaka 2050, plastiki baharini zitazidi samaki kwa uzito,” amesema Makenya akiainisha masuala manne ya muhimu yanayohitaji kuzingatiwa
Hatua muhimu zinazopendekezwa:
1. Utekelezaji wa sheria za kitaifa na kimataifa:
Makenya amehimiza utekelezaji thabiti wa sheria zinazolenga kulinda bahari dhidi ya utupaji wa taka, akisema kuwa ni wakati wa kuyatumia kikamilifu makubaliano yaliyopo ili kudhibiti uchafuzi wa bahari.
2. Uwekezaji katika miundombinu ya maji na taka:
Amesisitiza haja ya serikali na mashirika kuwekeza katika miundombinu bora ya ukusanyaji na usimamizi wa taka ili kuhakikisha plastiki haziishii kwenye mito na hatimaye baharini.
3. Ulinzi wa maeneo maalum ya bahari (Marine Protected Areas):
Makenya amependekeza kuanzishwa kwa maeneo ya bahari chini ya ulinzi ili kulinda mazalia ya viumbe vya baharini dhidi ya madhara ya taka, hasa plastiki.
4. Ushirikiano wa kikanda na kimataifa:
Ametoa wito wa kuimarisha ushirikiano kupitia mikataba kama Biodiversity Beyond National Jurisdiction (BBNJ) na mkataba wa High Seas, ambayo inalenga kulinda bayoanuai ya bahari hata nje ya mipaka ya kitaifa.
Kauli ya Clara Makenya inajumuisha ujumbe wa wazi kwamba ikiwa dunia haitachukua hatua za haraka, mustakabali wa bahari na maisha yanayoutegemea viko hatarini.
Mkutano wa UNOC3 unatarajiwa kuwa jukwaa muhimu kwa nchi wanachama, mashirika ya kimataifa, sekta binafsi na jamii kushirikiana kwa vitendo kulinda na kutumia bahari kwa njia endelevu.