Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maelfu ya watu wakosa makazi jimboni Niger, nchini Nigeria kufuatia mafuriko makubwa: UN

Watu wanakimbia mafuriko makubwa huko Mokwa, Jimbo la Niger katikati mwa Nigeria.
© Nigerian Red Cross Watu wanakimbia mafuriko makubwa huko Mokwa, Jimbo la Niger katikati mwa Nigeria.

Maelfu ya watu wakosa makazi jimboni Niger, nchini Nigeria kufuatia mafuriko makubwa: UN

Tabianchi na mazingira

Umoja wa Mataifa na washirika wake wa kibinadamu wanaongeza msaada wa dharura kufuatia mafuriko makubwa yaliyotokea katika jimbo la Niger, nchini Nigeria wiki iliyopita, na kusababisha zaidi ya watu 3,000 kukosa makazi na kuathiri zaidi ya kaya 500.

Tarehe 29 Mei, mvua kubwa ilizusha mafuriko ya ghafla katika eneo la Mokwa, na kusababisha uharibifu mkubwa wa nyumba, miundombinu, na njia za kujikimu kimaisha. Kwa mujibu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu na misaada ya dharura OCHA, mamia ya nyumba zimeharibiwa, huku barabara na madaraja muhimu yakisombwa na maji, na hivyo kuvuruga usafiri na shughuli za kijamii.

Watoto ni miongoni mwa waathirika wakubwa

Watoto ndio walioathirika zaidi, huku Shirika la Umoja wa Mataiifa la Kuhudumia Watoto UNICEF, likiripoti kuwa zaidi ya watoto 1,600 walio na umri wa chini ya miaka 12 wamekosa makazi.

Katika taarifa yake iliyotolewa leo Nigeria OCHA imesema “Kuna uhitaji wa dharura wa chakula, maji safi, makazi ya muda, huduma za usafi na msaada wa kisaikolojia. Tunafanya kazi kwa karibu na Serikali ya Nigeria kusaidia juhudi za kutoa misaada.”

Mafuriko mabaya yamekumba mji wa Mokwa nchini Nigeria katikati mwa Jimbo la Niger.
© Nigeria Red Cross Mafuriko mabaya yamekumba mji wa Mokwa nchini Nigeria katikati mwa Jimbo la Niger.

Serikali inaongoza katika kutoa msaada wa haraka, ikiwa ni pamoja na chakula, maji, na huduma za matibabu. Mashirika kadhaa ya Umoja wa Mataifa yamejitokeza kuimarisha juhudi hizo ambapo

  • WHO Shirika la Afyala Umoja wa Mataifa  Duniani linajiandaa kupeleka dawa na vifaa vya matibabu ili kuhakikisha huduma za msingi za afya zinaendelea kutolewa.
  • IOM  ambalo ni Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji litasambaza mahema 1,000 ya plastiki na vifaa vingine vya msingi visivyo vya chakula kusaidia mahitaji ya makazi ya muda.
  • UNFPA ambalo ni Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu na Afya ya Uzazi linaanzisha kliniki za muda na maeneo salama kwa wanawake na wasichana, ambapo watapata huduma za afya ya uzazi na ya mama, msaada wa kisaikolojia, na vifaa vya staha. Shirika hilo pia linashirikiana na serikali kupeleka wauguzi na wakunga katika eneo lililoathirika.

Mafuriko ni tishio kubwa Nigeria sababu ya mabadiliko ya tabianchi

Mashirika hayo yameonya kuwa mafuriko yameendelea kuwa tishio sugu nchini Nigeria, hasa wakati wa msimu wa mvua, na mara kwa mara husababisha watu wengi kukosa makazi na kuharibu miundombinu.

Mashirika hayo ya kibinadamu yanaonya kuwa kutokana na mabadiliko ya tabianchi, matukio haya ya hali mbaya ya hewa yanazidi kuongezeka kwa kasi na ukali.

Wakati juhudi za kusaidia waathirika zikiendelea, maafisa wa Umoja wa Mataifa wanasisitiza umuhimu wa msaada endelevu ili kuzuia hali ya kibinadamu kuzorota zaidi, hasa kwa watu walio hatarini kama vile watoto, wanawake na wazee.