Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Annalena Baerbock kutoka Ujerumani ndiye Rais Mteule wa UNGA80; Ataja vipaumbele vyake

Annalena Baerbock, Rais Mteule wa mkutano wa 80 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA80 akihutubia wajumbe katika Baraza Kuu.
UN Photo/Manuel Elías
Annalena Baerbock, Rais Mteule wa mkutano wa 80 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA80 akihutubia wajumbe katika Baraza Kuu.

Annalena Baerbock kutoka Ujerumani ndiye Rais Mteule wa UNGA80; Ataja vipaumbele vyake

Masuala ya UM

Tutakuwa Bora Tukishikamana, ndio maudhui ya Annalena Baerbock, Rais Mteule wa mkutano wa 80 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, #UNGA80 utakaoanza rasmi mwezi Septemba mwaka huu wa 2025.

Bi. Baerbock ambaye ni raia wa Ujerumani, amechaguliwa leo na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa baada ya kupendekezwa na kundi la nchi za Ulaya Magharibi na nchi nyinginezo ambazo ndio zamu yao mwaka huu kushika Urais wa Baraza Kuu. Alipata kura 167 kati ya nchi 193 wanachama wa Umoja wa Mataifa.

“Tutakuwa Bora Tukishikamana, haya ndio maudhui ya kipindi changu cha Urais, maudhui ambayo yataongoza kazi yangu. Ninashukuru sana kusikia kwamba yanaendana na wengi wenu,” amesema Bi. Baerbock wakati akihutubia wawakilishi wa nchi 193 wanachama wa Umoja wa Mataifa baada ya kuchaguliwa.

Amenukuu kauli ya Katibu Mkuu wa Pili wa  Umoja wa Mataifa Dag Hammarskjöld, ya kwamba Umoja wa Mataifa haukuanzishwa ili kupeleka binadamu mbinguni, bali kuokoa binadamu kutoka jehanamu.

Amesema nukuu hiyo ni kumbusho thabiti ya kwamba shirika liliundwa kutoka kwenye majibu ya Vita Vikuu Vya Pili vya Dunia kwa lengo la kusongesha haki za binadamu, ushirikiano wa kimataifa, sheria ya kimataifa na kuishi pamoja kwa amani.

Nitamulika kinachotuunganisha na si kinachotugawanya

Ameeleza kuwa “leo hii tunaishi katika zama za changamoto kubwa. Tunatembea katika Kamba nyembamba ya ukosefu wa uhakika. Lakini kuzaliwa kwa Umoja wa Mataifa miaka 80 iliyopita, kunatukumbusha kwamba: Tumeshawahi kupitia zama ngumu zaidi. Na hivyo ni juu yetu kukabiliana na changamoto za sasa.”

Annalena Baerbock, Rais Mteule wa mkutano wa 80 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA80 akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kuteuliwa.
UN Photo/Eskinder Debebe
Annalena Baerbock, Rais Mteule wa mkutano wa 80 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA80 akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kuteuliwa.

Bi. Baerbock amekumbusha wajumbe kuwa nchi wanachama wanaweza kuwa wanatoka maeneo tofauti, historia tofauti. Wanaweza kuwa na mtazamo tofauti wa dunia na nyakati nyingine kutofautiana.

“Lakini tunapokaa pamoja Umoja wa Mataifa, tunaunganishwa na dira moja, na misingi iliyoasisi Umoja wa Mataifa,” amesema, huku akieleza kuwa Chata ya Umoja wa Mataifa imesalia na itasalia kuwa msingi wa kazi za Umoja wa Mataifa usioweza kusambaratishwa.

Ameeleza kuwa katika kipindi chake cha mwaka mmoja “nitazingatia zaidi yale yanayotuleta pamoja badala ya yale yanayotugawanya. Hii ni kwa sababu tunakuwa bora zaidi tukishikamana.”

Mambo makuu 3 ya kumulika

Ametaja mambo makuu matatu ambayo atayapatia kipaumbele kwa kuzingatia maudhui yake ya Tutakuwa Bora Tukishikamana.

Mosi: Kusaidia nchi wanachama kurejelea upya na kujikita zaidi ili kuhakikisha Umoja wa Mataifa unakidhi mahitaji ya karne ya 21. “Shirika hili linahitaji ufadhili wa kutosha na wa uhakika. Na wakati huo huo tunahitaji kuongeza ufanisi na tija katika mfumo mzima.

Pili:Kutekeleza kwa vitendo Mkataba wa Zama Zijazo kama njia mojawapo ya kufanikisha Ajenda 2030 ya Malengo ya Maendeleo Endelevu, SDGs.

“Watu duniani kote lazima wahisi kuwa kazi yetu inaleta mabadilik ohalisi kwenye maisha yao ya kila siku. Baraza Kuu ni chombo chenye uwakilishi mpana na hutunga será za Umoja wa Mataifa. Ni vema tutumie vema nafasi hii.”

Tatu: Mshikamano na kila mtu kwani amesema, “naona utofauti ndani ya Baraza Kuu kama uthabiti wetu. Hapa ni pahala ambako mataifa yote yanakutana na ambako kila nchi ina kiti na sauti. Nikiwa ndiye Rais, ninalenga kuhakikisha mitazamo hii tofauti inazingatiwa. Kila nchi mwanachama, kila ukanda na kila kundi linasikika.”

Amesisitiza kuwa uwazi na ujumuishi utakuwa ndio msingi.

Katibu Mkuu António Guterres akihutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ambalo limefanya uchaguzi wa Rais wa Baraza Kuu kwa Mkutano wa 80.
UN Photo/Manuel Elías
Katibu Mkuu António Guterres akihutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ambalo limefanya uchaguzi wa Rais wa Baraza Kuu kwa Mkutano wa 80.

Kauli ya Katibu Mkuu Guterres

António Guterres, ambaye ni Katibu Mkuu wa 9 wa  Umoja wa Mataifa ametumia hotuba yake kumpongeza Bi. Baerbock kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa #UNGA80 akisema “unaongoza katika kipindi ambacho mfumo wa ushirikiano wa kimataifa unakabiliwa na nyakati ngumu na zisizo na uhakika.”

Ametaja vita, janga la tabianchi,  umaskini, ukosefu wa usawa ambavyo amesema vinaendelea kukumba binadamu, bila kusahau kutoweka kwa kutokuaminiana, migawanyiko na utekelezaji wa SDGs ukienda mrama.

“Huu ndio wakati wa sisi kuungana, kusaka majawabu ya pamoja na kuchukua hatua kukabilia changamoto hizi,” amesema Katibu Mkuu.

Maudhui ya UNGA80 yana mashiko kutokana na changamoto za sasa

Na  ndipo akaunga mkono dira au maudhui ya #UNGA80 ya Bi. Baerbock ya Tutakuwa Bora Tukishikamana akisema “wito unaotoa hamasa katika dunia ya assa na mfumo wa kimataifa wa kutatua matatizo unaotumiwa na Umoja wa Mataifa kutatua changamoto hizo.”

Ametambua nyadhifa mbalimbali za Rais huyo mteule wa UNGA80 ikiwemo Uwaziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani akisema, “ni uzoefu wa kidiplomasia katika jukumu hili. Na hebu tusisahau historia muhimu ya yeye kuwa mwanamke wa 5 kuchaguliwa kuwa Rais wa Baraza Kuu. Rais-Mteule Baerbock, unaweza kutegemea uungwaji mkono kamilifu kutoka kwangu wakati huu unapobeba jukumu hili muhimu.”

Mkutano wa 80 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, #UNGA80  utaanza rasmi tareye 9 mwezi Septemba 2025 huku Mjadala Mkuu ukitarajiwa kuanza Jumanne ya tarehe 23 Septemba 2025.