Wapalestina hawapaswi kupoteza maisha wakisaka chakula- Guterres
Wapalestina hawapaswi kupoteza maisha wakisaka chakula- Guterres
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amesikitishwa sana na ripoti kuhusu wapalestina waliouawa na wengine walijeruhiwa wakati wakisaka msaada wa chakula huko Gaza, eneo la Palestina linalokaliwa kimabavu na Israeli.
Taarifa iliyotolewa Juni 2 jijini New York, Marekani na Msemaji wa Katibu Mkuu, imemnukuu akisema wapalestina wanahatarisha maisha yao kwa sababu ya kutafuta chakula hali isiyoubalika.
Taarifa hiyo imetoa wito wa uchuguzi wa haraka kuhusu tukio hilo na wahusika wawajibishwe.
Katibu Mkuu amesema Israeli ina wajibu wa kuheshimu sheria ya kimataifa ya kibinadamu na ifanikishe upatikanaji wa msaada wa kibinadamu na kuruhusu misaada kuingia bila vizuizi.
Taarifa hiyo imehitimishwa na ujumbe, “ninaendelea kutoa wito wa kusitishwa kwa mapigano mara moja, kwa njia ya kudumu na endelevu. Mateka wote lazima waachiliwe mara moja bila masharti yoyote. Hii ndiyo njia pekee ya kuhakikisha usalama kwa wote. Hakuna suluhisho la kijeshi kwa mzozo huu.”amesema Katibu Mkuu
OHCHR nayo yanukuu Wizara ya Afya ya Gaza
Mapema jana Jumapili Juni Mosi, Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa lilieleza kwamba mapema asubuhi Jeshi la Israel liliripotiwa kuwafyatulia risasi Wapalestina waliokuwa wakijaribu kufika kwenye vituo vya usambazaji wa misaada katika eneo la kaskazini-magharibi mwa Rafah.
Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Gaza, zaidi ya Wapalestina 200 wameathirika, wakiwemo watu 31 waliouawa na wengine wengi kujeruhiwa sana.
Mfumo wa mgao wa chakula Gaza ni sawa na ‘mtego’ wa kifo - UNRWA
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina, UNRWA limesema mgao wa msaada wa chakula hivi sasa huko Gaza, eneo la Palestina linalokaliwa kimabavu na Israeli umegeuka kuwa mtego wa kifo.
UNRWA imenukuu ripoti za wahudumu wa afya wa kimataifa waliokuwa eneo hilo huku ikisema kuwa kituo cha mgao wa chakula kinachoungwa mkono na Israeli na Marekani kiliwekwa Rafah eneo la mbali kusini.
“Mfumo huu unaodhalilisha umewalazimisha maelfu ya watu wenye njaa na waliokata tamaa kutembea kwa makumi ya kilometa kuelekea eneo ambalo limedarimiwa kutokana na mashambulizi mazito ya mabomu ya jeshi la Israeli,” amesema Lazzarini.
Shirika hilo limesema uwasilishaji na usambazaji wa misaada lazima ufanyike kwa kiwango kikubwa na kwa usalama.
Halikadhalika serikali ya Israeli ni lazima iondoe mzingiro na kuruhusu Umoja wa Mataifa kupata fursa ya kufikia kwa usalama na bila vizingiti ili misaada iweze kuingia na kusambazwa kwa usalama.
“Hii ndiyo njia pekee ya kuzuia njaa ya kiwango kikubwa ikiwemo kwa watoto milioni moja,” ameseam Mkuu huyo wa UNRWA akiongeza kuwa, “wakati huu ambapo simulizi zinazopingana na kampeni za upotoshaji zikiwa zimepamba moto, vyombo vya habari vya kimataifa vinapaswa kuruhusiwa kuingia Gaza ili kuripoti kwa uhuru kuhusu ukatili unaoendelea, ikiwemo uhalifu wa kikatili uliofanyika Jumapili asubuhi.