Tuzo ya Mandela ya UN 2025 yawatunuku mabingwa wa mabadiliko ya jamii kutoka Canada na Kenya
Tuzo ya Mandela ya UN 2025 yawatunuku mabingwa wa mabadiliko ya jamii kutoka Canada na Kenya
Umoja wa Mataifa leo umetangaza kwamba Brenda Reynolds, mfanyakazi wa kijamii kutoka jamii ya watu wa asili ya Saulteaux nchini Canada, na Kennedy Odede, mjasiriamali wa kijamii kutoka Kenya, ndiyo washindi wa Tuzo ya Nelson Rolihlahla Mandela ya mwaka 2025.
Tuzo hii maarufu inayotolewa kila baada ya miaka mitano inawatambua watu ambao maisha yao yanaakisi urithi wa hayati Nelson Mandela kiongozi wa zamani wa Afrika Kusini, hasa katika masuala ya haki, maridhiano na uwezeshaji wa jamii.
Brenda Reynolds na Kennedy Odede wametambuliwa kwa mchango wao mkubwa kwa jamii na kwa kuhamasisha Ulimwengu kufuata nyayo za misingi alishoishikiilia kiongozi huyo.
Kutambuliwa kimataifa kwa mashujaa wa kijamii
Tuzo hizo zitawasilishwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres pamoja na Rais wa Kikao cha 79 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Philémon Yang, tarehe 18 Julai 2025, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Nelson Mandela.
Kaulimbiu ya mwaka huu ya siku ya Mandela ni “Bado liko mikononi mwetu kupambana na umasikini na ukosefu wa usawa.”
“Tunapoadhimisha miaka 80 ya Umoja wa Mataifa, urithi wa Nelson Mandela wa maridhiano na mabadiliko unaendelea kutuhamasisha,” amesema Katibu Mkuu Guterres akiongeza kuwa “Washindi wa mwaka huu wa Tuzo ya Mandela wanaakisi moyo wa umoja na matumaini wakitukumbusha kuwa sote tuna uwezo wa kuimarisha jamii zetu na kujenga dunia bora.”
Sauti ya watu wa asili katika kujikwamua na maridhiano
Brenda Reynolds, mwanachama wa mkataba wa jamii ya watu wa asili wa Fishing Lake Saulteaux First Nation huko Saskatchewan, ametambuliwa kwa mchango wake katika afya na uponyaji wa watu wa jamii ya asili, hasa kupitia mpango wa msaada wa afya kwa manusura wa Shule za Makazi za Kikoloni au Indian Residential Schools.
“Naongea lugha mbili, lakini maneno hayawezi kuelezea shukrani zangu za dhati na mshangao wangu kupokea Tuzo ya Umoja wa Mataifa ya Nelson Rolihlahla Mandela,” amesema Reynolds.
Ameeendelea kusema kwamba “Mandela, ambaye nimemheshimu kwa muda mrefu kwa kazi yake ya maridhiano na kupinga ubaguzi wa rangi, alitambua kufanana kwa hali ya nchi yake na changamoto za watu wa asili. Daima nimehisi uhusiano wa kina naye.”
Kutoka mtoto wa mtaani hadi kiongozi wa mageuzi ya kijamii
Mshindi kutoka Kenya, Kennedy Odede, ndiye mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Shining Hope for Communities (SHOFCO), linalotoa huduma muhimu kwa watu zaidi ya milioni 2.5 kila mwaka katika mitaa ya mabanda nchini Kenya.
Akiwa na historia ya kuishi mitaani katika mtaa wa Kibera kwa miaka 23, Odede sasa anaongoza harakati kubwa za kijamii zinazowezesha jamii za kipato cha chini.
Amesema “Tuzo hii si yangu peke yangu ni ya jamii na uongozi wa mitaa unaotegemewa.”
Ameongeza kuwa “Nelson Mandela alitufundisha kuwa hadhi na haki huanzia chini. Tuzo hii inathibitisha imani yetu SHOFCO kwamba dawa mujarabu ya umasikini na ukosefu wa usawa tayari ipo ndani ya watu wanaoathirika zaidi.”
Urithi wa uwezeshaji wa ulimwengu
Washindi wa mwaka huu walichaguliwa kutoka miongoni mwa mapendekezo 331 yaliyowasilishwa kutoka nchi wanachama 66. Rais wa Baraza Kuu, Philémon Yang, ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya 2025, amesema tuzo hiyo inaonesha uhai wa maadili ya Mandela katika kukabiliana na changamoto za leo.
“Tuzo ya Mandela ya Umoja wa Mataifa ya 2025 haimheshimu tu Madiba, bali pia inathibitisha kuwa moyo wa ushirikiano wa kimataifa unaishi kupitia juhudi zisizochoka za washindi wake, watu wawili ambao maisha yao yanaakisi ujasiri wa kuongoza, unyenyekevu wa kuhudumu, na maono ya kuunganisha zaidi ya mipaka,” amesema Yang.
Kusherehekea maisha yenye mchango
Wakati wa hafla ya Julai, washindi watapokea tuzo ya glasi iliyoandikwa nukuu ya Nelson Mandela: “Cha muhimu katika maisha si ukweli kwamba tumeishi, bali ni tofauti gani tumeleta katika maisha ya wengine.”
Tuzo ya Nelson Rolihlahla Mandela ya Umoja wa Mataifa ilianzishwa kwa maazimio ya Baraza Kuu mmwaka 2014 na 2015. Hutolewa kila baada ya miaka mitano kwa washindi wawili, mwanamke mmoja na mwanaume mmoja kutoka maeneo tofauti ya kijiografia kama heshima kwa mafanikio na mchango wao wa kipekee kwa ubinadamu, katika kuakisi moyo wa Madiba.