Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Walinda amani wa UN kutoka Mongolia waokoa wakazi wa Abiemnhom, Sudan Kusini

UNMISS ikilinda Helkopyta iliyolazimka kutua kwa dharura
UNMISS
UNMISS ikilinda Helkopyta iliyolazimka kutua kwa dharura

Walinda amani wa UN kutoka Mongolia waokoa wakazi wa Abiemnhom, Sudan Kusini

Amani na Usalama

Kuelekea siku ya walinda amani Mei 29, tunakwenda nchini Sudan Kusini kumulika walinda amani na ulinzi wa raia. Katika taifa hilo changa zaidi duniani  walinda amani wa Umoja wa Mataifa kutoka Mongolia wanaohudumu kwenye Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo (UNMISS) walikuwa msaada mkubwa wakati kijiji cha Abiemnhom kaskazini mwa Sudan Kusini kilipovamiwa. 

Walinda amani wa Umoja wa Mataifa kutoka Mongolia wanaohudumu kwenye ujumbe wa umoja huo nchini Sudan Kusini, UNMISS walifika haraka  kutoka kituo chao cha karibu na kutoa msaada wa kuokoa manusura na miili ya waliouawa. 

Kamera inatusogeza kwenye eneo hili likiwa na nyumba za nyasi na Mawut Lueth anaeleza jinsi walivyosaidiwa na walinda amani.

“Wakati wa shambulio lililotokea asubuhi, watu walikimbia na kuogelea ili wavuke mto. Watu wengi, wakiwemo watoto na wanawake, walizama. Walinda amani kutoka Mongolia walitusaidia sana. Hata wakati wa mazishi, wao ndio walileta malori na kutusaidia kubeba maiti na kuwazika kwenye makaburi ya pamoja. Siku iliyofuata, watu walipohofia tena, tuliwaomba turuhusiwe kuingia kambini mwao, na walitukubalia.”

Sasa video inatuonesha msafara wa walinda amani wa UN kutoka Mongolia wakiwa kwenye msafara wa doria wakitumia magari. Meja Davaadorj Boldbaatar, Kamanda wa Kituo cha Muda cha Operesheni cha walinda amani wa Mongolia katika UNMISS hapa Abiemnhom anasema,

“Doria ina umuhimu mkubwa. Sio tu kufuatilia hali ya usalama, bali ni njia ya kujenga uhusiano na jamii. Kila doria ni nafasi ya kuzungumza, kusikiliza matatizo yao, na kujenga imani.”

Baadhi ya wakazi waliokuwa wamekimbia, kama Teresa Nyuol, sasa wamerudi nyumbani ingawa bado wana wasiwasi juu ya usalama wao wa kila siku.Bi Nyuol anasema.. “Tuko salama kwa sasa, lakini tunatamani waongeze idadi ya walinda amani kwenye kambi.”

Meja Davaadorj Boldbaatar akiwa kwenye kituo chao cha kuendesha operesheni huku walinda amani wakiwa wameketi juu ya vifaru na bendera ya umoja wa Mataifa ikipepea anatamatisha kwa kusema

“Mradi tu Ujumbe wa Umoja wa Mataifa utaendelea kuwa hapa, na mradi uwepo wetu utaweza kuchangia amani katika eneo hili, walinda amani wa Umoja wa Mataifa kutoka Mongolia wataendelea kutekeleza wajibu wao hapa Abiemnhom, Sudan Kusini.”