Ukuaji wa ajira duniani wapungua kutokana na mivutano ya kisiasa na kibiashara
Ukuaji wa ajira duniani wapungua kutokana na mivutano ya kisiasa na kibiashara
Katika toleo lake jipya la Mtazamo wa Ajira na Kijamii duniani, shirika la Umoja wa Mataifa la Ajira, ILO limebainisha kuwa mivutano ya kisiasa na hitilafu za kibiashara ni sababu kuu za kudhoofika kwa matarajio ya uchumi wa dunia, hali ambayo imesababisha kudorora kwa ukuaji wa ajira.
Ikiwa imetolewa leo huko Geneva, Uswisi, ripoti imepunguza makadirio ya awali ya ajira duniani kwa mwaka 2025, kutoka ajira mpya milioni 60 hadi milioni 53, ikimaanisha kuwa ukuaji wa ajira duniani umepungua kwa asilimia 0.2, huku pato ukuaji wa pato la ndani la taifa, GDP nao ukikadiriwa kukua kwa asilimia 2.8, badala ya asilimia 3.2.
Chanzo ni nini?
ILO inataja migogoro ya kibiashara hasa baina ya nchi na Marekani kuwa moja ya sababu za kupungua kwa ajira.
Mathalani inasema ajira zipatazo milioni 84 katika nchi 71 zinahusiana moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja na mahitaji ya walaji wa Marekani.
“Ajira hizi na kipato kinachotokana nazo, sasa ziko katika hatari kubwa kutokana na kuongezeka kwa migogoro ya kibiashara. Kanda ya Asia-Pasifiki ndiyo yenye sehemu kubwa ya ajira hizo. Hata hivyo, Canada na Mexico zina asilimia kubwa zaidi ya ajira zilizoathirika,” imesema ripoti hiyo.
“Tunajua kuwa uchumi wa dunia unakua kwa kasi ndogo kuliko tulivyotarajia. Ripoti yetu sasa inaonesha kuwa kama mvutano wa kisiasa na hitilafu za kibiashara vitaendelea, na kama hatutakabili masuala ya msingi yanayobadilisha taswira ya ajira, basi athari hasi kwa masoko ya ajira duniani haziepukiki,” amesema Mkurugenzi Mkuu wa ILO, Gilbert F. Houngbo.
Mgao wa GDP kwa wafanyakazi
Ripoti hiyo pia inaangazia mwenendo wa kushuka kwa mgao wa kipato kwa wafanyakazi.
Mathalani sehemu ya mapato ya wafanyakazi – yaani asilimia ya Pato la Taifa (GDP) inayokwenda kwa wafanyakazi – imeshuka duniani kutoka asilimia 53.0 mwaka 2014 hadi asilimia 52.4 mwaka 2024.
Afrika na Amerika ndizo zilizoathirika zaidi. Kama sehemu hii haingebadilika, mapato ya wafanyakazi duniani yangekuwa dola trilioni 1 zaidi mwaka 2024, sawa na dola 290 zaidi kwa kila mfanyakazi kulingana na uwezo halisi wa ununuzi.
“Kushuka huku kunachochea ongezeko la pengo la kipato na kuonesha kutokuwiana kati ya ukuaji wa uchumi na malipo kwa wafanyakazi,” imetanabaisha ripoti hiyo.
Ripoti inaeleza pia mabadiliko ya ajira kuelekea kazi zinazohitaji ujuzi wa hali ya juu. Wanawake wanaongoza mwelekeo huu. Kati ya mwaka 2013 hadi 2023, asilimia ya wanawake walioko katika kazi za ujuzi wa hali ya juu iliongezeka kutoka 21.2 hadi 23.2, wakati wanaume waliokuwa katika kazi hizo walikuwa karibu asilimia 18 mwaka 2023. Hata hivyo, kuna mgawanyiko wa kijinsia, ambapo wanawake hawawakilishwi vya kutosha katika sekta kama ujenzi, lakini wako kwa wingi katika kazi za usaidizi na huduma za malezi.
Watumishi wana elimu kupita kiasi
Ingawa viwango vya elimu vinaendelea kupanda duniani, soko la ajira bado linaathiriwa na kutolingana kwa elimu.
Kufikia mwaka 2022, ni asilimia 47.7 tu ya wafanyakazi waliokuwa na sifa zinazolingana ipasavyo na mahitaji ya kazi zao.
Idadi ya wafanyakazi wasio na elimu ya kutosha ilipungua kutoka asilimia 37.9 hadi 33.4 katika kipindi cha muongo mmoja uliopita, lakini wale waliokuwa na elimu ya juu kupita kiasi waliongezeka kutoka asilimia 15.5 hadi 18.9.
Teknolojia ya kisasa na ajira
Ripoti pia inazungumzia athari za teknolojia mpya katika dunia ya ajira, ikionesha kuwa karibu mfanyakazi 1 katika kila wafanyakazi 4 wanne anaweza kuona kazi yake ikibadilika kutokana na Akili Mnemba ya kizazi kipya, GenAI.
Kazi za ujuzi wa kati ndizo zilizo na kiwango kikubwa cha uwezekano wa kuathirika, lakini kazi za ujuzi wa hali ya juu ndizo zilizo na uwezekano mkubwa zaidi wa majukumu yao kuweza kufanywa na AI.
Hitimisho na mapendekezo
“Matokeo ya ripoti hii kuhusu hali ya ajira ni ya kufikirisha sana, lakini pia yanaweza kuwa dira ya kuunda ajira zenye staha. Tunaweza kuleta mabadiliko, kwa kuimarisha ulinzi wa kijamii, kuwekeza katika stadi za ujuzi, kukuza mazungumzo ya kijamii, na kujenga masoko ya ajira jumuishi ili kuhakikisha mabadiliko ya kiteknolojia yawanufaisha wote. Na lazima tufanye hivyo kwa haraka, kwa malengo makubwa, na kwa mshikamano,” ameelezea Mkurugenzi Mkuu.
Makadirio haya mapya ya ajira kutoka ILO, yanatokana na makadirio ya kiuchumi yaliyotolewa na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) katika Mtazamo wa Kiuchumi mwezi Aprili mwaka 2025.
Soma ripoti nzima hapa.