Vyombo vya habari na mchango wake wa kuelimisha malezi na makuzi ya watoto Tanzania
Vyombo vya habari na mchango wake wa kuelimisha malezi na makuzi ya watoto Tanzania
Kadri dunia inavyojiandaa kwa Mkutano wa Pili wa Dunia kuhusu Maendeleo ya Kijamii mwezi Novemba 2025, maadhimisho ya hivi karibuni ya siku ya familia duniani yalilenga katika kuhakikisha ni kwa vipi familia zinasongesha Malengo ya Maendeleo Endelevu, SDGs hasa kujengea uwezo familia katika kuimarisha malezi na makuzi ya watoto na jamii kwa ujumla.
Nchini Tanzania kilele cha siku ya familia kilikutanisha wadau wakimulika pamoja na mambo mengine nafasi ya vyombo vya habari katika kuimarisha malezi na makuzi ya mtoto.
Katika Kongamano la Malezi lililowakutanisha wadau wa malezi, Serikali, Mashirika yasiyo ya kiserikali na watoto huko Mwanza, kaskazini magharibi mwa Tanzania Chiku Lweno Meneja wa Mawasiliano na Uchechemuzi wa Shirika la lisilo la Kiserikali la Children in Crossfire alizungumza na Hamad Rashid, kutoka Redio washirika wetu, KidsTime Fm nchini humo.
Bi. Lweno anasema katika uhamasishaji wa malezi na makuzi ya watoto wadogo, vyombo vya Habari vimekuwa na nafasi kubwa.
"Katika maadhimisho ya siku ya Familia Maelekezo ya Sekretarieti ya Mpango wa Serikali wa Malezi na Makuzi ya watoto ulielekeza kila Mkoa, ufanye mdahalo wa masuala ya familia na malezi kwa kushirikiana na vyombo vya Habari, na kweli vyombo vya Habari viliripoti kilichojiri kama sehemu ya mchango wao Mkubwa" amesema Bi, Lweno.
Ameongeza kuwa "Mpango jumuishi wa serikali kuhusu malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto umetaja vyombo vya Habari kama sehemu muhimu ya kimkakati katika kufikisha taarifa kwa jamii na wadau mbalimbali kwanzia ngazi ya kitaifa mpaka ngazi ya familia.
Kwa vyombo vya Habari vina nafasi kubwa sana kuyafikia makundi haya kwa wakati mmoja na hili limechangia sana kuongeza uelewa katika jamii na kuibua hoja zinazoweza kupatiwa majawabu na serikali.
Tazama video kwa kina.