Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mgogoro wa Sudan wasababisha janga kubwa la wakimbizi duniani: WHO

Familia zilizofurshwa na vita, wakiwa na watoto, ambao walikimbia jimbo la Sennar kusini mashariki mwa Sudan wakiwa katika makazi ya muda jimboni Kassala.
© UNICEF/Ahmed Mohamdeen Elfatih
Familia zilizofurshwa na vita, wakiwa na watoto, ambao walikimbia jimbo la Sennar kusini mashariki mwa Sudan wakiwa katika makazi ya muda jimboni Kassala.

Mgogoro wa Sudan wasababisha janga kubwa la wakimbizi duniani: WHO

Afya

Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa Duniani WHO, limeonya kuhusu kuongezeka kwa janga la kibinadamu nchini Sudan, ambako mzozo unaoendelea umechochea zahma kubwa ya watu waliolazimika kukimbia makazi yao duniani.

Kulingana na ripoti ya kumi ya hali ya afya ya kikanda iliyotolewa na WHO leo zaidi ya watu milioni 14.5 wamelazimika kuhama, huku karibu milioni nne wakikimbilia nchi jirani zikiwemo Misri, Sudan Kusini, Chad, Ethiopia, Libya na Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR.

“Kiwango cha mateso nchini Sudan ni cha kushtua na kinaendelea kuwa kibaya zaidi kila siku,” amesema msemaji wa WHO mjini Geneva akiongeza kuwa “Hii si dharura ya kitaifa tu, ni janga la kikanda lenye athari za kiafya kwa dunia nzima.”

WHO imesema mfumo wa afya nchini humo umeporomoka huku mamilioni wakikimbia mapigano, wakikumbwa na magonjwa na janga la kibinadamu

Mfumo wa afya karibu kuporomoka

Kwa mujibu wa WHO mzozo huo, ambao sasa unaingia mwaka wa tatu, umeufikisha mfumo wa afya wa Sudan karibu na kuanguka kabisa.

Hospitali na vituo vya afya vimeharibiwa au havifanyi kazi, vifaa vya matibabu vinaisha, na wahudumu wa afya wanakimbia au wanafanya kazi katika mazingira hatarishi.

WHO, ikiwa ni shirika kiongozi wa sekta ya afya kwa mashirika ya kibinadamu, inaongoza uratibu wa washirika kujaribu kukidhi mahitaji ya kiafya kwa mkakati katikati ya hali ya sintofahamu.

“Tunajitahidi kudumisha huduma muhimu na kudhibiti milipuko ya magonjwa, lakini miundombinu na rasilimali zimeelemewa kupita kiasi,” linasema shirika hilo.

Magonjwa yatishia katika kambi zilizofurika

Hatari za kiafya zimevuka mipaka ya Sudan limesema shirika la WHO likiongeza kuwa  “Wakimbizi wanaoingia nchini Misri, Sudan Kusini, Chad, Ethiopia, Libya na Jamhuri ya Afrika ya Kati wanakumbwa na  changamoto ya kambi zilizojaa pomoni, makazi ya muda yasiyo rasmi, na upungufu wa huduma muhimu.”

Hali hizi ngumu, kwa mujibu wa WHO ni pamoja na ukosefu wa maji salama na usafi wa mazingira, ambavyo vimeunda mazingira ya kuenea haraka kwa magonjwa ya kuambukiza.

WHO inaonya kuwa bila hatua za haraka, milipuko ya magonjwa inaweza kuenea kwa kasi. “Katika hali hizi chafu na zilizojaa watu, hata magonjwa yanayotibika yanaweza kuwa ya mauti,” shirika hilo limeeleza.

Mahitaji ya kibinadamu yafikia kiwango cha juu

WHO imesema mahitaji ya dharura ya kibinadamu yanajumuisha maji safi, chakula, makazi, huduma za afya, na bidhaa muhimu za msaada.

Mashirika ya kibinadamu yanakumbwa na changamoto kubwa za utoaji wa misaada kutokana na uhaba wa fedha na ukosefu wa usalama.

“Mgogoro huu unahitaji hatua za haraka na za pamoja,” WHO imesisitiza. “Maisha yako hatarini kila tunapochelewa kuchukua hatua.”

Dharura ya kikanda yahitaji hatua za kimataifa

Kwa kuwa mgogoro huu umeenea nje ya mipaka ya Sudan, WHO inatoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuongeza msaada kwa Sudan na nchi jirani zinazowapokea wakimbizi.

“Afya na utu wa mamilioni ya watu uko hatarini. Tunapaswa kuchukua hatua sasa kabla hali haijawa janga litakalohitaji miongo mingi kurekebisha.”