Ujumbe wa UN walaani shambulio la Urusi dhidi ya Ukraine
Ujumbe wa UN walaani shambulio la Urusi dhidi ya Ukraine
Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa Ufuatiliaji wa Haki za Binadamu nchini Ukraine (HRMMU) umelaani wimbi la mashambulizi makali ya makombora yaliyofanywa na Urusi kwa kutumia ndege zisizo na rubani au droni dhidi ya Ukraine, mashambulizi yaliyosababisha vifo vya takribani watu 13 na kujeruhi wengine 65.
Taarifa iliyotolewa Jumapili huko Kyiv, Ukraine imenukuu ujumbe huo ukionya kwamba shambulio hilo la Jumamosi kuamkia Jumapili linaonesha hatari kubwa ya matumizi ya silaha zenye mlipuko mkubwa katika maeneo yenye watu wengi.
Kwa mujibu wa ujumbe huo wa UN, mashambulizi hayo ni miongoni mwa makubwa zaidi tangu uvamizi kamili wa Urusi mnamo Februari 2022 – yalisababisha vifo vya raia na uharibifu wa makazi na miundombinu katika mikoa 10 ya Ukraine, ikiwa ni pamoja na mji mkuu, Kyiv.
Watoto watatu walikuwa miongoni mwa waliouawa na watoto tisa waliripotiwa kujeruhiwa. Ujumbe huo kwa sasa unaendelea kuthibitisha idadi kamili ya waathiriwa pamoja na athari mbayá kubwa zaidi za shambulio hilo.
"Kwa watu angalau 78 kuripotiwa kuuawa au kujeruhiwa kote nchini, shambulio la usiku wa kuamkia leo linaonesha kwa huzuni hatari ya kila mara kwa raia kutokana na matumizi ya silaha zenye nguvu katika maeneo ya mijini, hata yale yaliyo mbali na eneo la mbele zaidi kwenye mapigano," amesema Danielle Bell, Mkuu wa HRMMU, katika taarifa kwa vyombo vya habari siku ya Jumapili.
"Ni ongezeko lingine kwa idadi kubwa ya athari za kibinadamu ambazo vita hivi vinaendelea kusababisha kwa raia, na sasa familia zaidi kote nchini zinaomboleza wapendwa wao."
Hakuna mahali salama
Matthias Schmale, Mratibu wa Masuala ya Kibinadamu wa UN nchini Ukraine, pia ameeleza wasiwasi mkubwa juu ya mateso ya raia.
"Nimeshtushwa kuona kwamba tena raia – wakiwemo watoto – wameuawa katika mashambulizi makubwa ya usiku wa kuamkia leo," amesema katika taarifa iliyowekwa kwenye ukurasa wa mitandao ya kijamii X.
"Kote Ukraine, hakuna mahali salama. Nyumba na miundombinu ya kiraia vimeathirika. Tunawashukuru mashirika ya misaada ya kibinadamu na huduma za serikali kwa msaada wa haraka kwa watu walioathirika. Raia kamwe hawapaswi kuwa walengwa."
Matumizi ya silaha za masafa marefu
Mamlaka za Ukraine zimeripoti kuwa jeshi la Urusi lilirusha angalau makombora na silaha 367 za kujifyatua zenyewe wakati wa usiku, katika shambulio lililoratibiwa kwa kutumia mifumo ya ardhini, baharini na angani.
Shambulio hilo lilifuatia lingine kama hilo usiku uliotangulia, ambalo lililenga zaidi eneo la Kyiv, mji mkuu wa Ukraine.
HRMMU imeeleza kuwa matumizi ya silaha za masafa marefu katika maeneo ya mijini yamekuwa sababu kuu ya vifo vya raia katika miezi ya Machi na Aprili mwaka huu. Ingawa idadi ya vifo ilikuwa imepungua kidogo mwezi Mei kabla ya shambulio la hivi karibuni, madhara ya mashambulizi ya wikendi hii yataongeza takwimu za kila mwezi.