Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkimbizi wa Haiti aliyepata faraja na matumaini Mexico

Watu wanne wakiwa na mikoba ya mgongoni wakiondoka kwenye kamera wakivuka barabara ya vumbi huko Guatemala. Nyuma, kuna malori na miti ya kitropiki. Picha inahusiana na uhamaji wa binadamu na wanaotafuta hifadhi.
© UNHCR/Nicolo Filippo Rosso Wasaka hifadhi wakivuka Guatemala katika safari yao ya kaskazini kuelekea Mexico, Marekani na Kanada.

Mkimbizi wa Haiti aliyepata faraja na matumaini Mexico

Wahamiaji na Wakimbizi

Wakati raia wa Haiti Giovanni Rotschild alipowasili Mexico mwaka 2022 baada ya safari ndefu isiyo na uhakika kutoka nchi mwake kulikosheheni ghasia, hakufahamu mtu yeyote wala hakuzungumza kabisa lugha ya kispanyola. Lakini msaada alipata msaada kumwezesha kujenga upya maisha na kupata jamii mpya.

Giovanni huyu akiwa Mexico ambapo kupitia video ya shirika la Umoja wa MAtaifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR anaeleza kuwa huko nyumbani Haiti maisha yalikuwa ya kawaida na alikuwa anafuatilia masomo yake kama kawaida.

Hali ilibadilika pale Giovanni ambaye alikuwa muuguzi alipopokea vitisho kutoka magenge ya uhalifu na hivyo kulazimika kukimbilia Mexico akiacha nyuma mama yake na mpendwa wake.

Mexico amejifunza lugha ya kispanyola na kupata ajira kwenye gari la kusambaza vinywaji baridi kwenye mji mkuu Mexico City. Giovanni ambaye sasa ametambuliwa rasmi kama mkimbizi Mexico anasema,,,

Kila ninapokuwa njiani jambo zuri linatokea. Ninazidi kuifahamu Mexico. Ninakutana na watu wapya, ninapata uzoefu mpya.”

Ukata unasababisha UNHCR ishindwe kutekeleza ipasavyo programu zake za ujumuishi wa wakimbizi, akiwemo Giovanni. Ingawa hivyo sekta binafsi sasa imekuwa mstari wa mbele kuwezesha wakimbizi kujumuishwa kijamii na waweze kujitegemea. Sasa Giovanni amepata ukazi wa kudumu Mexico.

“Nimefurahi sana kupata ukazi wa kudumu. Sasa naweza kuishi bila hofu, wala tatizo. Ninajihisi huru. Ninaweza kufanya kila kitu kisheria. Na ninajiona siku za usoni nitakuwa mkurugenzi wa shirika linalosaidia wengine na kuokoa maisha kama nilivyookolewa mimi.”

Giovanni ni miongoni mwa wahaiti 7,537 waliopatiwa hadhi ya ukimbizi Mexico kati ya 2019 hadi Juni 2024.