Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuondolewa vikwazo dhidi ya Syria ni hatua muhimu kwa mustakabali wa taifa hilo - UN

Mtazamo mpana wa mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya Syria. Wanachama pia walipata maelezo mafupi na Geir Pedersen (kwenye skrini), Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu wa Syria.
UN Photo/Manuel Elías
Mtazamo mpana wa mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya Syria. Wanachama pia walipata maelezo mafupi na Geir Pedersen (kwenye skrini), Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu wa Syria.

Kuondolewa vikwazo dhidi ya Syria ni hatua muhimu kwa mustakabali wa taifa hilo - UN

Amani na Usalama

Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Syria, Geir O. Pedersen, amekaribisha kwa moyo mkunjufu  matangazo ya kuondoa vikwazo vya kimataifa dhidi ya Syria, akieleza ni hatua ya kihistoria ambayo ina uwezo wa kuboresha kwa kiasi kikubwa hali mbaya ya kibinadamu na uchumi nchini humo.

Hata hivyo, Pedersen ambaye alikuwa anahutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa njia ya video kutoka Damascus, Syria ameonya kuwa changamoto kubwa za usalama na muundo wa kiuchumi bado zinatishia mabadiliko ya kisiasa ya Syria ambayo ni tete.

Baraza la usalama limekutana leo ikiwa ni utaratibu wake wa kukutana kila mwezi kujadili Hali ya Kisiasa na Kibinadamu nchini Syria.

Katika mfululizo wa matukio muhimu yaliyotokea hivi karibuni, Marekani, Muungano wa Ulaya na Uingereza wametangaza kuondoa vikwazo vya muda mrefu dhidi ya Syria, hatua ambayo Pedersen amesema imesherehekewa kwa furaha na wasyria.

Mwanamke akiwa ameshikilia bendera mpya ya Syria  nje ya Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani wakati wa tukio la kuipandisha kwa mara ya kwanza kwenye eneo hilo.
UN Photo/Mark Garten
Mwanamke akiwa ameshikilia bendera mpya ya Syria nje ya Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani wakati wa tukio la kuipandisha kwa mara ya kwanza kwenye eneo hilo.

Kuondolewa vikwazo kutafungua milango ya ustawi

"Nimekuwa nikitoa wito wa hatua dhabiti juu ya vikwazo, kama ilivyofanywa na mamilioni ya wasyria, haya ni maendeleo ya kihistoria. Yanashikilia uwezo mkubwa wa kuboresha hali ya maisha na kusaidia mchakato wa kisiasa wa Syria."

Mjumbe huyo Maalum pia amepongeza msaada wa kiuchumi na jitihada za msamaha wa madeni kutoka Saudi Arabia, Uturuki, na Qatar, akisema jitihada hizi ni kwa ajili ya kusaidia kuimarisha uchumi wa Syria kwa kusaidia mishahara ya sekta ya umma, kutatua majukumu ya kifedha ya kimataifa, na kutoa rasilimali muhimu za nishati.

Uchumi umedamirika hatua endelevu wahitajika

Licha ya mafanikio haya, Pedersen amesisitiza kuwa njia mbele bado ina changamoto kubwa. "Syria inakutana na changamoto kubwa za kimfumo, ikiwa na uchumi ulioathiriwa vibaya na vita vya zaidi ya muongo mmoja," ameonya. "Kufufua uchumi uliodamirika kutahitaji hatua endelevu kutoka kwa mamlaka za mpito—hasa katika mageuzi ya utawala na mifumo ya kifedha—kwa msaada unaoendelea kutoka kimataifa."

Wavulana wanacheza katika kambi isiyo rasmi nchini Syria.
© UNICEF/Rami Nader
Wavulana wanacheza katika kambi isiyo rasmi nchini Syria.

Wasyria wameonesha mnepo, jamii ya kimataifa sasa ichukue hatua - OCHA

Katika kikao hicho, Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Misaada ya Dharura, OCHA, Tom Flesher amesema hali ya kibinadamu Syria ni mbayá ambapo zaidi ya watu milioni 16.5 wanahitaji msaada wa dharura.

Katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba na Ramesh Rajasingham ambaye ni Mkuu wa Ofisi ya OCHA mjini Geneva, Uswisi, Fletcher ametaja mambo makuu matatu ya ambayo Baraza linapaswa kutambua. Mosi; mahitaji ya kibinadamu na ulinzi wa raia; Pili; licha ya changamoto operesheni za kiutu zimeendelea na kufikia mamilioni ya watu; Tatu; Ukata unatishia kurejesha nyuma mafanikio yaliyopatikana ikiwemo huduma za afya.

Hivyo amesema “jumuiya ya kimataifa lazima ichukue hatua haraka kufikia wahitaji. Wakati huu wananchi wa Syria wamendelea kuonesha mnepo, jumuiya ya kimataifa lazima ichukue uamuzi madhubuti wa kuwapatia msaada unaohitajika, ili waweze kujenga maisha yao na kupata utulivu wa kudumu.”