Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Katika kipindi cha mwezi mmoja zaidi ya wakimbizi 25,000 wa Sudan Kusini wamekimbilia Sudan: UNHCR

Watu wanaokimbia ghasia nchini Sudan wawasili Renk nchini Sudan Kusini.
© UNHCR/Ala Kheir
Watu wanaokimbia ghasia nchini Sudan wawasili Renk nchini Sudan Kusini.

Katika kipindi cha mwezi mmoja zaidi ya wakimbizi 25,000 wa Sudan Kusini wamekimbilia Sudan: UNHCR

Amani na Usalama

Nchini Sudan Kusini, kuzuka upya kwa mapigano kati ya wafuasi wa Rais na Makamu wa Kwanza wa Rais kumesababisha kuhama kwa idadi kubwa ya watu ambapo zaidi ya Wasudani Kusini 25,000 wamevuka mpaka ndani ya mwezi mmoja na kuomba hifadhi nchi Jirani ya Sudan ambayo nayo inakumbwa na vita.

Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR, jimbo la White Nile nchini Sudan limeshuhudia ongezeko kubwa la wakimbizi na waomba hifadhi kutoka Sudan Kusini tangu tarehe 8 Aprili 2025, wengi wao wakiwa wanawake na watoto.

UNHCR inasema takwimu zilizokusanywa kufikia tarehe 6 Mei 2025 zinaonesha kuwa raia 25,400 wa Sudan Kusini wameingia Sudan tangu mwanzo wa Aprili kutokana na hali ya machafuko na ukosefu wa usalama nchini mwao. Hii inafanya jumla ya wakimbizi wa Sudan Kusini katika Jimbo la White Nile kufikia zaidi ya 435,000.

Wengi wa wakimbizi hawa wapya wametoroka kutoka miji ya Wad Dakona, Aborje, Tonja, Kadok, Malakal, Wau Shilluk, Auya, Wantong, Renk na Algaigar, katika Jimbo la Upper Nile la Sudan Kusini.

"Raia wanaokimbia mapigano wanavuka mipaka kupitia maeneo ya Almeginis, Alkuaeik na Joda," imesema UNHCR katika ripoti yake.

Ukosefu wa usalama na vurugu za Kijamii

Idadi kubwa ya waliokimbia upya wanatoka katika makabila ya Nuer na Shilluk. "Ukosefu wa usalama, machafuko ya kijamii na kuzorota kwa hali ya kibinadamu katika Jimbo la Upper Nile vimetajwa kama sababu kuu za watu hao kukimbia makazi yao."

Hishirika hilola wakimbizi limesema “Baada ya miaka saba ya utulivu wa kiasi, mapigano yalizuka tena katikati ya Februari kati ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Sudan Kusini SSPDF na Jeshi la White Army, ambalo ni kundi la wanamgambo wa kujilinda linalomuunga mkono Makamu wa Kwanza wa Rais Riek Machar.”

Viongozi hao wawili, Rais Salva Kiir na Riek Machar, walikuwa wapinzani wakuu wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyofuatia uhuru wa taifa hilo changa mwaka 2011.

Kwa mujibu wa UNHCR, mji wa Kosti katika Jimbo la White Nile umelengwa na mashambulizi ya ndege zisizo na rubani katika wiki za hivi karibuni. "Ingawa mji haujashambuliwa moja kwa moja, kuna hatari kubwa ya kuzuka kwa hali ya kutoelewana, ukimbizi wa ndani, na vizuizi vya upatikanaji wa misaada ya kibinadamu." Limeonya shirika la UNHCR

Maeneo ya ziada kwa ajili ya wakimbizi wapya

Aidha, uwepo wa makundi yenye silaha na mashambulizi ya hivi karibuni kaskazini mwa mji wa Al-Gitaina, katika Jimbo la White Nile, umesababisha "ongezeko la hofu miongoni mwa jamii zinazowahifadhi wakimbizi na kusababisha wimbi kubwa la wakimbizi wa ndani kuelekea mji wa Al-Gitaina. Ukosefu wa utulivu katika Jimbo la Upper Nile unachangia pia ongezeko la watu kuvuka mpaka kuingia Sudan.”

Haya yote yanachochea mahitaji makubwa ya kibinadamu na kuonyesha athari za ukosefu wa usalama wa ndani na wa kuvuka mipaka kwa nchi ya Sudan, hasa katika Jimbo la White Nile.

UNHCR na washirika wake nchini Sudan wamebaini makazi ya pamoja yaliyopo katika kambi za wakimbizi za Aljameya na Khor Alwaral, pamoja na ardhi ya ziada katika kambi ya wakimbizi ya Um Sangour kwa ajili ya kuwahifadhi waliowasili.

Shirika hilo limesisitiza kkuwa "Rasilimali za ziada zinahitajika ili kuiwezesha UNHCR kuboresha na kupanua huduma za maji, usafi wa mazingira, afya na makazi kwa ajili ya wakimbizi wapya."